«Regina Coeli» (Malkia wa Mbingu) ziara huko Aquileia na Venezia (Italia) 8-5-2011
Benedikto XVI
Bustani ya Mtakatifu Juliani – Mestre (Italia), 8 Mei 2011
Katika ziara ya kichungaji huko Aquileia na Venezia, kabla ya sala ya “Regina Coeli” (Malkia wa Mbingu, tenzi kwa Bikiria Maria katika kipindi cha Pasaka, Benedikto XVI aliomba kumwita Bikira ili ategemeze na “kuimarisha kazi ya walei wengi hivi, wanaoshirikiana kikamilifu katika Uinjilishaji Mpya” na miongoni mwao ameikumbuka Njia ya Neokatekumenato.
“Ndugu wapendwa:
Mwishoni mwa adhimisho hili tukufu la Ekaristi, tunaelekeza macho yetu kwa Maria, Malkia wa Mbingu. Katika pambazuko la siku ya Pasaka, amekuwa Mama wa Mfufuka na muungano wake pamoja naye ni wa kina sana kiasi kwamba pale alipo Mwana hawezi kukosekana Mama. Katika maeneo haya mazuri, yaliyo zawadi na ishara ya uzuri wa Mungu, ni mahekalu mangapi, Makanisa makubwa na madogo ambayo yamewekwa wakfu kwa Maria! Katika yeye uso wenye mwanga wa Kristo unaakisiwa. Tukimfuata kwa unyenyekevu, Bikira Maria hutuongoza Kwake Kristo. Katika siku hizi za kipindi cha Pasaka, tujiruhusu kushindwa na Kristo Mfufuka. Ndani Yake huanza ulimwengu mpya unaanza wa upendo na amani unaojumuisha matamanio ya ndani ya moyo wa kila mwanadamu. Bwana na awajalie ninyi ambao mnaishi katika nchi hizi, zilizo tajiri kwa historia ndefu ya kikristo, kuishi Injili kulingana na mfano wa Kanisa linalozaliwa, ambamo “kundi la waumini lilikuwa na moyo mmoja na roho mmoja” (Matendo 4:32). Tumwombe Maria Mtakatifu sana, aliyewategemeza mashahidi wa kwanza wa Mwana wake katika kuihubiri Habari Njema, ili pia ategemeze leo juhudi za kitume za makuhani; afanye ushuhuda wa watawa kuzaa matunda; ahuishe kazi ya kila siku ya wazazi katika upitishaji wa kwanza wa imani kwa watoto wao; aangazie njia kwa vijana ili wasonge mbele bila wasiwasi katika njia iliyofuatiliwa na imani ya baba zao; ajaze na tumaini thabiti mioyo ya wazee; afariji na ukaribu wake wagonjwa na wote wanaoteseka; aimarishe kazi ya walei wengi hivi wanaoshirikiana kikamilifu katika Uinjilishaji Mpya, katika parokia, katika vyama, kama vile maskauti na Kitendo cha Kikatoliki -ambacho kimepata mizizi mirefu na kilichopo katika nchi hizi- kama vilevile katika mikondo, ambayo kwa uwingi wa karama zao na matendo yao ni ishara ya utajiri wa muunganiko wa kikanisa – ninafikiria mikonfo kama vile Wafocolari, Komunyo na Ukombozi au Njia ya Neokatekumenato, kwa kutaja michache tu. Ninawahimiza wote kufanya kazi kwa roho iliyo kweli ya ushirika katika shamba hili kubwa ambalo Bwana ametuitia kufanya kazi. Ewe Maria, Mama wa Mfufuka na wa Kanisa, utuombee sisi!”.