Mario Pezzi

Mario Pezzi

Mario Pezzi

Mario Pezzi alizaliwa huko Gottolengo (Brescia, Italia), mnamo Septemba 19, 1942, na ni mtoto wa tatu kati ya watoto watano. Aliingia katika seminari ya Wamisionari wa Comboni akiwa na umri wa miaka 10. Baada ya Unovisi alitumwa na Wakuu wake kwenda Roma kwenye Chuo cha Kimataifa na kusomea Teolojia katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana. Alipata Daraja la Upadre tarehe 19 Machi 1969 na kuanza udaktari katika Teolojia ya Dogmatiki katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian pamoja na Profesa Padre Zoltan Alszeghy.

Katika mwaka huo huo, alikutana na Kiko na Carmen, waanzilishi wa Njia ya Neokatekumenato, na alihudhuria katekesi za mwisho katika parokia ya Natività (“Kuzaliwa kwa Bwana”) huko Roma. Mnamo Januari 1970, alipokea katekesi za Njia katika parokia ya Mtakatifu Yohane wa Mungu, ambamo alitekeleza huduma yake ya kichungaji, na akawa sehemu ya jumuiya ya kwanza ya neokatekumenato ya parokia hiyo. Akiona matumaini katika Njia kwa ajili ya ukatekumeni katika utume huko Afrika, hasa baada ya maang’amuzi mabaya ya mauaji kati ya Wakristo nchini Burundi, alipata ruhusa kutoka Wakuu wake ili kufanya maang’amuzi kama msafiri wa Njia, akitazamia utume za Afrika. Mnamo Septemba 1970 alikatiza masomo yake ya kupata udaktari na alitumwa na Kiko na Carmen kuanzisha Njia katika parokia mbili za Jimbo la Brescia na Milan, na Januari 1971 hadi parokia ya Mtakatifu Leo huko Catania.

Mnamo Juni 1971, alialikwa na Kiko na Carmen kuchukua nafasi ya P. Fransisko Cuppini, mpresbiteri ambaye alikuwa amewasindikiza tangu 1968, na kuwa hivyo sehemu ya kikundi chao katika vipindi ambavyo waliinjilisha nchini Italia, hasa katika miji ya Roma, Florence na Ivrea. Katika vipindi ambavyo Kiko na Carmen walikuwa Hispania, wakisindikizwa na Padre Jesús Blázquez kama mpresbiteri, Padre Mario alitumwa kuinjilisha huko Lombardia na kisha Ureno. Desemba 1981, pamoja na barua kutoka kwa Mkuu wa Wamisionari wa Comboni, alitumwa kama mmisionari msafiri wa Comboni kuanzisha Njia huko Khartoum (Sudan), moyo wa utume za Comboni, na kisha, mnamo Machi 1982, huko Kampala (Uganda). Tangu mwaka huo alifanya safari nyingi barani Afrika: akitembelea Maaskofu mbalimbali wa Kenya, na familia katika utume wa Njia katika Ivory Coast, Cameroon, Zambia, na Seminari za Redemptoris Mater za Kitwe (Zambia), Douala (Cameroon), Dar es Salaam (Tanzania), Goma (Kongo), na Morondava (Madagascar). Pia alitembelea maaskofu kadhaa kwanza Angola na kisha Msumbiji ili kufungua Njia. Alikuwepo pia huko Bangui (Jamhuri ya Afrika ya Kati) na Bujumbura (Burundi).

Tangu 1982 ameitwa kuwa sehemu ya kikundi cha wawajibikaji wa Njia ya Neokatekumenato pamoja na Kiko na Carmen, kwa daima, akiwasindikiza katika kuhusiana na Mapapa, Kiti Kitakatifu, Maaskofu, katika hatua, katika kuishi pamoja za kiulimwengu za makatekista wasafiri, na katika safari na mikutano ya kimataifa, hadi leo. Mnamo 1992, Mwelekeo Mpya wa Wamisionari wa Comboni ulimwalika kujiunga tena na Taasisi au kuandikishwa katika Jimbo la Roma. Akiisha kuacha Taasisi hiyo, Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Roma, Mha. Camilo Ruini, alimkaribisha kama Mpresbiteri Katekista Msafiri.

Kwa idhini ya Statuta mwaka 2002 “ad experimentum” (kama majaribio), na mnamo 2008 kwa idhini mkataa, amepewa jina na Kiti Kitakatifu mpresbiteri wa Kikundi cha Kimataifa pamoja na Kiko na Carmen (kabla ya Carmen kufariki).