«Regina Coeli» (Malkia wa Mbingu) ya Papa Fransisko kwa utume nyanjani huko Roma 7-4-2013
Fransisko
Ndugu wapendwa, habari za asubuhi!
Mwinjili Yohana anatuonyesha, katika Dominika hii ya 4 ya kipindi cha Pasaka, sura ya Yesu Mchungaji Mwema.
Tukitafakari ukurasa huu wa Injili, tunaweza kuelewa aina ya uhusiano ambao Yesu alikuwa nao na wanafunzi wake: uhusiano unaosimama katika upole, katika upendo, katika kujuana na katika ahadi ya kipaji kisichopimika: “Mimi nimekuja,” asema Yesu, “ili wawe na uzima na wawe nao tele” (Yn 10, 10). Uhusiano kama huo ni kielelezo cha mahusiano kati ya wakristo na cha mahusiano ya kibinadamu.
Leo pia, kama ilivyokuwa wakati wa Yesu, wengi hujipendekeza kama “wachungaji” wa maisha yetu; lakini Mfufuka tu ndiye Mchungaji wa kweli anayetupatia uzima tele. Ninawaalika nyote kuwa na imani katika Bwana anayetuongoza. Lakini si tu kutuongoza: anatusindikiza, anatembea nasi. Tusikilize neno lake pamoja kwa akili na moyo wazi, ili kulisha imani yetu, kuangaza dhamira yetu na kufuata mafundisho ya Injili.
Dominika hii tuwaombee wachungaji wa Kanisa, maaskofu wote, pamoja na askofu wa Roma, mapadre wote, wote. Hasa, tuwaombee mapadre wa jimbo la Roma, ambao nimewapadrisha hivi punde katika basilika ya Mtakatifu Petro. Salamu kwa mapadre hawa kumi na watatu. Bwana na atusaidie sisi, wachungaji, kuwa waaminifu daima kwa Bwana na kuwa viongozi wenye hekima na walioangaziwa kwa ajili ya taifa ambalo Mungu amekabidhi kwetu. Ninyi pia, nawaomba mtusaidie: mtusaidie kuwa wachungaji wema. Wakati fulani nilisoma kitu kizuri sana kuhusu jinsi taifa la Mungu wanavyosaidia maaskofu na mapadre kuwa wachungaji wema. Ni maandishi ya Mtakatifu Caesarius wa Arles, Baba wa Kanisa wa karne za kwanza za Kanisa. Alieleza jinsi taifa la Mungu wanavyohitaji kumsaidia mchungaji, na aliweka mfano huu: ndama anapokuwa na njaa anaenda kwa ng’ombe, kwa mama yake. Ili kunyonya. Lakini ng’ombe hampi mara moja: inaonekana kwamba anayazuia kwa ajili yake. Na ndama hufanya nini? Anaita na pua yake katika chuchu ya ng’ombe, ili maziwa yatoke. Picha nzuri kama nini! “Hivyo ndivyo”, anasema mtakatifu huyu, “mnavyopaswa kuwa pamoja na wachungaji: kubisha daima mlangoni mwao, moyoni mwao, ili wawape ninyi maziwa ya mafundisho, maziwa ya neema, maziwa ya mwongozo”. Na ninawaomba, tafadhali, mtusumbue wachungaji, mwasumbue wachungaji, wachungaji wetu wote, ili tuwape ninyi maziwa ya neema, ya mafundisho na ya mwongozo. Mtusumbue! Fikirieni juu ya picha hiyo nzuri ya ndama mdogo, jinsi anavyomsumbua mama yake ili amlishe.
Kwa kumwiga Yesu, kila mchungaji “mara nyingine atakuwa mbele ili kuonyesha njia na kutunza matumaini ya watu -mchungaji lazima wakati mwingine atangulie-, mara nyingine atakuwa tu katikati ya wote pamoja na ukaribu wake rahisi na wenye huruma, na wakati mwingine itambidi kutembea nyuma ya taifa ili kuwasaidia wanaovunjika moyo” ( Wosia wa Kitume Evangelii Gaudium, 13).
Laiti wachungaji wote wawe hivyo! Lakini ninyi mwasumbue wachungaji, ili wawape ninyi mwongozo wa mafundisho na wa neema.
Jumapili hii inaadhimishwa Siku ya Kuombea Miito Duniani. Katika Ujumbe wa mwaka huu nimekumbusha kwamba “kila wito (…) inahitaji daima kuanzisha mwendo wa kutoka katika wao wenyewe ili kumweka Kristo katikati ya maisha yao pamoja na Injili yake” (Na. 2). Ndiyo maana wakati huo huo wito wa kumfuata Yesu unakuwa kipindi cha kusisimua na cha kujihusisha. Ili itekelezwe, ni lazima daima kuanzisha urafiki wa kina na Bwana ili kuweza kuishi kutoka Kwake na kwa ajili Yake.
Tuombe ili pia katika wakati huu vijana wengi wasikie sauti ya Bwana, ambayo daima ina hatari ya kuzamishwa na sauti nyingine nyingi. Tuwaombee vijana: labda hapa, katika uwanja huu, yupo mtu anayesikia sauti hii ya Bwana ikimwita kwa upadre; tumuombee, ikiwa yuko hapa, na kwa ajili ya vijana wote wanaoitwa.
Baada ya “Regina Coeli” (Tenzi kwa Bikira Maria “Malkia wa Mbingu”, kwa kilatini)
Ndugu wapendwa:
Ninawasalimu ninyi nyote, familia, vikundi vya parokia, vyama na waamini kutoka Italia na nchi nyingi (…).
Salamu kwa Jumuiya za Neokatekumenato, ambao katika Jumapili hizi za kipindi cha Pasaka wanabeba tangazo la Yesu mfufuka katika viwanja/nyanja 100 hapa Roma na katika majiji mengi ya dunia. Bwana awape furaha ya Injili! Na songeni mbele, ninyi mliojaa ujasiri!
Baraka maalum kwa watoto na vijana wadogo ambao wamepokea au wanakaribia kupokea komunyo ya kwanza na kipaimara. Na pia kwa wanafamilia na marafiki wa mapadre wapya wa jimbo la Roma, niliowapadrisha asubuhi hii ya leo.
Na leo ninawaalika kuwatolea kumbukumbu nzuri/rembo/nyororo na sala kwa akina mama wote. Tuwasalimie akina mama! Tukiwakabidhi kwa mama yake Yesu, tumuombe Bikira kwa ajili mama zetu na kwa akina mama wote: “Salamu Maria…”.
Salamu kubwa kwa akina mama wote, salamu kubwa!
Jumapili njema kwa wote! Mlo mwema, tutaonana tena!