Kiko Argüello
Francisco José Gómez de Argüello Wirtz, alizaliwa León mnamo Januari 9, 1939. Alisomea Sanaa katika Chuo cha San Fernando huko Madrid na mwaka wa 1959 akapokea Tuzo ya Kitaifa ya Pekee ya Uchoraji. Baada ya dhahama kubwa ya kiutu, uongofu mkubwa ulifanyika ndani yake ambao ulimpeleka kutoa maisha yake kwa Kristo Yesu na kwa Kanisa.
Mnamo 1960, pamoja na mchongaji sanaa Coomontes na mchoraji wa vioo Muñoz de Pablos, alianzisha kikundi cha utafiti na maendeleo ya Sanaa Wakfu “Gremio 62”. Alifanya maonyesho huko Madrid (Maktaba ya Taifa na mnamo 1964 anaiwakilisha Hispania, akiteuliwa na Wizara ya Utamaduni, katika Maonyesho ya ya Sanaa Takatifu Ulimwenguni huko Royan (Ufaransa). Huko Uholanzi (1965) alionyesha baadhi ya kazi zake (Nyumba ya sanaa “Sura mpya” ).
Akisadikishwa kwamba Kristo yupo katika mateso ya wasio na hatia na walio wa mwisho wa dunia, mwaka 1964 anaenda kuishi kati ya maskini, akienda kwenye kibanda kimoja huko Palomeras Altas, nje kidogo ya Madrid. Huko alimfahamu Carmen Hernández, na wote wawili, wakiongozwa na mazingira ya watu maskini, waligundua namna ya mahubiri, muhtasari kikerigma-kikatekesi, ambao uliwezesha uundaji wa jumuiya ndogo ya Kikristo. Jumuiya hii, ambamo upendo wa Kristo msulubiwa ukaonekana, ukawa “mbegu” ambayo, shukrani kwa Askofu Mkuu wa Madrid wakati huo, Mons. Casimiro Morcillo, ilipandwa katika parokia za Madrid na baadaye za huko Roma na za mataifa mengine.
Baada ya uongofu wake aliweka sanaa yake kwa huduma ya Kanisa. Hasa, kwa njia ya uchoraji, muziki, usanifu majengo na uchongaji; hizi mbili za mwisho kwa lengo la kusambaza “uzuri mpya” ambao umewaongoza watu kwenye imani.
Kama mchoraji, amefanya kazi muhimu popote duniani . Huko Hispania, hasa Madrid – linatokeza hasa “taji la kifumbo” la Kathedrali yake- au huko Murcia. Huko Italia hivi karibuni amechora picha kubwa ukutani ndani ya Seminari ya Redemptoris Mater ya Roma. Kazi zake zipo katika parokia za Roma, kama ya Mashahidi wa Kanada, na katika miji kama Piacenza na Perugia. Mfano mwingine ni picha kubwa ukutani kuhusu Hukumu ya Mwisho katika Domus Galilee (Israel), kituo kilichopo juu ya Mlima wa Heri na ambao kwa matakwa yenyewe ya Yohane Paulo II, kinatumika pia kujenga madaraja na taifa la kiyahudi.
Kama msanifu majengo ameunda mtindo mpya wa parokia na wa seminari unaosimama juu ya uzuri mpya na ambamo pia kuna madirisha ya vioo yaliyotengenezwa na yeye. Kuna mifano yake huko Hispania, Italia, Nicaragua, Marekani, Finland, Jamhuri ya Dominika, na baadhi ya nchi za Asia na Afrika. Kwa maana hii, inatokeza hasa nyumba ya Domus Galilee
Katika miaka hii, Kiko Argüello ametunga sura ya kimuziki kwa ajili ya Njia ya Neokatekumenato . Tangu alipokwenda vibandani vya Palomeras Altas akibeba Biblia na gitaa, ametunga zaidi ya nyimbo 300 ambazo zimekusanywa katika kinachojulikana kama “AMEFUFUKA, nyimbo kwa ajili ya Jumuiya za Neokatekumenato”. Baadhi zinaimbwa leo katika parokia nyingi duniani kote na nyingine zimeimbwa mara nyingi mbele ya Mapapa mbalimbali. Kwa ajili yao, Kiko amebuni usindikizaji wa muziki akitumia idadi kubwa ya ala.
Mnamo 2010, Argüello aliunda Okestra ya kisinfonia ya Njia ya Neokatekumenato na ametunga “Mateso ya wasio na hatia”, ambayo inaelezea kwa njia ya muziki maumivu ya Bikira Maria akiwa chini ya msalaba. Baada ya kuimbwa huko Israeli mbele ya mamlaka mbalimbali na maaskofu 200, waebrania, wakishangazwa mno, walitambua kuwa wanaeleweka na kupendwa na Kanisa mbele ya maumivu ya Shoah (Mauaji ya kimbari). Baada ya hapo, inatumika kama daraja la mazungumzo kati ya wayahudi na Kanisa Katoliki. Tangu utungaji wake, imeimbwa katika mahali kama vile Vatikano -wakati mmoja mbele ya Benedikto XVI–, Jerusalem, Bethlehemu, Madrid, Paris, Tokyo, New York, Chicago, Boston, Düsseldorf au Auschwitz, na pengine.
Kiko Argüello pia ni mwandishi wa vitabu viwili: mnamo 2012 alichapisha “Kerigma, katika vibanda pamoja na maskini” na mwaka wa 2016 “Noti. 1988-2014”.