NJIA YA NEOKATEKUMENATO NI NINI?
MUHTASARI WA KITEOLOJIA-KIKATEKESI MIONGONI MWA WALIO MASKINI ZAIDI
Njia ya Neokatekumenato ilizaliwa mnamo 1964 katika vibanda vya Palomeras Altas, huko Madrid (Hispania). Mazingira ya vibanda hivyo yaliundwa na watu walioharibika zaidi katika jamii: wazururaji (“gypsies”) na wahalifu, wengi wao wasiojua kusoma na kuandika, walalahoi, wezi, makahaba, vijana wahalifu, wahamiaji, nk. Katika mazingira haya mbegu ya Njia ya Neokatekumenato iliota. Miongoni mwa maskini na waliowekwa kando, ambao baada ya kupokea tangazo la Kristo aliyekufa na kufufuka wanaona jinsi Roho Mtakatifu anavyoinua safari ya uanzishwaji wa kikristo kwa sura ya ukatekumeni wa Kanisa la mwanzo.
Mwanzoni mwa miaka ya 60, Francisco José Gómez Argüello (Kiko), mchoraji kutoka Hispania, aliyeshinda Tuzo la Kitaifa la Uchoraji mnamo 1959, baada ya misukosuko ya kimaisha, aligundua katika mateso ya wasio na hatia fumbo la Kristo Msulubiwa, aliyeko katika wale wa mwisho wa dunia. Maang’amuzi haya yalimfanya aache vyote na, akifuata nyayo za Charles de Foucauld, alikwenda kuishi kati ya maskini hawa wa Palomeras Altas.
Katika mchakato huu, anapata uvuvio kutoka Bikira Maria: “Inabidi kufanya jumuiya za kikristo kuwa kama Familia Takatifu ya Nazareti, zinazoishi katika unyenyekevu, urahisi na sifa. Mwingine ni Kristo.”
Carmen Hernández, pia Mhispania, mwenye shahada ya Kemia, alilelewa katika Taasisi ya Wamisionari wa Kristo Yesu. Alihitimu katika Teolojia pamoja na Wadominiko wa Valencia na kugundua upyaisho wa Mtaguso wa Vatikano II kupitia kwa mwana liturujia Mons. Pedro Farnés Scherer.
Baada ya miaka miwili katika Israeli akiwa karibu na mapokeo hai ya taifa la kiyahudi, pamoja na mahali kadhaa katika Nchi Takatifu, alirudi Madrid akiwa na matumaini ya kuunda kikundi cha wamisionari ili kuwainjilisha wachimba migodi wa Oruro (Bolivia), kupitia Askofu Mkuu wa wakati huo wa jimbo la La Paz, Mons. Jorge Manrique Hurtado. Kupitia mmoja wa dada zake, alikutana na Kiko Argüello katika vibanda vya Palomeras, akajenga kibanda kwenye ukuta wa kiwanda fulani na akaanza kushirikiana naye.
JUMUIYA YA KWANZA VIBANDANI KWA PALOMERAS HUKO MADRID
Tabia ya kisanii ya Kiko, maang’amuzi yake ya kiutu, malezi yake kama katekista katika “Cursillos de Cristiandad” (Kozi ya Ukristo) na msukumo wa uinjilishaji wa Carmen, malezi yake ya kiteolojia, ujuzi wake wa Fumbo la Pasaka na wa upyaisho wa Mtaguso wa Vatikano II, pamoja na mazingira hayo ya walio maskini zaidi duniani, yaliunda maabara ambamo ulizaliwa muhtasari wa kikerigma, wa kiteolojia-katekesi, ambao ndio uti wa mgongo wa safari hii ya uinjilishaji kwa watu wazima ambao kiini cha Njia ya Neokatekumenato.
Ndivyo ilivyozaliwa jumuiya ya kwanza iliyosimama katika miguu hii mitatu: Neno la Mungu-Liturujia-Jumuiya, ikiiongoza kwa ushirika wa kindugu na imani mpevu.
Mang’amuzi haya ya kikatekesi, yaliyojitokeza sambamba na upyaisho uliochochewa na Mtaguso wa Vatikano II, yalipokelewa vema na Askofu Mkuu wa Madrid wa wakati huo, Mons. Casimiro Morcillo, ambaye aliwahimiza waanzilishi wa Njia kuieneza katika parokia ambazo zingeiomba. Maang’amuzi haya yalienea polepole katika Jimbo kuu la Madrid, katika jimbo la Zamora na majimbo mengine ya Hispania.
NJIA INAFIKA ROMA
Baada ya jumuiya ya kwanza kuundwa miongoni mwa maskini na baada ya Kiko na Carmen kualikwa na baadhi ya maparoko wa Madrid kuleta mang’amuzi haya katika parokia zao, kama vile huko Zamora, katika aina mbalimbali za mazingira, walihamia Roma kwa mikono ya Mons. Dino Torreggiani, mwanzilishi wa Taasisi ya Watumishi wa Kanisa (shirika la mapadre linalojitoa kwa ajili ya uchungaji wa watu waliowekwa kando na jamii, wahalifu wa mitaani na wahamiaji), na ambaye sasa yuko katika mchakato wa kutangazwa kuwa mwenyeheri.
Torreggiani aliwafahamu Kiko na Carmen huko Ávila (Hispania), akihudhuria katekesi kadhaa walizotoa katika parokia ya Santiago, katika miaka ya 66-67. Alitambua jibu katika mang’amuzi ya Kiko na Carmen kwa haja ya uinjilishaji wa walio mbali zaidi, akawaalika Roma, ambako walikuja pamoja na padre kutoka Sevilla.
Kabla ya kuanza safari hiyo, walikutana na aliyekuwa Askofu Mkuu wa Madrid wakati huo, Mons. Casimiro Morcillo, ambaye alikuwa amewaunga mkono Kiko na Carmen katika vibanda na aliyewatia moyo ili Njia iendelee kuenea katika mji mkuu huo. Morcillo aliwakabidhi barua ya mapendekezo kwa mwakilishi wa Papa huko (Askofu mkuu wa Roma), Kardinali Angelo Dell’Acqua, na barua nyingine kwa Kardinali wa Florence, Ermenegildo Florit.
Kiko na Carmen walifika Roma mnamo Julai 1968. Muda mfupi baada ya kuwasili kwao, Torreggiani aliwapeleka kwa Bikira wa Pompeii (Naples) ili waweze kukabidhi utume wao kwa jina hilo la Maria lililo maarufu sana nchini huko.
P. Dino aliandamana nao kutembelea maparoko kadha wa kadha, ambao waliwaelezea Njia ni nini na jinsi ilivyokuwa imeanza miongoni mwa walio maskini zaidi huko Madrid. Hata hivyo, upyaisho wa Mtaguso bado ulikuwa haujaeleweka kikamilifu na hawakukaribishwa. Hapo ndipo Kiko aliposikia wito wa Mungu wa kurudi tena kuishi kati ya maskini wa “Borghetto Latino” huko Roma, akimngoja Bwana awaonyeshe mapenzi yake.
Kiko akiwa tayari akikaa katika eneo hilo lililoharibika la Roma, vijana kadhaa walistaajabu na mang’amuzi yake, wakamwalika kwenye mkutano wa jumuiya ndogo ndogo katika mji wa Nemi (nje kidogo ya Roma).
Huko, katika darasa lililojaa vijana – wengi wao wenye itikadi za mrengo wa kushoto – walimwomba atoe ushuhuda wake. Baadaye, baadhi yao walimwalika Kiko kwenye misa iliyochangamshwa na gitaa, katika groto ya parokia ya Mashahidi wa Kanada huko Roma. Hapo, alipoulizwa maoni yake, Kiko aliwaambia: “Kanisa halifanywi upya kwa gitaa, bali kwa tangazo la Kerigma na Fumbo la Pasaka.”
Muda mfupi baadaye, Kiko aliwapeleka kundi hili la vijana katika mafungo, na baada ya hapo walimpendekeza uwezekano wa yeye kuanza kutoa katekesi za Njia katika parokia yao.
Hivyo, mnamo Novemba 2, 1968, ilizaliwa jumuiya ya kwanza ya neokatekumenato ya parokia ya Mashahidi wa Kanada, ikiwa na watu 70.
Njia iliendelea kuenea katika parokia nyingine, na katika kikundi kilichoundwa na Kiko na Carmen akajiunga Padre Mario Pezzi.
NJIA, TUNDA LA MTAGUSO WA PILI WA VATIKANO II
Mwaka 1974, Papa Paulo VI, katika hadhira iliyotolewa kwa jumuiya za kwanza za neokatekumento, alitambua Njia kama tunda la Mtaguso wa Vatikano II: “Tazameni matunda ya Mtaguso! Ninyi mnafanya baada ya Ubatizo kile ambacho Kanisa la mwanzo lilifanya kabla ya Ubatizo: kabla au baada, si muhimu. Swala ni kwamba ninyi mnatazamia uhalisi, utimilifu, uwiano sawia, unyofu wa maisha ya Kikristo. Na hii ina stahili kubwa sana, ambayo inatufariji ajabu (…) Ni furaha gani mnayotupatia kwa uwepo wenu na matendo yenu!
Mapapa waliofuata wamesukuma na kutambua Njia kama tunda na uvuvio wa Roho Mtakatifu kwa ajili ya msaada wa Kanisa. Hata Yohane Paulo I, ambaye, akiwa Patriarki wa Venice, alikuwa amewakaribisha Kiko na Carmen kuanzisha Njia katika jimbo hilo.
Mtakatifu Yohane Paulo II alitia msukumo, aliimarisha na kuwezesha maendeleo ya uanzishwaji huu wa kikristo kwa watu wazima, akiwezesha pia namna mpya za wito wa kimisionari kama vile familia katika utume na malezi ya seminari za kijimbo na za kimisionari za Redemptoris Mater.
Mnamo 1990, Mtakatifu Yohane Paulo II aliandika katika barua yake Ogniqualvolta: “Ninaitambua Njia ya Neokatekumenato kama njia ya malezi ya kikatoliki inayofaa kwa jamii na kwa nyakati za leo “, na “Ninatamani sana, hivyo, kwamba ndugu zangu katika uaskofu wathamini na kusaidia. –pamoja na mapadre wao– kazi hii kwa ajili ya uinjilishaji mpya”.
MATUNDA YA KWANZA YA KIMISIONARI PAMOJA NA MTAKATIFU YOHANE PAULO II
Njia ya Neocatekumenato inapoanza kusambaa kama safari ya malezi ya kikatoliki na ya kukomaa katika imani, yanatokea matunda na karama za uinjilishaji za kwanza zinazoendana na mkondo huu wa kikanisa. Mnamo 1986, Mtakatifu Yohane Paulo II alikaribisha kwa furaha na kuwezesha seminari ya kwanza ya Redemptoris Mater huko Roma.
Tangu Jubilei ya Vijana ya mwaka 1984 na Siku ya Kwanza ya Vijana Duniani (SViD) iliyoitishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II mwaka 1986, maelfu ya vijana kutoka Njia ya Neokatekumenato wameandamana na Baba Mtakatifu katika sikukuu hizi. Tangu hapo, katika kila SViD wawajibikaji wa Njia hufanya mkutano wa kuitisha miito katika siku zinazokuja baada ya mkutano, ambapo mamia ya wavulana na wasichana wanaonyesha utayari wao kwa upadre au kwa maisha ya wakfu
Mwaka 1988, katika mji wa Porto San Giorgio, huko Italia, Mtakatifu Yohane Paulo II alituma familia 100 za kwanza kuinjilisha sehemu mbalimbali za dunia.
Pia alikuwa yeye aliyesukuma Statuta za Njia ya Neokatekumenato kuanzia mwaka 1997.
KUIDHINISHWA KWA STATUTA NA BENEDICT XVI
Benedikto XVI vile vile, amesindikiza, ameunga mkono na kutia moyo usambaaji wa kimisionari wa Njia. Katika kipindi chake cha Upapa, mwaka 2008, Statuta ziliidhinishwa kwa daima na Idara ya Kipapa kwa Walei. Kwa upande mwingine, Idara ya Mafundisho ya Imani ilitoa idhini yake kwa Orodha ya Katekesi katika mwaka 2010.
MSUKUMO MPYA WA PAPA FRANSISKO
“Namshukuru Bwana kwa furaha ya imani yenu na kwa moto wa ushuhuda wenu wa kikristo, tumshukuru Mungu! (…) Ninawashukuru kwa kila kitu mnachofanya katika Kanisa na katika ulimwengu”, alisema Papa Fransisko katika hadhira yake ya kwanza pamoja na waanzilishi na ndugu wa Njia mnamo 2014.
Baba Mtakatifu ametuma rasmi katika nafasi mbalimbali familia katika utume, mapadre na Missio ad Gentes mpya katika sehemu mbalimbali za ulimwengu zilizopoteza ukristo wao.
Mnamo Machi 6, 2015, katika hadhira nyingine ya Njia, aliwaambia hivi waanzilishi na washiriki wa Njia waliokuwepo: “Nawasalimu waanzilishi wa Njia ya Neokatekumenato, Kiko Argüello na Carmen Hernández, pamoja na Padre Mario Pezzi; Pia ninawatoleaa shukrani zangu na kuwapa moyo kwa yote ambayo, kupitia Njia, wanafanya kwa manufaa ya Kanisa. Sikuzote ninasema kwamba Njia ya Neokatekumenato ina manufaa makubwa kwa Kanisa!”
NJIA LEO
Tarehe ya Julai 19, 2016, alifariki Carmen Hernández, mwanzilishi wa Njia pamoja na Kiko Argüello, akazikwa katika Seminari ya Redemptoris Mater ya Madrid. Kwa vile kikundi cha wawajibikaji wa kimataifa kilikuwa hakijakamilika, na kwa ombi la Kiti Kitakatifu-kulingana na Statuta za Njia-, mwaka mmoja na nusu baadaye alijiunga kama sehemu ya kikundi hicho María Ascensión Romero, Mhispania, katekista msafiri kwa miaka 25 nchini Urusi.
Njia ya Neokatekumenato iko kwa huduma ya maaskofu na maparoko kama safari ya kugundua upya ubatizo na ya malezi endelevu katika imani, na inapendekezwa kwa waumini wanaotamani kufufua katika maisha yao utajiri wa uingizwaji wa Kikristo.
Njia – ambayo safari yake inafanyika katika maparokia, katika jumuiya ndogo zinazoundwa na watu wa umri na hali ya kijamii mbalimbali- hatua kwa hatua inaongoza waumini kwenye uhusiano wa kina na Yesu Kristo na kuwageuza kuwa watendaji katika Kanisa na mashahidi wa kuaminika wa Habari Njema. Ni chombo cha uanzishwaji wa kikristo kwa watu wazima wanaojiandaa kupokea ubatizo.
Habari za Njia ya Neokatekumenato
Kama ilivyokuwa mnamo Novemba 2022:
Jumuiya: 21,066
Majimbo: 1,366
Parokia: 6.293
Mataifa: 135
Seminari za kimisionari za kijimbo:
Seminari za Redemptoris Mater (SRM): 121
Waseminari: 1,900
Mapadre waliopata malezi katika SRM: 2,950
Familia za kimisionari:
Familia katika utume: 1,000 zinazoinjilisha katika Missio ad Gentes 212 katika mataifa 62.
Zinazoimarisha na kutegemeza Njia katika imani: 800 katika mataifa mbalimbali
Familia zilizomo katika vikundi vya makatekista wasafiri: 300
KIKUNDI CHA KIMATAIFA
Kikundi cha kimataifa kinachohusika na Njia kimeundwa tangu 2018 na Kiko Argüello -mwajibikaji wa Njia–, María Ascensión Romero, na P. Mario Pezzi. Tangu mwanzo wa Njia mnamo 1964, na hadi 2016, kiliundwa na Kiko Argüello na Carmen Hernández, waanzilishi wake, na pia na P. Mario Pezzi. Baada ya Carmen kufariki mnamo Julai 19, 2016, na kama ilivyoandikwa katika Statuta za Njia, María Ascensión Romero alijiunga na kikundi hicho. Kikundi hiki kinasimamia uongozi wa Njia ya Neokatekumenato duniani kote, wakishirikiana na vikundi vya makatekista wasafiri katika kila taifa. Miongoni mwa majukumu yake yapo yale ya kuongoza utekelezaji wa Njia ya Neokatekumenato na kudhamini uhalisi wake; kutimiza wajibu wao wenyewe, kama ulivyoelekezwa katika Statuta rasmi; kuomba mashauriano ambayo yanachukuliwa kuwa yanafaa; kudumisha mahusiano ya mara kwa mara na Maaskofu wa jimbo; kudumisha mahusiano ya mara kwa mara na Idara ya Walei, Familia na Uhai kutoka Kiti kitakatifu, pamoja na majukumu mengine.