Hadhira ya kutuma “Missio ad gentes” 20-1-2012

Hadhira ya kutuma “Missio ad gentes” 20-1-2012

Benedikto XVI

Mji wa Vatikano – Ukumbi Paulo VI, 20 januari 2012 *

Mnamo tarehe 20 Januari 2012, katika kuchapishwa “Tamko” ambalo kwalo maadhimisho yaliyomo katika Orodha ya Katekesi ya Njia ya Neokatekumenato yameidhinishwa, Baba Mtakatifu Benedikto XVI alitamka kwa waliohudhuria hotuba hii ambayo tunachapisha hapa chini. Katika tukio hili muhimu, linalohitimisha safari ya uidhinishaji wa Njia ya Neokatekumenato (2008: Statuta; 2010: Amri ya kuidhinisha Orodha ya Katekesi ya Njia ya Neokatekumenato; 2011: Amri ya kuidhinisha maadhimisho yanayosindikiza hatua mbalimbali za njia hiyo ya uingizwaji wa kikristo) walikuwepo waanzilishi, Kiko, Carmen na padre Mario, makateskista wasafiri wote wa dunia, familia katika utume, “Missio ad gentes” zilizotumwa tayari na zile “Missio ad gentes” 15 mpya ambazo Papa ametuma katika tukio hili. Pia walikuwepo wawajibikaji wa jumuiya ambazo zimehitimisha njia ya Neokatekumenato, mapadre wa seminari za Redemptoris Mater za Ulaya, waseminari, makatekista na “Jumuiya katika utume” (“Communitates in missione”) za Roma.

«Ndugu wapendwa: Mwaka huu tena nina furaha ya kuweza kukutana nanyi na kushiriki wakati huu wa kutuma kwa utume. Salamu maalum kwa Kiko Argüello, Carmen Hernández na padre Mario Pezzi, na salamu za upendo kwenu nyote: mapadre, waseminari, familia, walezi na ndugu wa Njia ya Neocatekumenato. Uwepo wenu leo ni ushuhuda unaoonekana wa kujitolea kwenu kwa shangwe ya kuishi imani, katika ushirika na Kanisa zima na Khalifa wa Petro, na ya kuwa watangazaji hodari wa Injili.

Katika kifungu kutoka Mtakatifu Mathayo ambacho tumesikia, mitume wanapokea amri wazi kutoka Yesu: “Basi enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi” (Mt 28, 19). Mwanzoni walisita, mioyoni mwao bado kulikuwa na wasiwasi, mshangao mbele ya tukio la ufufuko. Na ni Yesu mwenyewe, Mfufuka, – mwinjili anasisitiza- ambaye anawakaribia, anawafanya wasikie uwepo wake, anawatuma kufundisha yote aliyowajulisha, akiwapa uhakika unaomsindikiza kila mtangazaji wa Kristo: “Jueni ya kwamba mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata mwisho wa nyakati” (Mt 28, 21). Ni maneno ambayo yanavuma kwa nguvu moyoni mwenu. Mmeimba “Resurrexit” (“Amefufuka“), wimbo unaoonyesha imani katika Yeye Aliye Hai, katika yule ambaye, kwa tendo kuu la upendo, ameshinda dhambi na mauti na kumpatia mwanadamu, sisi, joto la upendo wa Mungu, tumaini la kuokolewa, maisha yaliyojaa umilele. Katika miongo hii ya maisha ya Njia, moja kati ya ahadi zenu thabiti imekuwa kumtangaza Kristo mfufuka, kuitikia maneno yake kwa ukarimu, mara nyingi mkiacha usalama wenu binafsi na wa mali, hata kuacha nchi yenu wenyewe, na kukabili hali mpya na zisizo rahisi kila mara. Kumpeleka Kristo kwa wanadamu na kuwaleta watu kwa Kristo: hiki ndicho kinachohuisha kazi yoyote ya uinjilishaji. Ninyi mnaitekeleza kupitia njia inayowasaidia wale ambao tayari wamepokea Ubatizo kugundua upya uzuri wa maisha ya imani, furaha ya kuwa mkristo. “Kumfuata Kristo” kunahitaji safari ya kiutu ya  kumtafuta, ya kwenda pamoja Naye, lakini pia inamaanisha kutoka katika kifungo cha umimi, kuvunja ubinafsi ambao mara nyingi ndiyo sifa ya jamii ya wakati wetu, kuweka badala ya ubinafsi jumuiya ya mtu mpya katika Yesu Kristo. Na hili linafanyika katika uhusiano wa kina wa kibinafsi pamoja naye, katika kulisikiliza Neno lake, huku mkitembea katika njia aliyotuonyesha, lakini pia inafanyika, bila kutenganishwa, katika kusadiki pamoja na Kanisa lake, pamoja na watakatifu, ambao ndani yao daima hujulikana upya uso halisi wa Bibi-arusi wa Kristo.

Kama tunavyojua, ahadi hii si rahisi kila wakati. Wakati fulani mpo katika mahali ambapo linahitajika tangazo la kwanza la Injili, “Missio ad gentes”; mara nyingi, pengine, katika maeneo ambayo, hata baada ya kumjua Kristo, wamekuwa wasiojali imani: uduniaisho umefunika hisia ya Mungu na kuficha thamani za kikristo. Hapo ahadi yenu na ushuhuda wenu vinapaswa kuwa kama chachu ambayo, kwa saburi, kwa kuheshimu nyakati, kwa hisia ya kikanisa, huumusha unga wote. Kanisa limetambua katika Njia zawadi ya pekee ambayo Roho Mtakatifu amejalia kwa wakati wetu, na kuidhinishwa kwa Statuta na “Orodha ya Katekesi” ni ishara ya hilo. Ninawahimiza mtoe mchango wenu wenyewe kwa sababu hii ya Injili. Katika kazi yenu ya thamani, tafuteni daima ushirika wa kina na Kiti cha Kitume na wachungaji wa Makanisa mahalia ambamo mmeingizwa: umoja na mapatano ya mwili wa kikanisa ni ushuhuda muhimu wa Kristo na wa Injili yake katika ulimwengu tunamoishi. Familia wapendwa, Kanisa linawashukuru; linawahitaji kwa Uinjilishaji Mpya. Familia ni kiini muhimu kwa jumuiya ya kikanisa, ndani yake maisha ya mwanadamu na ya kikristo yanaundwa. Kwa furaha kubwa ninawaona watoto wenu, watoto wengi wanaowatazama ninyi, wazazi wapendwa, wanatazama mfano wenu. Familia mia moja ziko karibu kuondoka kwenda kwa Missio ad gentes kumi na mbili. Ninawaalika msiogope: anayebeba Injili hayuko peke yake kamwe. Ninawasalimu kwa upendo mapadre na waseminari: mpende Kristo na Kanisa, sambazeni furaha ya kumpata na uzuri wa kumpa yote. Pia ninawasalimu makatekista wasafiri, wawajibikaji na jumuiya zote za Njia. Endeleeni kuwa wakarimu kwa Bwana: atawapatia daima faraja yake.

Muda mchache uliopita ilisomwa kwenu Amri inayoidhinisha maadhimisho yaliyopo katika “Orodha Katekesi ya Njia ya Neokatekumenato”, ambayo si ya kiliturujia haswa, bali ni sehemu ya safari ya ukuaji katika imani. Ni ishara nyingine inayowaonyesha jinsi Kanisa linavyowasindikiza kwa uangalifu katika upambanuzi wenye subira, ambao unaelewa utajiri wenu, lakini pia unazingatia ushirika na upatanifu wa Mwili Mzima wa Kanisa .

Jambo hili linanipa fursa ya kufanya tafakari fupi juu ya thamani ya liturjia. Mtaguso wa Pili wa Vatikano unaifafanua kama kazi ya Kristo kuhani na ya mwili wake, ndio Kanisa (taz. Sacrosanctum Concilium, 7). Kwa mtazamo wa kwanza, hii inaweza kuonekana ya ajabu, kwa sababu inatoa hisia kwamba kazi ya Kristo inamaanisha matendo ya ukombozi ya kihistoria ya Yesu, mateso yake, kifo na ufufuko wake. Kwa maana gani, basi, liturujia ni kazi ya Kristo? Mateso, kifo na ufufuko wa Yesu si matukio ya kihistoria tu; yanaifikia na kuipenya historia, lakini pia yanaenda mbali zaidi na kubaki daima katika moyo wa Kristo. Katika utendaji wa kiliturjia wa Kanisa kuna uwepo hai wa Kristo mfufuka, ambaye anafanya fumbo lile lile la pasaka liwepo na lifae kwetu leo, kwa ajili ya wokovu wetu; anatuvuta katika tendo hili la kujitoa mwenyewe, ambalo daima liko moyoni mwake na kutufanya tushiriki katika uwepo huu wa fumbo la pasaka. Kazi hii ya Bwana Yesu, ambayo ndiyo maudhui halisi ya liturjia, namna hii ya kuingia katika uwepo wa Fumbo la Pasaka pia ni kazi ya Kanisa, ambalo, likiwa ni mwili wake, ni kitu kimoja na Kristo -Christus totus caput et corpus- (“Kristo mzima, kichwa na mwili“), asema Mtakatifu Agostino. Katika adhimisho la sakramenti, Kristo anatuzamisha katika Fumbo la Pasaka ili kutuvusha kutoka mauti kwenda uzimani, kutoka dhambi hadi katika maisha mapya ndani ya Kristo. Hayo ni kweli kwa namna ya pekee sana katika adhimisho la Ekaristi, ambayo, kwa vile ni kilele cha maisha ya kikristo, pia ni kitovu cha ugunduzi wake mpya, ambapo neokatekumenato inaelekea. Kama Statuta zenu zinavyosema, “Ekaristi ni ya msingi kwa neokatekumenato, kwa kuwa ni ukatekumeni baada ya ubatizo, unaofanyika katika jumuiya ndogo” (n. 13 § 1). Ili kuhamasisha mtazamo mpya katika utajiri wa maisha ya kisakramenti kwa watu waliojitenga na Kanisa, au ambao hawajapata malezi yapasavyo, wananeokatekumenato wanaweza kuadhimisha Ekaristi ya Jumapili katika jumuiya ndogo, baada ya Masifu ya kwanza ya Jumapili, wakifuata maagizo ya askofu wa jimbo (Taz. Statuta, n. 13 § 2). Lakini kila adhimisho la Ekaristi ni tendo la Kristo yule yule mmoja pamoja na Kanisa lake moja, na kwa sababu hiyo kwa asili yake liko wazi kwa wote walio sehemu ya Kanisa lake. Tabia hii ya kihadhara ya Ekaristi takatifu inadhihirika kwa kadri kila adhimisho la Misa Takatifu linaongozwa, hatimaye, na askofu mwenyewe kama mshiriki wa Baraza la Maaskofu, anayewajibika kwa Kanisa maalum mahalia (taz. Lumen Gentium, 26). Adhimisho katika jumuiya ndogo, likidhibitiwa na vitabu vya kiliturjia, ambavyo ni sharti vifuatwe kwa uaminifu, pamoja na maswala maalum yaliyoidhinishwa na Statuta za Njia, adhimisho hilo lina kama lengo kuwasaidia wale wanaopitia safari ya kineokatekumeni ili waonje neema ya kuingizwa kwenye fumbo la wokovu la Kristo, linalowezesha ushuhuda wa kikristo unaoweza kupata sifa za msimamo mkataa. Wakati huo huo, ukomavu endelevu wa mtu na wa jumuiya hiyo ndogo katika imani lazima ihamasishe uingizwaji wake katika maisha ya jumuiya kuu ya kikanisa, ambayo ina sura yake ya kawaida katika adhimisho la kiliturujia la parokia, ambalo ndani yake na kwa njia yake Ukatekumeni hutendeka (cf. Statuta, n. 6). Lakini pia wakati wa kufanya Njia ni muhimu kutojitenga na jumuiya ya kiparokia, haswa katika adhimisho la Ekaristi, ambayo ni mahali pa kweli pa umoja wa wote, ambapo Bwana hutukumbatia katika hali mbalimbali za ukomavu wetu wa kiroho na kutuunganisha katika mkate mmoja, unaotufanya kuwa mwili mmoja (taz. 1Kor 10, 16 nk.). Jipeni moyo! Bwana anawasindkiza daima, na mimi pia ninawahakikishia maombi yangu na kuwashukuru kwa ishara zenu nyingi za ukaribu. Nawaomba pia mnikumbuke katika maombi yenu. Bikira Maria Mtakatifu awasaidie kwa mtazamo wake wa kimama, mwimarishwe na Baraka yangu ya Kitume, ninayoeneza kwa ndugu wote wa Njia. Asanteni”.

(*) Taz. Gazeti la «L’Osservatore Romano», toleo la 21 Januari 2012.