Tarehe 26 Agosti 1986, Yohane Paulo II alikaribisha kwa shauku pendekezo la Kiko, Carmen na Padre Mario la kuanzisha huko Roma Seminari ya Kijimbo ya Kimisionari kwa ajili ya malezi ya wapresbiteri kwa ajili ya Uinjilishaji Mpya na akamteua Kardinali Ugo Poletti, Askofu Msaidizi wa Baba Mtakatifu, aisimike.
Tangu hapo seminari 122 zimesimikwa, ambazo zina sifa 3 za msingi: ni za kijimbo, za kimisionari na za kimataifa. Ndani ya malezi ya kitaaluma, ya kibinadamu na ya kiroho ya seminari hizi kipo kipindi cha uinjilishaji wa kimisionari, na wakiisha pata daraja la upadre -baada ya miaka michache ya kufanya kazi katika parokia-, askofu wa jimbo anawaruhusu kuondoka kwenda kuhudumu katika namna mbalimbali za utume zinazotekelezwa na Njia ya Neokatekumenato, kulingana na yale ambayo yameidhinishwa na kupitishwa na Vatikano katika Statuta.
Seminari inasimikwa na askofu wa jimbo na inawakaribisha vijana ambao wamegundua wito kupitia safari ya neokatekumenato ya uingizwaji wa Kikristo. Katika seminari, malezi ya kikristo kupitia Njia ya Neokatekumenato ndani ya jumuiya ni kipengele maalum na cha msingi cha safari ya malezi.
Katika miaka iliyofuata, maaskofu wengi wamefuata mfano wa Baba Mtakatifu kwa kufungua seminari nyingine.
Tangu 1990, mwaka wa ibada za kwanza za kutoa daraja takatifu, hadi leo, wapresbiteri waliopata daraja katika Seminari za Redemptoris Mater ni takriban 2,380. Hivi sasa, kuna vijana 2,300 wanaojiandaa kupokea daraja takatifu.