Hadhira ya wote 12-1-1977
Mt. Paulo VI
Katika hadhira ya watu wote ya Jumatano, Januari 12, Baba Mtakatifu Paulo VI alitamka hotuba ifuatayo:
“Tunawasalimu ninyi nyote ‘in nomine Domini’ (katika jina la Bwana)
Ingawa kipindi hiki cha mwaka -tupo katikati ya msimu wa baridi- hakifai kwa hija, matembezi, ziara na mikutano, hata hivyo, tunasikia shangwe ya kuweza kuwasalimu kwa mara nyingine tena katika ukumbi huu, ambao unaheshimiwa na uwepo mkubwa hivi wa wageni ambao sasa tutawataja.
Jueni kwamba tunawasalimu nyote kwa kweli, tukifahamu kuwa wabebaji na wasambazaji wa baraka inayotuzidi, yaani, kuwa wawakilishi na watumishi wa neema kutoka kwa Bwana, ambayo tungependa kuwagawia watu wote; na kuiwasilisha, haswa, kwa maana ya muungano huo, ya upendo huo, ya mmiminiko huo wa roho na ya umoja huo, inayotutofautisha kwa imani yetu na kwa bahati iliyoje, ambayo sisi sote tunayo, ya kuwa ndani ya Mwili wa kifumbo wa Kristo.
Kwenu nyote, basi, salamu zetu na baraka yetu. Tutasindikiza, baadaye, na sala zetu na kwa kumbukumbu ya kiroho, wakati huu mnaotupatia, mnapotutembelea, katika furaha ya kuwa pamoja na ya kuwa pamoja na Kristo.
Kwa mridhiko na hisia kubwa kwa upande wetu, tunalo hapa kundi maalum la maaskofu, ambao tutasalimia, ili tusirefushe mno utangulizi huu kwa Hadhira Yetu, baadaye, kando, katika chumba kinachofuata … Lakini, ili mjue, angalau, asili ya maaskofu hawa na umuhimu wa ndugu hawa zetu katika uaskofu, ambao tunayo heshima ya kuwa nao leo pamoja nasi, tutasoma, kama ilivyopendekezwa kwetu, asili yao.
Tuna maaskofu wawili kutoka Mexico; tuna askofu mmoja kutoka El Salvador, kutoka Guatemala, kutoka Honduras, kutoka Jamhuri ya Dominikani; pia, maaskofu wawili kutoka Brazil, kutoka Ecuador, kutoka Peru, kutoka Uruguay, kutoka Ufilipino; tuna askofu mmoja kutoka Uingereza, mmoja kutoka Uhispania, mmoja kutoka Ureno na wengine zaidi kutoka Italia, ambao ni: askofu mkuu wa Rossano, askofu wa Sarzana na Burgnato, wa Macerata na Tolentino, wa Fabriano, wa Rieti, wa Térano, wa Crotone na, hatimaye, wa Piazza Armerina.
Angalieni kwamba ni Hadhira, ambayo ina kweli hulka ya kikatoliki, tungesema kiekumene, lakini ya kikatoliki inamaanisha bado zaidi, kwa sababu ni utimilifu uliyotekelezwa na kukamilika tayari. Kwa hiyo, tunawasalimu ndugu hawa wote, tukitafuta kusoma moyoni mwao sababu ya kuja kwao na kuitikia, kwa usikivu wetu wote na mhimizo wetu, kwa tendo hili lao lenye maana kubwa hivi ya fumbo lake.
Wanasindikiza kundi hili kubwa, ambalo sasa tutataja, na ambao tumewabakizia hotuba fupi, ambayo huwa tunatoa katika Hadhira za watu wote. Narudia. Tunawasalimu maaskofu hawa wote na, karibu niseme, tunawakumbatia; tumeunganika sana hivi, kwa uwepo wao, katika kuheshimu Kanisa letu Takatifu, na kumheshimu Yesu Kristo, kwa kuwa na hamu ya kitume ya kuzifikia roho za watu, jinsi zilivyo leo ulimwenguni, na pia katika tumaini tunaloshiriki, linalodumu katika nyakati na kuzizidi nyakati, hadi kufikia eskatolojia ya mwisho ya mkutano mtimilifu wa kuonekana pamoja na Bwana wetu Yesu Kristo.
Kwa ajili yao, kwa hiyo, shukrani zetu za dhati, kwa ushiriki wao katika Hadhira hii, na salamu na baraka zetu, ambazo zinataka pia kuwafikia, mzipeleke, basi, ndugu wapendwa katika uaskofu, katika majimbo yenu. Tunajua, kwa kweli, kwamba sala, matamanio na tumaini la pamoja katika Kristo, zinasindikiza matakwa yetu haya.
Sasa, basi, tunatoa salamu, kwanza kabisa, kwa kundi kubwa, linalounda sehemu kubwa ya Hadhira hii. Tutawaambia kitu baadaye. Ni maparoko na wamisionari walei kutoka Jumuiya za Neokatekumenato. Wanatoka nchi tofauti na, kama mnavyoona, wanaunda jumuiya yenye watu wa aina mbalimbali: mapadre, watawa, walei, nk. Tunawakaribisha ninyi nyote kwa moyo. Baadaye tutasema baadhi ya maneno kwa ajili ya tukio hili na kwa nia inayowakusanya na kuwafanya kukiri imani yao katika Kanisa na, hatimaye, tutawapa baraka yetu maalum. Tunarudia: Jumuiya za Neokatekumenato kutoka mabara na nchi mbalimbali.
Tunawasalimu sasa, tukiwapa zawadi hii ndogo, tuseme hivyo, ambayo sisi kawaida tunatoa katika Hadhira yetu ya watu wote, yaani, neno moja; neno ambalo lingependa baadaye kuwa kitu cha kutaamuli, cha kutafakari au, angalau, thibitisho la ukaribu wetu kwa anayelisikiliza.
Uwepo katika Hadhira hii ya kundi dhahiri hivyo kwa idadi yake -karibu ni ninyi tu mliopo hapa- na kwa sababu ya hadhi ya washiriki -viongozi wenu na, zaidi ya yote, kikundi cha maaskofu ambao mmeleta pamoja nanyi- walio ndani ya Jumuiya za Neokatekumenato, inatupa fursa ya kuchukua umakini wa wageni wetu na wa wale wanaosikia neno hili letu linalojulikana, kwa kipindi hiki, kuhusu matukio mawili katika Kanisa la kikatoliki.
La kwanza ni Sinodi ya Uaskofu ya mwaka 1974, miaka mitatu iliyopita, ambayo wakati huo mada yake ilikuwa “Uinjilishaji”; uinjilishaji katika wakati wetu: jinsi ya kufanya leo, ili kueneza Injili. Hii ilikuwa mada ya Sinodi ya 1974, ambayo ilileta maudhui kwa ajili ya Wosia wetu wa Kitume uliofuata, “Evangelii Nuntiandi“, ambao ulichapishwa mnamo Desemba 8, 1975. Ikiwa tungekuwa na hamu ya kutangaza hati zetu, karibu tungependa kuipendekeza. Kwa nini? Kwa sababu imejaa sana, inaheshimu sana kila kitu ambacho Maaskofu katika Sinodi – imetaka kufasiri, kukusanya na kupanga mawazo yao yote, kufanya lugha yao kufikika, rahisi iwezekanavyo, lakini, wakati huo huo, iliyo muhimu na wazi zaidi iwezekanavyo-, kiasi kwamba inatufanya, narudia, kuipendekeza haswa kwenu, ambao mnataka kuwa “Wakatekumeni Wapya (Neo-katekumenato)”, yaani, kwamba mnataka kufunza na kuinjilisha umati huo mkubwa wa mataifa, ambao mnafanikiwa kuwavutia. Nadhani mngefanya huduma nzuri, kwa ajili yenu, kama vile kwa wafuasi na wanafunzi wenu.
Tukio la pili ni la baadaye, bado, kwa maana itafanyika mwaka huu, kuanzia Septemba 30: Sinodi ya Maaskofu ijayo. Tutakuwa hapa na maaskofu takriban mia mbili, kutoka sehemu zote za dunia, wakiteuliwa na Mabaraza yao ya Maaskofu. Mada itakuwa ipi? Tena, mada ya Uinjilishaji, katika kipengele kingine, ambacho ni cha katekesi, yaani, jinsi ya kufundisha dini, hasa kwa watoto, wabalehe, vijana na pia kwa wanaume waliokomaa, katika wakati huu wa ustaarabu wetu; jinsi ya kufika kuwa walimu wa katekisimu. Maaskofu ndio waliotaka mada hii. Tutaichukua tena na tutaiendeleza. Hii nawaambia ili mwone jinsi ninyi, wakatekumeni, ni wa leo.
Hii inaonyesha hadi wapi ufahamu wa utume wa msingi wa Kanisa, ambao ni kueneza ujumbe wa kiinjili, kulingana na amri ya mwisho ya Yesu, mwishoni mwa uwepo wake wazi duniani – maneno yake yalikuwa yapi? Nendeni mkahubiri!, “Nendeni mkafundishe mataifa yote”-, Ufahamu huu, narudia, uko macho na hai katika Kanisa letu la leo. Ni mara ngapi, wakati wa kuchunguza historia ya zamani, iliyoathiri mihula ya historia ya Kanisa, inasemwa: “Lakini walishughulikia nini?”
Kulikuwa na vita kati ya mataifa fulani, au vile kulikuwa na maswali maarufu ya kidogma, nk, ambayo yalivutia, ndiyo na hapana, maoni ya watu na utume wa kichungaji. Kanisa limerudi tena katika kazi zake na kazi majukumu yake ya kichungaji. Na jukumu la kwanza la kichungaji ni kutangaza Injili, kwenda kukutana na ulimwengu na kusema: “Angalia, nakuletea ujumbe”; ujumbe ambao malaika walileta duniani: “Utukufu kwa Mungu na Amani duniani”; na kisha ujumbe wa Kristo wa kutangaza Injili, yaani, neno jema, Yesu Kristo alilotufundisha.
Ufahamu huu, narudia, uko macho na unatenda kazi katika Kanisa leo na kulihusisha kabisa. Hiki ni kitu kizuri ajabu: wahudumu, yaani, maaskofu, mapadre, watawa, wa kiume na wa kike, nk. Na waumini, waumini wenyewe wanageuka sauti hiyo ambayo lazima ieneze ujumbe huu; ujumbe wa tangazo la kiinjili ambalo leo, kuliko wakati mwingine wowote, unastahili kutangazwa kwa sababu mbili, ambazo inaonekana zinapingana kati yao. Kwanza: tunapaswa kuitangaza kwa sababu ulimwengu wa leo ni kiziwi na tunahitaji kupaza sauti, tunahitaji kupata namna ya kufanya tueleweke, tunahitaji kusisitiza, tunahitaji kuwaita wote kwenye shule mpya, nk. Ugumu unatusisimua, unakuwa kichocheo, ambacho kinatusukuma kugeuka mwalimu wa katekisimu yetu, yaani, ya Ukweli wa Injili, ambao lazima utangazwe.
Sababu ya pili ni haswa kinyume cha ya kwanza. Anayejua kuona, anayejua kusoma moyoni mwa watu, katika moyo wa ulimwengu, anagundua kwamba, ndani kabisa, kuna hali ya kutoridhika, ya kutotulia, hitaji la neno la kweli, la neno jema, neno linaloonyesha maana ya maisha, ambayo ulimwengu haujui tena ni ipi, hauna tena uwezo wa kuifafanua; unaishi kama asiyeona, au kama kipofu, katikati ya giza. Sisi tunayo tochi; sisi tunayo taa; sisi tunalo Neno la Injili, ambayo ni nuru ya ulimwengu.
Bwana aliwaambia wanafunzi wake: “Ninyi ni nuru ya ulimwengu.” Hapo kabisa: ikiwa sisi ni nuru ya ulimwengu, tunapaswa kwenda kukutana na watu hawa waliopotea, wenye kinyongo hivi, wakatili hivi; ambao wamefikia, hata, kupotoka kabisa, bila kanuni, bila mistari ya tabia njema na ya kibinadamu. Ni lazima twende kuwalaki na kusema: Tazama! Tazama! Hii ndiyo njia; Hii ndiyo njia! Narudia: kwa sababu hizi mbili, moja iliyo ugumu, na ya pili iliyo nafasi ya kuitangaza Injili, tazama, Kanisa linaanza kusema.
Kwa hiyo, tuko katika awamu ya kitume, ya kimisionari, ya kufundisha, ambayo haijawahi kusisitizwa hivi katika maisha ya Kanisa. Ni lazima sote tuhusike. Ujenzi wa Mwili wa Kifumbo wa Kristo duniani, ambao ni Kanisa letu la sasa, ni wajibu, kama Mtaguso unavyosema, si tu wa mapadre, maaskofu, nk, bali wa kila muumini. Kila mmoja anapaswa kuwa shahidi, anapaswa kujua kutafsiri, angalau kwa mfano wake na kwa mchango wake, nk, ujumbe ambao anabeba ndani. Hakuna mkristo bubu; hakuna mkristo tasa; hakuna mkristo anayeishi kwa ajili yake mwenyewe. Anapaswa kuishi kwa ajili ya jumuiya, kwa ajili ya Mwili wa Kifumbo, unaoitwa “Kanisa”.
Mtazamo huu, ni wazi, na inaahidi, kwamba juhudi zitazidishwa, ili kuweka katika vitendo tekeleza programu hii kubwa na ya dharura: kuinjilisha, katekesi. Kuna mipango mingi sambamba na inayofanana kidogo na yenu hiyo sasa sikiliza. Kwa njia hii tunashuhudia kushamiri kwa kazi na njia kutoa tangazo la ujumbe wa kiinjili uenezi wake bora na tafsiri, tunaweza kusema.
Tunataka iangaliwe kwamba tukio hili lenye aina nyingi katika Kanisa Takatifu halihusu tu elimu na mafundisho ya shughuli zake. Sio tu mafundisho ya mwalimu kwa mwanafunzi. Badala yake, ni pana zaidi, lenye ufundishaji zaidi na la kimaisha zaidi, ambalo pia linahusu namna ya kuishi, ili mafundisho ya ukweli wa kidini yawe sambamba na mafundisho ya kielimu; zaidi ya hayo: yanaunganishwa na ushuhuda wa maisha, ambao kwao mafundisho ni elekezo na kanuni.
Pili, tunaangaliza kwamba wajibu huu, katika yule anayeutekeleza kama kwa yule anayenufaika nao, haufuati sifa ya “mzito sana na mgumu“, ingawa kihalisia ndivyo. Tatizo moja kubwa ambalo mapdre hujikwaa nalo, ni lipi? Kwamba watu hawaji, bali wanasema: Inachosha sana, kusikiliza mahubiri, kusikiliza somo, kujifunza katekisimu…! inanichosha; Napendelea kutembea, kwenda kwenye sinema, kufurahia, nk. Yaani: Kanisa hili linalofundisha, linachosha sana… si kweli!
Tujiambie sisi wenyewe na tuwaambie watu wetu. Aliyeelewa siri ya Ukweli, ambayo maneno yetu yanabeba, anabaki kama aliyepigwa na umeme na Nuru hii, na Ukweli huu, na inamgeuza, awe mtume, padre ama yeyote anayeitangaza, kama vile vile mfuasi, anayeisikiliza, na inamfanya atangaze. Ah…! mimi sikuwahi kuwaza kwamba ingekuwa nzuri ajabu hivi! Ah, ni kweli, nzuri mno, angalia! Unafunguka, narudia, upeo wa mwanga na wa uzuri, ambao haukutarajiwa. Utekelezaji wa wajibu huu mgumu unakuwa heshima, unakuwa hazina, unakuwa wito, unaoturembesha na kutupa shauku.
Ningependa kuwauliza, ikiwa wapo wamisionari miongoni mwenu: Kwa nini ninyi ni wamisionari? Kwa sababu mmeinuliwa na Roho wa Injili. Ni ajabu gani kutangaza Kweli, kutangaza siri ya Uzima, mipango ya Mungu matumaini ambayo hayafi. Inakuwa kitu chenye uzuri kiasi kwamba unashindwa kujiondoa na tunajisikia kuitwa kuwa, sisi pia, mitume na watangazaji wa Ukweli huu. Hivyo, kutimiza wajibu huu wa kutangaza si jambo la kuchosha tena, kwani kusikiliza hakusumbui tena; zinabeba ndani yao faraja ya uchovu unaokuja nazo; inawafurahisha mashahidi wake, inawahakikisha, inawashirikisha malimbuko ya Ufalme wa Mungu wanaoutangaza.
Katika nafasi yetu, hapa katikati ya Kanisa, tunawapokea wengi, wanaotoka mbali, kutoka utume mbalimbali. Tunawapokea kwa kuridhika sana na tunawaacha waongee, ili kupokea ushuhuda wao. Baadhi yao wanapitia matatizo makubwa sana, yanayofanya ushindwe kueleza jinsi wanavyoweza kuishi, kuvumilia, kushinda magonjwa, uadui, hatari, nk. Hata hivyo, ninawaambia haya ili nanyi pia mfurahi wanapojifafanua, wanasema juu ya furaha ambayo haiwezi hata kulinganishwa na furaha zingine ulimwenguni. Na, ikiwa sisi tunathubutu kuwaambia: “Lakini wewe, je, ungebaki hapa au ungependelea kurudi?” “Kurudi, kurudi,” wanasema. Na wanarudi, katikati ya matatizo makubwa, kwa sababu wamekuwa wafungwa wa furaha ya Injili.
Tutasema, basi, zaidi ya hayo, kwamba wale ambao, kwa moyo rahisi na wa ukarimu, wanajiweka katika huduma ya uinjilishaji, wanaonja, bila shaka kupitia karama ya Roho Mtakatifu, ya kisiri na isiyo na dosari, mgeuzo wa kisaikolojia na wa kimaadili, ambao ni kawaida yake. Katika mgeuzo huo, badiliko linalogeuza matatizo katika vichocheo. Ninarudia niliyosema kabla kuhusu wamisionari. Kwa nini wanarudi? Kwa sababu kuna mengi ya kufanya; kuna watu maskini wa kufariji; kwa sababu kuna hatari; “Lazima niende mimi kuwaponya wenye ukoma; Inabidi niende mimi kuzuia kwamba watu hao maskini kafara wa harakati za kijamii, au kuwa mtumwa wa hali zisizovumilika.”
Ugumu, kikwazo, unakuwa wa kuvutia; kile kilichokuwa cha kutisha hapo awali, kilichochosha na kukera, baadaye, kinyume chake, kinakuwa nguvu inayovutia, inayosisimua, inayomfunga na kumfanya mtume – tutumie neno hili kuu, ingawa likitumika kwa maana pana – ‘mfiadini’, yaani, shahidi. Tukio hili linashangaza sana ambapo yeyote aliye na macho ya kuona matukio ya Kanisa – sisi tunalo jukumu hili na bahati hii- hawezi kufanya chochote ila kumshukuru Mungu, kwa sababu yameniruhusu kupata ono hili: kuona, haswa, wengi mno, ambao ni: wenye shauku ya Injili, Injili isiyokata tamaa, Injili inayogongana na fikra zote, maovu yote na vikwazo vyote vya dunia hii.
Injili, narudia, huwafanya wenye heri wanaoihubiri, hugeuza magumu kuwa vichocheo, katika kuwa vivutio, na hata kushindwa, yaani kutofanikiwa kunageuka kuwa vyeo vya sifa, ingawa inaonekana kama bumbuwazi, vya kusema ‘Nimefanya nilichoweza’, na pia vya amani, ambayo inashuka kwa utulivu ndani ya mioyo hii ambayo imekosa hata kuridhishwa na mafanikio ya juhudi zao.
Sasa tunaweza kuelewa pia ushuhuda ambao wageni wa leo wanatupatia. Ushuhuda huu unasitawi karibu na mhimili wa maisha ya kikristo, ambao ni Ubatizo.
Ukatekumeni ulikuwa kipindi cha maandalizi kwa Ubatizo. Ubatizo sasa, angalau katika usambazaji na mafundisho yake, hauna tena usitawi huu. Basi hawa wanasema: “Sawa, Tutafanya baada ya Ubatizo.” Neema ya utakaso haijatosha. Zaidi ya hayo: neema ya utakaso haijafanya zaidi ya kuwasha moto, ambao lazima uwe nuru, ambayo huenea maishani. Mtakatifu Augustino anarejea hili: “Je, hatuwezi kufanya kabla? Tufanye basi Ukatekumeni baadaye”, yaani, mafundisho, elimu, ukomavu, mbinu yote ya elimu ya Kanisa, baada ya Ubatizo.
Sakramenti ya kikristo ya kuzaliwa upya, ambayo inapaswa kurudi kuwa jinsi ilivyokuwa katika dhamiri na katika desturi za vizazi vya kwanza vya Ukristo. Utendaji zoefu, zoezi, ambalo ni kawaida ya Kanisa, viliingiza desturi takatifu ya kutoa Ubatizo kwa watoto wachanga. Je, wamepata mafundisho gani? Tazama kwamba msimamizi, aliyepo badala yake, ningesema kwamba anaongea kwa niaba ya mbatizwa. Lakini mbatizwa hafaidiki na ushuhuda huu ambao msimamizi anatoa kwa padre, wakikuruhusu ibada ya ubatizo ifupishwe kiliturujia – liturujia bado inahifadhi masalia ya uingizwaji huu wa kimaandalizi – hayo maandalizi ambayo, katika nyakati za kwanza, jamii ilipokuwa ya kipagani sana, yalifanana na Ubatizo na yaliitwa “ukatekumeni”. Baadaye Kanisa lilifupisha kipindi hiki. Kwa nini? Kwa sababu familia zote zilikuwa za kikatoliki, zote zilikuwa nzuri, zote za kikristo; jamii, ndani ndani, ilikuwa na mwelekeo wa kikristo: watajifunza njiani.
Lakini sasa ambapo jamii haina tena sura moja, aina moja, bali zipo nyingi, zaidi ya hayo, imejaa ukinzani na vikwazo kwa Injili yenyewe, katika mazingira ya leo ya kijamii, ni muhimu kwamba njia hii ikamilishwe na mafundisho, uingizwaji utakaofuata, kama nilivyosema, kwa mtindo wa maisha unaofaa kwa mkristo, ambao unatakiwa kufanyika baada ya Ubatizo.
Hii ndio siri ya muundo wenu. Yaani: hutoa msaada wa kidini, hujalia maandalizi kimatendo kwa uaminifu wa kikristo na hutekeleza uingizaji wenye ufanisi katika jumuiya ya waumini, ambayo ni Kanisa, baada ya mtu kuwa ameshaingia, kwa ufanisi na katika roho, kwenye Kanisa; imekuwa kama mbegu ambayo bado haijapata nafasi ya kumea.
Hapa, basi, ni kuzaliwa upya kwa neno “ukatekumeni” ambako, kwa hakika, hakutaki kubatilisha, au kupunguza, umuhimu wa taratibu za ubatizo zilizopo hadi sasa, bali inataka kulitumia kupitia utaratibu wa hatua kwa hatua na wa kina, unaokumbusha na kufanya upya, kwa namna fulani, ukatekumeni wa nyakati nyingine. Aliyebatizwa anahitaji kuelewa, kufikiria tena, kuthamini na kusema amina kwa utajiri usio na kifani wa sakramenti iliyopokelewa.
Na Sisi tunasikia furaha ya kuona kwamba hitaji hili limeeleweka leo na miundo ya taasisi ya kikanisa, parokia na majimbo hasa, na kisha nyingine zote za familia za kidini. Katika uwanja huu wa miundo, kama nilivyosema, parokia ndio msingi.
Kwa njia hii, inatolewa picha ya katekesi inayokuja baada ya ile ambayo Ubatizo ulikosa: “Uchungaji kwa watu wazima” ambayo, kama inavyosemwa leo, imekuwa ikifafanua na ikiunda mbinu mpya na mikakati mipya, kama vile wizara mpya -jinsi gani kuna haja ya atakayekuja kusaidia: tazama makatekista; tazama watawa wa kike wenyewe; tazama familia, zinazokuwa walimu wa Uinjilishaji huu wa baada ya Ubatizo. “Uchungaji kwa watu wazima“, kama inavyosemwa leo, imekuwa ikifafanua na ikiunda mbinu mpya, mikakati mipya na wizara mpya za kusaidia, zinazotegemeza msaada unaohitaji uangalifu mkubwa leo kwa ajili ya padre na shemasi katika kufundisha na kushiriki katika liturjia; aina mpya za upendo, za utamaduni na za mshikamano wa kijamii zinakuza uhai wa jumuiya za kikristo na zinakabili dunia, zikitoa ulinzi, utetezi na zikivutia.
Watu wengi wanaelekea na kuingia katika Jumuiya hizi za Neokatekumenato, kwa sababu wanaona kwamba ndani yao kuna uhitaji , ukweli, kuna kitu kilicho hai na halisi, ambacho ni Kristo, anayeishi ulimwenguni. Na liwe hivyo pamoja na Baraka Yetu ya Kitume.