
Na Javier Lozano
Maandishi na picha: Jarida la Misión www.revistamision.com, makala imechapishwa katika toleo la 72.
Mtumishi wa Mungu Marta Obregón alikufa akiwa tu na umri wa miaka 22, akitetea hadi mwisho jambo la thamani zaidi alilokuwa nalo: usafi wake. Ushuhuda wa msichana huyu kutoka Burgos, ambaye kwa sasa yuko kwenye mchakato wa kutangazwa kuwa mwenye heri, unaleta neema kubwa kadhaa, hasa katika ulimwengu huu wa sasa ambao hauupi mwili thamani uliyonayo.
“Ninakuomba jambo moja tu: kwamba, lolote lile, unipe nguvu za kutosha kulikubali na kulitimiza. Nisijitenge kamwe na Wewe kwa sababu yake, bali likaze zaidi na zaidi kamba zinazonifunga Nawe. Kwa sababu nakuruhusu Wewe tu uniongoze. Wewe tu, Mungu wangu. Wewe unaniamulia na mimi ninakubali. Hivi ndivyo nitakavyopata heri.” Haya ndiyo aliyoyaandika muda mfupi kabla ya kifo chake mtumishi kijana wa Mungu, Marta Obregón (1969-1992), shahidi wa usafi wa mwili, aliuawa januari 21, 1992 huko Burgos akiwa na umri wa miaka 22 tu, akitetea usafi na ubikira wake kwa nguvu zake zote. Mchakato wake wa kutangazwa mwenye heri tayari uko Roma.
Mwaminifu hadi kifo
Marta alitekwa nyara na kuuawa mnamo januari 21, sikukuu ya Bikira Maria na ya Mtakatifu Anyesi, shahidi, na kwa njia inayofanana sana na Mtakatifu Maria Goretti, ambaye pia ni bikira na shahidi, kwani alipokea majeraha 14 ya kuchomwa kama yeye, kikionekana hivyo kifungo kikubwa kinachowaunganisha Marta na watakatifu hawa wawili wa nyakati tofauti.
“Kutetea hadi mwisho fadhila ya usafi wa kimwili haieleweki leo katika ulimwengu uliojaa itikadi isiyojizuia, inayotafuta raha na ya haraka, ambapo hakuna nafasi ya kufikiri kwamba maisha ya dunia ni sehemu ya kwanza tu ya maisha yetu na kwamba yanatusubiri maisha mengine ya pili, ya milele. Mungu, kwa kutuumba kwa mfano na sura yake, ametufanya kuwa wa milele. Kwa sababu hii, mwili wetu una thamani kubwa sana, zaidi ya maswala ya urembo au ya kutendeka, kwa sababu ndiyo makao ya roho zetu,” hivyo anaeleza Carlos Metola, mjumbe wa kamati inayoomba mchakato wa Marta kutangazwa kuwa mwenye heri, kwa ajili ya jarida Utume (Misión.)
“Marta alikuwa amekutana na Mungu, lakini aliendelea kumtafuta kwa ukaribu na kwa kina zaidi na zaidi”
Msichana huyu kutoka Burgos alifahamu vizuri sana jambo hili, kiasi kwamba katika uchaguzi wake kati ya uhai wake na usafi wake wa kimwili, hakusita kutoa uhai wake ili kulinda usafi wa mwili wake. Metola adokeza kwamba “kujikinga dhidi ya mbakaji huonekana kuwa jambo la kawaida, na kwa hakika ni jambo la kisilika, lakini haliko dhahiri sana kunapokuwa swala la kufa na kupona, kwa sababu mtu kuokoa uhai wake mwenyewe pia ni jambo la kisilika, pengine lenye nguvu zaidi kuliko kujilinda tu”. Lakini alipinga hadi mwisho katika kifo cha kishahidi. Kwa njia hii, anaongeza: “Marta hakukubali kujiingiza kwa sababu tayari alikuwa na mume wake na alitaka kuwa mwaminifu kwake hadi mwisho!”
Akimtafuta mpendwa wake
Marta alikuwa msichana aliyejaa maisha na shauku, aliyetabasamu na kujitolea. Alikuwa akisomea Uandishi wa Habari na alikuwa anamalizia shahada yake alipouawa. Kupitia kazi yake alitaka kufanya vile vile alivyofanya na maisha yake mwenyewe: “kuboresha ulimwengu.” Alikuwa msichana mwenye kujitoa mara na daima tayari kusaidia wengine. Alipata maang’amuzi yenye nguvu ya Mungu yaliyomgeuza kabisa, hasa katika miaka yake miwili ya mwisho ya uhai, baada ya kushinda hali ndogo ya msukosuko katika imani ambayo ilimpeleka mbali na Kanisa kwa muda.
“Marta alirudi kuwa kama zamani, ilikuwa wazi kwamba Mungu alikuwa amemfanya asing’ang’anie lolote: masomo, mpenzi, mipango… Namna yake ya kuwa, kwa maoni yangu, ilikuwa ya mwanamke ambaye alikuwa amempata Mungu, lakini aliendelea kumtafuta kwa ukaribu na kwa kina zaidi na zaidi” akasema rafiki yake, ambaye maneno yake yalikusanywa katika kitabu Marta Obregón, ‘Hágase’. Mimi ni kwa mpenzi wangu (Fonte Monte Carmelo, 2018), iliyoandikwa na padre Saturnino López, mwombaji katika ngazi ya kijimbo wa mchakato wake wa kutangazwa mwenye heri.
Wazazi wake, José Antonio na María Pilar, waliokuwa wa Opus Dei, walimptisha imani hiyo, na Marta alihusishwa na vikundi vya Opus Dei hadi siku yenyewe ya kifo chake, kwa vile alipoondoka kutoka kwenye Klabu ya Arlanza huko Burgos, na baada ya kuagana na Bwana katika kanisa dogo la kuabudu, alianza safari yake kuelekea nyumbani kwake, ambapo hangewahi kufika.
Katika utafutaji huu wa kina wa Mungu alipata maang’amuzi ya nguvu sana wakati wa hija ya Taizé. Lakini ilikuwa muda mfupi baadaye, ndani ya Njia ya Neokatekumenato ambamo msichana huyu alipata jibu kwa kupata “maana ya kweli ya maisha.”. Wakati fulani, padre mmoja aliyemfundisha chuoni alimwendea Marta na kumuuliza kuhusu mipango yake kwa wakati ujao kama mwandishi wa habari, kitu ambacho alikuwa akikitamani sana hapo awali. Lakini jibu lake liliacha muhuri katika padre huyo: “Leo kama leo, kichwani pangu yupo Mungu tu.”

Bikira Maria kama mfano
Zaidi ya hayo, miezi michache kabla ya kifo chake, akiitikia wito katika jumuiya yake huko Burgos, alijitolea kabisa kwa Mungu kama mmisionari “msafiri,” yaani, kama mwinjilishaji mlei aliye tayari kutangaza Injili popote duniani.
“Ninahitaji kukufuata wewe, Bwana; Ninapoenda mbali na wewe, ninaonja kifo.”
Kwa kufuata mfano wa Bikira Maria, neno “Litendeke” likawa neno alilolipenda Marta zaidi. Daima alikuwa nalo mdomoni. Jitihada zake wakati wake wa mwisho, kama inavyoonyeshwa katika maandishi na maelezo aliyokuwa akiandika, zilikuwa kutimiza mapenzi ya Mungu nyakati zote na kutoa yote kwa Mpenzi wake, kwa Kristo, kwa yule ambaye alikuwa amempatia maisha yake maana. Hivyo, aliandika hivi mwishoni mwa 1990: “Mkristo ni mtu mwenye furaha na anayepanda furaha, kupitia amani ya ndani anayobeba daima na uwepo wa Mungu katika maisha yake. Ombi langu kuu katika kuishi pamoja hii ni: upambanuzi na amani. Uniongezee imani, nahitaji kukufuata wewe, Bwana; Ninapoenda mbali na wewe, ninaonja kifo.”
Akishikwa na upendo kwa Ekaristi
Muungano huo wa ndani ulidhihirishwa kupitia uwepo halisi wa Kristo, na hicho kilimfanya Marta aandike baadhi ya tafakari zake fupi zilizoonyesha jinsi roho yake ilivyokuwa ikifurika: “Bila sala na bila Ekaristi hakuna mtakatifu awezaye kuvumilia.” Na mahali pengine amendika: “Uhai wa nafsi zetu na afya ya kifo chetu ndiyo Ekaristi.”
Shahidi mmoja wa usiku wake wa mwisho alisimulia kwamba, kabla ya kwenda nyumbani, Marta alilisogelea kanisa dogo la taasisi alipokuwa akisoma ili kumuaga Bwana, akapiga goti mbele ya Sakramenti Takatifu na akaondoka, akiacha vitabu na maandishi yake pale ili kurejea kesho yake baada ya kusali Misa na kukomunika katika kanisa la karibu.
Miaka 32 imepita tangu kifo chake na maisha yake yanaendelea kuwa mfano, hasa kwa walio vijana zaidi. Alikuwa na furaha na akili, na alijua jinsi ya kujiburudisha bila kutumia dhambi, lakini Marta Obregón ndiye kielelezo ambacho vijana wa leo wanaweza kutazama ili kugundua uzuri wa usafi na thamani halisi ya mwili.
“Laiti ningeweza kutoa mfano …!”
Carlos Metola anaeleza kwamba kuna neema na fadhila nyingi zinazosababishwa na maombezi yake, na ingawa kuna watu wengi wa kila aina ambao wamemgeukia, idadi kubwa ya vijana inatia alama. Kumekuwa na wasichana ambao wamepata wito wao kwa maisha ya kitawa kutokana na ushuhuda wake, watu wengi kuponywa na magonjwa kwa namna zisizoelezeka na pia misaada mbalimbali katika hali mbaya za familia. “Ninaona kwamba Mungu ‘anadai’ zaidi na zaidi kutoka kwangu, na hata katika hilo ninajihisi kuwa na upendeleo. “Laiti ningeweza kutoa mfano na maisha yangu…” aliandika Marta, bila kujua hapo kwamba ushuhuda wake ungekuwa zawadi kwa Kanisa zima, na kwamba mfano wake unahitajika zaidi leo kuliko wakati alipogeuka kuwa shahidi kwa ajili ya usafi wa mwili.