Mmewasha moto wa Injili pale ambapo ulionekana kuzimika.
Papa Leo XIV



Papa Leo XIV akutana na Makatekista 1.000 kutoka Njia ya Neokatekumenato
Asubuhi ya leo, 19 Januari 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV, katika “Ukumbi wa Baraka” aliwapokea makatekista wasafiri zaidi ya 1,000, wawajibikaji wa Njia ya Neokatekumenato katika mataifa 138 katika mabara yote matano.
Mwishoni mwa kuishi pamoja, iliyofanyika katika Kituo cha “Mtumishi wa Yahweh” huko Porto San Giorgio (Italia), chini ya mwongozo wa kikundi cha wawajibikaji wa Njia duniani kote, Kiko Argüello, Padre Mario Pezzi na María Ascensión Romero, wamekutana mjini Roma kwa mkutano wao wa kwanza pamoja na Baba Mtakatifu Leo XIV.
Katika kuishi pamoja, kama inavyofanyika kila mwaka tangu mwanzo wa Njia , wameshirikishana maang’amuzi ya uinjilishaji ambao Njia inatekeleza katika zaidi ya parokia 6,200 katika majimbo 1,408 ulimwenguni, ili kuhimiza uingizwaji wa kikristo, chombo kinachowasaidia maaskofu na mapadre wa nchi mbalimbali katika kazi ya tangazo la Injili katika dunia ya leo.
Pia walihudhuria mkutano huo na pamoja na Baba Mtakatifu magombera 115 wa Seminari za Kijimbo za Kimisionari ambazo Njia imesaidia kufungua katika majimbo mengine mengi zaidi, pamoja na walezi wapatao mia.
Katika kuishi pamoja imewezekana kuthibitisha, kupitia maang’amuzi mbalimbali katika mabara tofauti, hali ngumu ambamo Kanisa la leo limeitwa kuendeleza utume wake. Katika muktadha huu wa kidunia, imeonekana waziwazi kwamba Njia ya Neokatekumenato imeitwa kuchangia katika amani na maelewano kati ya watu, ikileya matumaini ya tangazo la kikristo, la kerygma, na ikiunda jumuiya za kikristo zenye uwezo wa kutoa ishara za imani kwa kizazi hiki, upendo na umoja.
Kufika na kuondoka kwa Papa kumesindikizwa na makofi mengi na shangwe, kama vile nyimbo za Kiko Argüello ambazo kusanyiko zima limeimba kwa shauku.
Kiko amempa Baba Mtakatifu nakala ya mchoro wa Mchungaji Mwema, uliochorwa na yeye mwenyewe mwaka 1982. Aidha, na kwa wakati mwafaka, kwa vile Papa amepanga ziara huko Hispania katika miezi ijayo, Kiko amempa pia makala kuhusu Kanisa Kuu la Madrid, Bikira Maria Mama wa Almudena, ambapo mwaka 2004 Kiko alichora “taji la kifumbo” (mpangilio wa michoro mbalimbali inayoeleza historia ya wokovu katika Kristo), pamoja na madirisha ya vioo yenye michoro yaliyoko kwenye dari juu ya madhabahu.



Papa Leo alisema nao waliohudhuria kwa maneno yafuatayo:
Ningependa kutoa shukrani zangu kwa familia zote ambazo, kwa kukaribisha msukumo wa ndani wa Roho, wanaacha usalama wa maisha ya kawaida na kuondoka katika utume, hata katika maeneo ya mbali na magumu, kwa hamu tu ya kutangaza Injili na kuwa mashahidi wa upendo wa Mungu.
Vikundi vya wamisionari wasafiri, vilivyounda na familia, makatekista na mapadre, wanashiriki katika utume wa Kanisa zima wa kuinjilisha na… vinachangia “kuamsha” imani ya wasio wakristo ambao hawajawahi kusikia habari za Yesu Kristo.
Kuishi maang’amuzi ya Njia ya Neokatekumenato na kutekeleza utume huo kunadai pia, kwa upande wenu, kuwa macho ndani yenu na uwezo wa kupambanua kwa hekima, ili kutambua baadhi ya hatari ambazo daima zinatishia maisha ya kiroho na ya kikanisa .
Karama zinawekwa daima kwa huduma ya Ufalme wa Mungu na ya Kanisa pekee la Kristo, ambamo hakuna kipawa cha Mungu kilicho muhimu zaidi kuliko vingine.
Mema mnayofanya ni makubwa, kwa sababu kusudi lake ni kuwawezesha watu kumjua Kristo.
Songeni mbele kwa furaha na unyenyekevu, bila kujitenga, kama wajenzi na mashahidi wa ushirika.
Wapendwa, nawashukuru kwa juhudi yenu, kwa ushuhuda wenu wenye furaha na kwa huduma mnayotoa katika Kanisa na duniani. Ninawatia moyo mwendelee kwa shauku na ninawabariki, huku nikiita juu yenu maombezi ya Bikira Maria ili awasindikize na kuwalinda. Asanteni!




HADHIRA PAMOJA NA WAWAJIBIKAJI WA NJIA YA NEOKATEKUMENATO
Ukumbi wa Baraka (Ukumbi wa Paulo VI)
Jumatatu, tarehe 19 Januari 2026
Kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu.
Amani iwe kwenu!
Ndugu wapendwa, za asubuhi! Karibuni!
Nimefurahi kukutanana nanyi mkiwa wengi hivi. Nawasalimu ninyi ndugu wa Kikundi cha Kimataifa cha Njia ya Neokatekumenato, Kiko Argüello, María Ascensión Romero, na Padre Mario Pezzi, pamoja na maaskofu na mapadre wanaowasindikiza.
Wazo maalum linaenda kutoka kwangu kwa familia zilizopo hapa, ishara ya hamu yenu ya kimisionari na shauku ambayo inapaswa kuhuisha Kanisa zima kila wakati: kutangaza Injili kwa ulimwengu mzima, ili wote wapate kumjua Kristo.
Hamu hiyo hiyo imekuwa ikihuisha na inaendelea kulisha maisha ya Njia ya Neokatekumenato, karama yake na kazi za uinjilishaji na katekesi zinazoakisi mchango wenye thamani kwa ajili ya maisha ya Kanisa. Kwa wote, hasa kwa wale ambao wameenda mbali au ambao imani yao imedhoofika, mnawapa uwezekano wa safari ya kiroho inayowaruhusu kugundua tena maana ya Ubatizo, ili waweze kutambua kipawa cha neema walichopokea na, hivyo, wito wa kuwa wanafunzi wa Bwana na mashahidi wake duniani.
Mkihimizwa na roho hii, mmewasha tena moto wa Injili pale ambapo ulionekana kuzimika, na mmesindikiza watu wengi na jumuiya za kikristo, mkiwaamsha kwa furaha ya imani, mkiwasaidia kugundua upya uzuri wa kumjua Yesu, na kuendeleza ukuaji wao wa kiroho na wito na wajibu wao wa kushuhudia.
Kwa namna ya pakee, pamoja na walezi na makatekista, ningependa kutoa shukrani zangu kwa familia ambazo, kwa kupokea msukumo wa ndani wa Roho, zinaaacha usalama wa maisha ya kawaida na kwondoka katika utume, hadi katika maeneo ya mbali na magumu, kwa hamu pekee ya kutangaza Injili na kushuhudia upendo wa Mungu. Kwa njia hii, vikundi vya makatekista wasafiri, vinavyoundwa na familia, makatekista, na mapadre, vinashiriki katika utume wa kuinjilisha wa Kanisa zima na, kama Papa Fransisko alivyothibitisha, vinachangia “kuamsha” imani ya “wasio Wakristo ambao hawajawahi kusikia kuhusu Yesu Kristo,” lakini pia Wakristo wengi waliobatizwa ambao, ingawa ni Wakristo, “wamesahau […] Yesu Kristo ni nani” (Hotuba kwa ndugu wa Njia ya Neokatekumenato, Machi 6, 2015).
Kuishi maang’amuzi ya Njia ya Neokatekumenato na kutekeleza utume wake pia kunahitaji, kwa upande wenu, hali ya kukesha ndani yenu, pamoja na uwezo wa kupambanua kwa busara, ili kuweza kutambua baadhi ya hatari ambazo zinajificha na kutishia kila wakati katika maisha ya kiroho na ya kikanisa.
Ninyi mnapendekeza kwa wote njia ya kugundua upya Ubatizo, na Sakramenti hiyo, kama tunavyofahamu, ikituunganisha na Kristo, inatufanya kuwa viungo hai vya Mwili wake, taifa lake pekee, familia yake pekee. Lazima tukumbuke daima kwamba sisi ni Kanisa na kwamba, hata ikiwa Roho atampa kila mtu udhihirisho au ufunuo fulani, huo unatolewa—kama Mtume Paulo anavyotukumbusha—“kwa manufaa ya wote” (1 Kor 12:7) na, kwa hiyo, kwa ajili ya utume wenyewe wa Kanisa. Karama lazima ziwekwe katika huduma ya Ufalme wa Mungu na Kanisa moja na pekee la Kristo, ambamo hakuna kipawa cha Mungu kilicho muhimu zaidi kuliko kingine—isipokuwa upendo, unaokamilisha na kuoanisha mambo yote—na hakuna huduma inayopaswa kuwa sababu ya kujisikia bora kuliko ndugu na kuwatenga wale wanaofikiri tofauti.
Kwa sababu hii, ninawaalika ninyi pia, ambao mmekutana na Bwana na kumfuata katika Njia ya Neokatekumenato, kuwa mashahidi wa umoja huu. Utume wenu ni wa pekee, lakini si wa peke yenu tu; karama yenu ni ya kipekee, lakini inazaa matunda katika ushirika na vipawa vingine vilivyopo katika maisha ya Kanisa; mema mnayofanya ni makubwa, lakini kusudi lake ni kuwaongoza watu kumjua Kristo, mkiheshimu daima safari ya maisha na dhamiri ya kila mtu.
Mkiwa walinzi wa umoja huu katika Roho, ninawasihi kuishi tasaufi yenu bila kujitenga kamwe na mwili mzima wa kikanisa, mkiwa sehemu hai ya kazi ya kawaida ya kichungaji ya parokiani na ya hali zao mbalimbali, katika ushirika kamili na ndugu, hasa na mapadre na maaskofu. Songeni mbele kwa furaha na unyenyekevu, bila kujitenga, mkiwa wajenzi na mashahidi wa ushirika.
Kanisa linawasindikiza, linawategemeza, na linashukuru kwa yale mnayoyafanya. Wakati huo huo, linawakumbusha wote kwamba “palipo na Roho wa Bwana, hapo uhuru upo” (2 Kor 3:17). Hivyo, tangazo la Injili, katekesi, na aina mbalimbali za shughuli za kichungaji zinapaswa kuwa bila aina yoyote ya shuruti, mawazo finyo, au masharti ya maadili, ili zisije zikasababisha hisia za hatia na hofu badala ya uhuru wa ndani.
Wapendwa, ninawashukuru kwa kujitolea kwenu, ushuhuda wenu wenye furaha, na kwa huduma mnayotoa katika Kanisa na ulimwengu. Ninawatia moyo muendelee kwa shauku na ninawabariki, huku nikiomba maombezi ya Bikira Maria ili awasindikize na kuwalinda. Asanteni!
