Mnamo mwaka wa 2006, Benedikto XVI alizindua aina hii mpya ya uinjilishaji kwa kutuma missio ad gentes 7 za kwanza. Kila moja imeundwa na mpresbiteri, akisindikizwa na familia 4 ama 5 zilizo na watoto kadhaa. Kwa ombi la askofu, familia inapokea wajibu wa kuinjilisha katika maeneo yaliyopoteza ukristo au ya kipagani, pamoja na utume wa kuonyesha jumuiya ya kikristo ambamo “wawe kitu kimoja ili ulimwengu upate kusadiki.”
Yohane Paulo II, kwenye Kongamano la VI la Maaskofu wa Ulaya la 1985, alielekeza kwamba ili kukabiliana na uduniaisho wa Ulaya ilikuwa ni lazima kurejea mfano wa kitume wa kwanza.

Hivyo, missio ad gentes hizi, kwa kuiga domus ecclesiae (“nyumba-kanisa”), wanakutana majumbani kati ya wasiobatizwa na waliotengwa.
Miaka kumi na miwili baada ya kutuma kwa mara ya kwanza matokeo yake ni kwamba wengi waliotengwa na wapagani ambao hawakuwahi kuingia kanisani wanajikaribisha kwenye jumuiya hizi za kikristo na kuanza safari ya wongofu ama ya kurudi kwenye imani.
Jumuiya hizi – ambazo hazijatokea kutoka eneo wakfu, bali zinaishi katikati ya ulimwengu- zinageuka kuwa”uwanda wa Mataifa ambapo watu wanaweza kumkaribia Mungu bila kumjua”, kama Benedikto XVI alivyoeleza katika hotuba yake kwa Watendaji wa Roma mnamo 2009.
Kipengele cha ajabu cha maang’amuzi haya ni matunda ya ushirika na umoja yanayotokea ndani ya familia yenyewe, kati ya wazazi na watoto.
Mnamo tarehe 18 Machi 2016, Papa Fransisko alituma familia 250 akiunda missio ad gentes 50 mpya kwa mabara matano. Wakati wa mkutano huu, Fransisko mwenyewe alieleza mtindo huu wa kimisionari unamaanisha nini: “missio ad gentes zinaundwa kwa ombi la maaskofu wa majimbo wanapokusudiwa na zinaundwa na familia 4 hadi 5 – wengi wao wakiwa na zaidi ya watoto wanne–, mpresbiteri, kijana na dada wawili. Wote wanaunda jumuiya ambayo ina utume wa kutoa ishara za imani zinazowavutia watu kwa uzuri wa Injili”, alieleza.
Papa Benedikto XVI, kutoka 2006 hadi 2012, alituma missio ad gentes 58 na Papa Fransisko ametuma 128.
Mei 5, 2018 kwenye mkutano wa kimataifa wakati wa kuadhimisha miaka 50 ya kuzaliwa kwa jumuiya ya kwanza ya Njia huko Roma, iliyoadhimishwa huko Tor Vergata (Roma), Papa Fransisko alituma missio ad gentes 34 mpya.
Idadi ya familia kwenye Njia zilizo katika utume kwa uinjilishaji mpya ni 1,668, zenye watoto takriban 6,000, katika nchi 108 kwenye mabara 5, tukihesabu pia missio ad gentes 216 katika mataifa 62.