Habari za hivi punde: Takwimu rasmi kutoka kwa ulinzi wa raia na polisi wa Lisbon zinathibitisha mahudhuria¡o ya zaidi ya watu 100,000 kwenye mkutano wa miito

VIJANA WA NJIA YA NEOKATEKUMENATO WAJAZA MIJI YA ULAYA KWA NYIMBO.

Toleo la 37 la Siku ya Vijana Duniani (Lisbon, Agosti 1-6, 2023) lilikuwa na dakika ya mwisho ya furaha ya ajabu katika mkutano wa Vijana zaidi ya elfu sabini na tano wa Njia ya Neokatekumenato, waliowasili kutoka duniani kote, pamoja na Kikundi cha Wawajibikaji cha Kimataifa, Mwanzilishi Kiko Argüello, Padre Mario Pezzi na Ascensión Romero.

Tangu mwanzo wa Siku za Vijana Duniani (Roma 1986), Kiko na Carmen waliona kwamba hija hizo zinawapa vijana wa Njia fursa kubwa: baada ya kuhiji wakijiandaa kwa ajili ya mikutano na Baba Mtakatifu, vijana wanakutana na Askofu mahalia pamoja na Maaskofu wengine, ili kurusha nyavu na kwa adhama kuu kuitisha miito kwa upresbiteri, maisha ya kitawa na ya kimisionari, kwa kuunda familia za kikristo na kuziitisha familia hizo zenyewe kwenye utume.

Wakati wa hija ya SViD huko Cologne (2005), Kiko na Carmen pia walipata wazo kwamba, pamoja na sala na kusikiliza Neno katika siku hizi, vijana watumwe kwa utume wa kutangaza Injili katika miji walipopitia katikasafari zao.

Pia mwaka huu, huko Hispania – nchi ya mpito ili kufikia Lisbon – na vile vile huko Ureno, maelfu na maelfu ya wavulana na wasichana walifika katika miji na viwanja vingi kuleta furaha na matumaini kwa kesho, ili nchi hizi zisisahau mizizi yao ya kikristo: ukristo ule uliowapatia historia yao, utamaduni wao na kila kitu kilichowafanya kuwa wakuu.

Katika miji hii yote ilivuma habari njema ya Injili, tangazo la tukio hilo lililoshtua na kuugeuza ulimwengu: habari njema ya ushindi wa Kristo juu ya kifo. Vijana walitoa uhuhuda wa mkutano wao na Yesu Kristo katika maisha yao wenyewe.

Hija hii iliwaunganisha pamoja katika mikutano mbalimbali na Baba Mtakatifu, Papa Fransisko, katika Mkesha na katika kushiriki Ekaristi ya mwisho jumapili asubuhi.

Alasiri ya siku iliyofuata, Agosti 7, ulifanyika mkutano wa vijana 75,000 wa Njia, kwenye Njia ya Bahari huko Algés, ulioongozwa na Patriaki wa Lisbon, Kard. Manuel José Macário do Nascimento Clemente, akisindikizwa na Balozi wa Papa nchini Ureno, Mons. Ivo Scapolo, na makardinali wengine sita: Jean-Claude Hollerich (Luxembourg), Gérald C. Lacroix, Askofu Mkuu wa Quebec (Kanada), Odilo P. Scherer, Askofu Mkuu wa São Paulo (Brazili), Sean P. O’Malley, Askofu Mkuu wa Boston (Marekani), Antonio M. Rouco Varela, Askofu Mkuu Mstaafu wa Madrid na maaskofu wengine 47. Mkuu wa Idara ya Walei, Familia na Uhai, Kard. Kevin J. Farrell alimtuma Dk. Paul Metzlaff, kutoka “Sekta ya Vijana,” kama mwakilishi wake.

Meya, Isaltino Morais, pamoja na wanachama kadhaa wa manispaa ya Oeiras, ambapo tukio hilo lilifanyika, pia waliheshimu mkutano huo na uwepo wao. Hapa ndipo mahali ambapo jumapili iliyopita Baba Mtakatifu aliwashukuru na kuwasalimia vijana 25,000 waliojitolea kusaidia katika SViD 2023.

Kwenye jukwaa, pamoja na Makardinali na Maaskofu, walikuwepo vikundi vya makatekista wasafiri kutoka mataifa 114 ambao wamewasindikiza vijana katika hija yao.

Mkutano wa Miito SViD 2023 Lisbon – Kiko Argüello na Pd. Mario Pezzi

Baada ya utangulizi na wimbo wa “Nakuja kukusanya,” Kiko aliwatambulisha vijana, akitaja nchi yao ya asili. Kisha, Kiko akawaalika wapresbiteri wengi kubeba sanamu ya Bikira wa Fatima katika maandamano hadi kwenye jukwaa, wakati wimbo “Shlom lej Mariam” uliimbwa—maneno ambayo Malaika alimwambia Mariamu kwa lugha ya kiaramayo (“Salamu, Maria”!)-. Upande wa pili wa jukwaa zilikuwepo msalaba mkubwa na picha ya mtumishi wa Mungu, Carmen Hernández Barrera, ambaye pamoja na Kiko alianzisha Njia na ambaye Jimbo kuu la Madrid lilimfungulia mchakato wa kutangazwa mwenye heri Desemba mwaka jana, na ambaye amekumbukwa mara kadhaa wakati wa mkutano.

Hii ilifuatwa na tangazo la sura ya pili ya Matendo ya Mitume, tangazo lililofanywa na Petro siku ya Pentekoste, ambalo lilifuatwa na tangazo la kerigma ya Kiko: “Nawatangazia habari inayotendeka sasa hivi: utu wa kimungu wenyewe, utu wa kimungu uliofunuliwa na kudhihirishwa katika Kristo ni kwamba Mungu ni Upendo kwako, Upendo kamili.”

Kiko aliwaalika vijana kutazama juu kwenye msalaba mkubwa jukwaani na kuuliza swali moja: “Je, mnajua hii inamaanisha nini?: Kwamba Mungu anakupenda! Mungu hawezi kujikana mwenyewe. Asili ya kimungu ni hilo haswa: anataka kuwa mmoja ndani yako, anataka kuwa ndani yako. Mungu yumo katika uumbaji wote, bali anataka kuwa ndani yako, si kama alivyo katika uumbaji, bali ndani katika Roho Mtakatifu, kama mtu, wote ndani yako, akijifanya mmoja nawe, ili ushirikishwe katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ambao ni Upendo. Upendo huu unakuzalisha upya, unakufanya kushiriki asili ya kimungu na kuasiliwa kama Mwana. Upendo huu wa kimungu ndani yako unakuwezesha kupenda.”

Kilio: “Kristo amefufuka,” kiligusa moyo kwelikweli kilipotolewa mara kadhaa na Kiko, ambapo wale vijana 75,000 waliitikia: “Kweli kweli amefufuka.”

Liturujia ya Neno ilihitimishwa kwa kuimba kwa adhama kuu Injili ya siku hiyo: kuzidishwa kwa mikate na samaki (Mt 14: 13-21) pamoja na homilia ya Kiongoza-ibada wa mkutano huo, Patriaki wa Lisbon.

María Ascensión Romero

Sehemu ya tatu ya mkutano, ile ya kuitisha miito, ilianza na wimbo wa “Carmen ’63” na utambulisho wa Kiko. Padre Mario Pezzi aliwapa vijana neno, akiwaalika wasiogope kutoa maisha yao kwa Bwana, akisimulia maang’amuzi yake mwenyewe ya zaidi ya miaka hamsini ya upresbiteri kwa furaha, aliyoshi katika mabara yote matano; Ascensión Romero—mmisionari nchini Urusi kwa miaka mingi—ambaye amekuwa sehemu ya Kikundi cha Wawajibikaji tangu 2018, alikumbuka maneno ya Papa mwishoni mwa homilia ya Jumapili: “Msiogope,” akiwapa vijana moyo kujiachia kwa Bwana.

Wakati huo, baada ya muda mfupi wa ukimya, wakati wa miito kuitishwa ulifika, tunda la siku hizo walizoishi. Kwanza, Kiko aliwaalika vijana wanaojisikia kuitwa kwa upresbtieri wasimame. Wakati uliimbwa “Nakuja kukusanya”, maneno yaliyotolewa kutoka sura ya 66 ya nabii Isaya ambayo yanatangaza kazi ya Bwana ambaye atakuja kukusanya mataifa yote, zaidi ya vijana 2000 walilikaribia jukwaa. Vijana hawa wataanza mchakato wa upambanuzi wa miito katika majimbo yao. Kisha, wito ulitolewa kwa wasichana ambao wanasikia wito kwa maisha ya kitaamuli au utume: 1,500 waliinuka na wakiimba “Wewe u mzuri” walilikaribia jukwaa. Hawa pia watasindikizwa na wapresbiteri na makatekista wao kwa ajili ya mchakato wa upambanuzi.

Juu ya vijana walioitikia wito huu na waliopanda kwenye jukwaa, kiongoza-ibada alimwita Roho Mtakatifu, na kila mmoja akapokea baraka kutoka Patriaki na Maaskofu waliokuwepo.

Mkutano ulihitimishwa na wimbo kwa Maria: “Ishara kuu ilitokea mbinguni” pamoja na baraka kutoka Patriaki.

Maana ya tukio hili, ya matunda haya, haiwezi kueleweka katika maana yakehalisi bila njia hiyo ya imani ambayo imewatayarisha: sio hisia ya muda mfupi, bali ni utendaji wa Mungu unaofanya kazi ndani ya mioyo yao kupitia uingizwaji wa kikristo mrefu na wa dhati, kwa miaka mingi, waliopitia katika jumuiya zao, katika parokia zao.

Mkutano wa Miito wa SViD 2023 Lisbon – Maandamano ya kuingia na Bikira wa Fátima
Share: