Tamasha la Neocatechumenal Way katika programu ya jalada ya Novemba 2023 ya Trieste "The Messiah"

Trieste, Italia – 19 Novemba 2023 – saa mbili usiku.

Shairi la kisinfonia linalotolewa kwa ajili ya mashahidi.

Jumapili tarehe 19 Novemba, saa mbili usiku, katika Teatro Verdi huko Trieste (Italia) onyesho mashuhuri la kwanza duniani litafanyika.

Kipengele cha kwanza ni simfonia yenyewe ya “Masiya”, ambayo inaundwa na sehemu tatu: “Akeda”, “Binti za Yerusalemu” na “Masiya, simba kwa kushinda”. Katika hizi tatu kuna hewa ya kisimfonia ambapo kinanda kinachukua sehemu kubwa.

Majina hayo yanarejelea vipindi vitatu vya Historia ya Wokovu: Sadaka ya Isaka iliyofanywa na baba yake, Abrahamu. “Akeda”, neno la Kiebrania linalomaanisha “Nifunge”, ni neno ambalo Isaka anasema kwa baba yake ili sadaka yake ikubalike; na kilio cha malaika, wanaotangaza: “Njooni mkaone imani juu ya nchi.” “Akeda”, Fumbo la imani: zawadi ya Mungu kwa mwanadamu.

La pili: “Binti za Yerusalemu” ni maneno ya Kristo kwa wanawake wanaomsindikiza kwenye njia ya Msalaba, ili wasimlilie Yeye, bali kwa ajili yao wenyewe na watoto wao.

La tatu: “Masiya, simba kwa kushinda”, ni maneno ya shahidi mkristo mmoja wa karne ya 4, Victorinus wa Pettau, ambaye anafunua na kutangaza kwa ushairi Fumbo la Kristo, ambaye, akiwa amekuja kama simba ili kushinda, anajifanya mwanakondoo akibeba uovu wa mwanadamu, ili kumpitisha kutoka mauti hadi uzima.

Maudhui ya kikerigma ambayo yanamtangazia mkristo wa leo njia ya kuishi katika historia: kumsindikiza Kristo Msalabani, kubeba dhambi ya mwanadamu, kujifanya mwanakondoo, kumpenda mwingine hadi kutoa uhai kwa ajili yake. Kila mkristo, aliyeungana na Kristo, anaitwa kugeuka shahidi, kuwa ushahidi wa upendo huu.

Kipengele cha pili cha kuangazia katika onyesho hili la kwanza duniani ni mwandishi wake, Kiko Argüello, mtunzi wa simfonia nyingine: “Mateso ya wasio na hatia”, ambayo ilikuwa na mvumo na umuhimu wa kimataifa. Ilifanyika kwenye majukwaa ya majumba ya maonyesho na katika kumbi mbalimbali za matamasha duniani kote: Madrid, New York Metropolitan, Chicago Symphony Hall, Berliner Philharmoniker Hall – Berlin, Gerard Behar Auditorium – Jerusalem, Suntory Hall – Tokyo, Hungarian State Opera – Budapest. , Tamasha la Ukumbusho – Auschwitz, Uwanja wa Umoja wa Italia – Trieste, nk.

Mwandishi ni mchoraji mhispania ambaye alizaliwa León mnamo Januari 9, 1939. Alisomea Sanaa katika Chuo cha San Fernando huko Madrid na mnamo 1959 akapokea Tuzo ya Kitaifa ya Pekee ya Uchoraji. Mwanzoni mwa miaka ya 1960 aliishi dhahama kubwa ya kiutu iliyomsababishia wongofu wa kina, uliompelekea kutoa maisha yake kwa Kristo na kwa Kanisa.

Mnamo 1964 aliamua kuishi miongoni mwa maskini kwenye kibanda nje kidogo ya Madrid. Katika hali hiyo ya kuwekwa kando, Kiko alikutana na uwepo wa Kristo msulubiwa.

Baadaye alikutana na mmisionari, Carmen Hernández , mwenye shahada ya Kemia na Teolojia, na leo ni Mtumishi wa Mungu, ambaye pamoja naye alihuisha aina mpya ya mahubiri ambayo baada ya muda mfupi yalisababisha kuzaliwa kwa jumuiya ya kikristo. Hivyo katikati ya maskini jumuiya ya kwanza ya neocatekumenato ilizaliwa, ambamo upendo wa Kristo msulubiwa ulionekana.

Mbegu hii ilianza kuota kwanza huko Hispania, katika baadhi ya parokia za Madrid, na baada ya mang’amuzi ya Kiko kati ya maskini wa nje kidogo ya Roma, katika Borghetto Latino, ikaenea baadaye nchini Italia; na kutoka Hispania na Italia ikasambaa duniani kote. Leo, katika mabara yote matano, katika nchi 135, kuna Jumuiya za Neokatekumenato zaidi ya 20,000.

Zaidi ya miaka 50 iliyopita, mwaka wa 1971, Kiko na Carmen walituma kikundi cha makatekista wasafiri kwenda Trieste na katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Justus Shahidi jumuiya ya kwanza ya neokatekumenato ilizaliwa.

Kwa hivyo, Kiko Argüello na Carmen Hernández ni waanzilishi wa Njia ya Neokatekumenato, uingizwaji wa kikristo kijimbo, ambayo, kwa njia ya katekesi, Neno la Mungu na Sakramenti wanazoishi kama jumuiya, huwaongoza watu kwenye imani pevu na ushirika wa kindugu.

Mnamo 2008, Kiti Kitakatifu kiliidhinisha Statuta za Njia ya Neokatekumenato, inayotambuliwa na Mapapa kadhaa kama “zawadi ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa la leo.”

Kiko Argüello, pamoja na kuwa mwanzilishi wa mkondo huu wa kikanisa, na mtunzi wa simfonia hizi mbili, ni mbunifu pia wa michoro, usanifu na uchongaji muhimu ulimwenguni kote: Kathedrali ya Madrid , Parokia ya Mtakatifu Bartholomayo huko Tuto, (Scandicci, Florence), Kanisa la Seminari ya Redemptoris Mater ya Roma, Parokia ya Mtakatifu Katerina Labouré huko Madrid, Seminari ya Redemptoris Mater ya Macerata (Italia) na Warsaw (Poland), Senta ya Neokatekumenato ya Porto San Giorgio (Italia), Senta ya Kimataifa ya “Domus Galilaeae” juu ya Mlima wa Heri kwenye Nchi Takatifu, nk. Kupitia uchoraji, unaotungwa kama kiakisi cha nuru ya Mungu, na pia kupitia muziki, lugha inayozungumzwa ulimwenguni pote inayoweza kufungua moyo kwa ulimwengu wa kiroho, Kiko anapata njia ya kutangaza Injili kwa mwanadamu wa kisasa. Anaweka wito wake wa kisanii kwa huduma ya Kanisa na Liturjia, anaweka muziki katika Zaburi, vifungu vya Maandiko Matakatifu, tenzi za Kanisa la mwanzo na pia mashairi ya kiroho yaliyotokana na maandishi yake mwenyewe.

Kipengele cha tatu cha kuangazia kutoka katika onyesho hili huko Trieste ni okestra. Ilianzishwa na Kiko mwaka 2010 ili kucheza tungo ya kwanza: “Mateso ya wasio na hatia”. Washiriki wa Okestra na wa Kwaya, wanamuziki takriban 180 kutoka Italia, Hispania na mataifa mengine, wote ni wasanii ambao wanatolea vipaji vyao bila malipo kwa huduma ya Uinjilishaji Mpya. Utume kama namna inayoonyesha uzuri kupitia muziki ili kutangaza na kutoa ushuhuda wa Injili ulimwenguni kote.

Mwongozaji wa okestra ni Tomáš Hanus, mzaliwa wa Brno, Jamhuri ya Czech. Tangu msimu wa 2016-2017 amekuwa na wadhifa wa mwongozaji wa kimuziki wa Opera ya Kitaifa ya Wales (Uingereza). Ameongoza katika majumba ya opera za kifahari zaidi na makumbi ya matamasha ya kimataifa kama vile Bayerische Staatsoper, Opera ya Paris, Grand Théâtre huko Geneva, Teatro Real ya Madrid, Philharmonic ya Berlin, na amekuwa kwenye jukwaa la Royal Philharmonic Orchestra, London Symphony Orchestra na BBC Symphony Orchestra. Mwezi wa Juni mwaka jana alicheza kwa mara ya kwanza kwenye jukwaa la La Scala huko Milan.

Onyesho la kwanza duniani la tungo hii bila shaka ni upendeleo kwa Teatro Verdi na kwa jiji la Trieste.Share: