
Mateso ya wasio na hatia na Masiya, 19 Oktoba 2025
Orkestra na Kwaya ya Kisimfonia ya Njia ya Neokatekumenato ilitumbuiza huko Cordoba (Hispania), katika mazingira ya kuvutia ya Kathedrali yake, inayotambulika kwa muundo wake kama Msikiti, mbele ya kanisa lililojaa waamini na makasisi kadhaa. Miongoni mwao, waliohudhuria ni Askofu wao Mkuu, Monsinyori Jesús Fernández, pamoja na Askofu Mstaafu wa jimbo hilohilo, Monsinyori Demetrio Fernandez, na Askofu Mstaafu wa Jimbo la Callao (Peru), Monsinyori José Luis del Palacio.
Walipiga kwa mara ya kwanza nchini Hispania kazi kamili za kisimfonia za Kiko Argüello: simfonía iitwayo “Mateso ya Wasio na Hatia” na shairi la kisimfonia “Masiya”. Kabla ya kila wimbo, mtunzi, Kiko Argüello, alitoa maelezo juu yake. Alisisitiza katika maneno yake kwamba tamasha hili pia ni muhula wa sala kwa ajili ya wale wasio na hatia; Mhashamu Jesús, Askofu wa Cordoba, aliteuliwa kuongoza sala hiyo kabla ya muziki kuanza.

Tukio hili lilifanyika katika sadfa maalum, yaani, kumbukumbu ya miaka 1100 ya kifodini cha Mtakatifu Pelagius, au Pelagio, kama anavyojulikana katika jiji la Cordoba.
Takriban washiriki 5,000 wa Njia ya Neokatekumenato kutoka mkoa mzima wa Andalusia walihudhuria, wapatao 2,500 ndani ya Kanisa na wengine wengi ambao waliweza kushuhudia tukio hilo kupitia skrini kubwa zilizoandaliwa na mapadre katika Uwanda wa Michungwa. Maelfu zaidi walikuwa waliofanya hivyo kupitia utangazaji wa kidijatli kwa njia ya chaneli ya YouTube ya Kathedrali hiyo yenyewe.
@mezquita-catedraldecordoba
Orkestra na Kwaya ya Kisimfonia ya Njia ya Neokatekumenato, iliyoanzishwa na Kiko Argüello mwaka 2010 na inayojumuisha zaidi ya wanamuziki 200 kutoka mataifa mbalimbali, ilishirikisha katika tukio hili waimbaji 160, wakiwemo wapiga ala na wanakwaya, wakatumbuiza kwa ustadi na uchangamfu, wakisababisha misisimko na kustaajabishwa katika nyakati mbalimbali. Orkestra iliongozwa kwa ustadi na Tomáš Hanus, mmoja wa waongozaji bora kwenye eneo la muziki kwa sasa, akiwa ameongoza baadhi ya orkestra zenye fahari zaidi duniani, naye kwa sasa ni pia mwongozaji mkuu mwalikwa wa Orkestra ya Kisimfonia ya Iceland. Aidha, Hanus ni baba wa watoto wanane na mshiriki katika Njia ya Neokatekumenato.
Tangu 2010, orkestra hii imeimba kwenye kumbi maarufu kutoka popote ulimwenguni. Baada ya tamasha lake la kwanza katika Ukumbi wa Paulo VI (pia uitwao “Sala Nervi”) mbele ya Papa Benedikto XVI, Orkestra na Kwaya ya Njia ya Neokatekumenato imefanya matamasha huko Jerusalem, Paris, Madrid, New York, Boston, Krakow, Tokyo, Budapest, na Berlin, zikiwa tu baadhi ya sehemu chache muhimu zaidi. Tamasha la 2013 katika kambi za Auschwitz, katika kumbukumbu ya wahanga wa itikadi ya Unazi (Hitler), ulikuwa kwa namna ya pekee wa kusisimua na wenye hisia nyingi. Matamsha yaliyofuata yalifanyika Trieste, Roma, na Cordoba; Oviedo hivi karibuni atajiunga na orodha ya miji ambayo imekuwa na furaha ya kusikia nyimbo hizi za kisimfonia zilizoundwa kwa roho ya muziki Mtakatifu wa kale.



Katika nyimbo hizi, lengo si kupata hisia nzuri kwa ajili yake yenyewe au ukuu wa kisanii. Mtunzi wao, kama vile anavyotumia michoro yake, anageuza muziki kuwa chombo cha uzuri wa kipekee ili kufikisha Habari Njema ya Injili kwa mtu wa kisasa, asiye na dini, kwa lugha ambayo anaweza kuelewa na ambayo, kwa kutumia maneno sahihi zaidi, husisimua na hulewesha kuanzia mpigo wa kwanza.
Wanamuziki wanafanikiwa kwa ustadi wasikilizaji washiriki katika sala hiyo yenye kupasua mioyo na yenye nguvu inayobubujika kwa kila noti. Ni orkestra inayosali na kutualika kumsindikiza Kristo na Mama yake Mbarikiwa katika saa hizi za mwisho za huzuni yaje yenye baraka na ukombozi, ikituburuza kwake kupitia uzuri wake na fumbo lake la ajabu; inatualika kujiruhusu kuoshwa na kutakaswa kwa sadaka yake. Na wakati hisia na huzuni zinapoonekana kututeketeza, sehemu ya mwisho ya “Simfonia ya wasio na hatia”, iitwayo Resurrexit (“Amefufuka”), inagueza machozi hayo matamu kuwa mkondo wa uzima unaounganisha maumivu pamoja na furaha ya ufufuko, mkondo ambao unatiririka milele kutoka ubavu wa Kristo. Ameshinda mauti; yu hai na amefufuka kwa sababu yetu na kwa ajili yetu.
Baada ya Simfonia ya Wasio na Hatia wimbo mwingine ulifuata, shairi la kisimfonia lenye kinanda, kwaya, na orkestra , ambalo linaitwa “Masiya”. Shairi hilo ni jibu mbele ya kikwazo cha mateso, na ambalo mtunzi wake, Kiko Argüello, alipenda kuwatolea wafiadini wote ambao leo wanadhihirisha duniani sura ya Kristo, Mwana-Kondoo aliyechinjwa, anayetoa maisha yake kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. Naye Kiko anafanikiwa kufanya hivyo katika vipande vitatu: cha kwanza kuhusu sadaka ya Isaka, cha pili kinatuonyesha Kristo kwenye Njia ya Msalaba na Mateso akielekea Kalvari, na cha tatu kinatafakari ukuu wa Mungu anayeokoa kwa kutoa damu yake.

Kwa hiyo, katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 1100 ya Mtakatifu Pelagio, na kwa heshima yake na ya wafiadini watakatifu wengi sana ambao, wakiwa waliweza kuchagua njia nyingine za kibinadamu zinazovutia zaidi na zenye nguvu zaidi, waliamua kuungana na sadaka ya ukombozi ya Kristo. Wao wanatukumbusha kwamba hii ilikuwa njia iliyochaguliwa na Mungu ili kuokoa dunia: kwamba damu ya wafiadini, kma vile mateso yetu yote yakiungana na yale ya Kristo, ndiyo mbegu ya Uzima wa Milele inayorutubisha na kurembsha kila kizazi, ikidhihirisha mateso na ufufuo wa Bwana Wetu Yesu Kristo.
Kwa sababu hizi zote, mtunzi wa wimbo huu na mwanzilishi wa Njia ya Neokatekumenato, Kiko Argüello, alitaka kwamba katika jiji hili la Cordoba, ambalo fahari yake ya kale inaonekana katika Kathedrali yake Takatifu, noti hizi zipate kusikika, ambazo zinadokeza sio tu Mateso ya Kristo, bali pia yale ya mashahidi wake wasio na idadi kwenye ukingo wa mto Guadalquivir, mto ambao umerudisha kwenye kingo zake miili na kunywa damu ya mamia ya mashahidi: kwanza kutoka wale wa kipindi cha maudhia ya Decius na Diocletian, kisha mashahidi wasiohesabika wa Mozarabic, na hivi karibuni zaidi maudhia ya kikatili yaliyotukia kwenye miaka ya 1936-1939.
Yote hayo kwa heshima yake na kwa utukufu mkubwa wa Mwenyezi.


