Kama hitimisho la Jubilei ya Vijana, iliyotakwa na Baba Mtakatifu Fransisko na kuadhimishwa na Baba Mtakatifu Leo XIV, ili kurejesha matumaini kwa dunia ya leo, vijana 120,000 kutoka jumuiya za Njia ya Neokatekumenato kutoka nchi 109 katika mabara matano wamekusanyika alasiri ya leo, tarehe 4 Agosti 2025, mahali pale pale pa mkutano na Papa, pamoja na Kikundi cha Kimataifa cha Kiko Argüello, María Ascensión na Padre Mario.
Katika jukwaa kuu, ambapo Papa aliongoza Mkesha wa Sala, walikuwepo Makardinali 6, Maaskofu wakuu 4 na Maaskofu 26, pamoja na mamia ya makatekista wasafiri na makatekista wengine ambao waliwasindikiza vijana hawa wote hadi Roma, katika hija ya sala, lakini pia ikawa hija ya kutangaza Injili katika miji kadhaa ya Ulaya, ambako wamelala usiku wakati wa safari zao ndefu, wakihusisha jumuiya mahalia za kila eneo, jumuiya zao wenyewe na serikali za mitaa, zilizowaandalia ukaribisho mkubwa wenye ishara nyingi.
Hivyo, Hija imekuwa ni fursa ya kushuhudia uzuri wa imani yao, furaha ya siku walizokaa pamoja, na sherehe ya kusafiri kwenda Roma kukutana na Papa na kuweka misingi ya njia yao ya imani juu ya Petro.

Mkutano huo uliongozwa na Kardinali Baldassare Reina, Naibu wa Papa kwa ajili ya Jimbo la Roma, ambaye alisalimiana na mkutano huo mkubwa.
Katika roho ya sherehe na ushirika wa kweli, kati ya bendera zinazopeperushwa za nchi takriban 50 za Ulaya, 30 za Amerika, 11 za Afrika (na nyinginezo ambazo zilishindwa kuhudhuria kwa sababu ya kutoweza kupata viza kwa ajili ya mkutano), na nchi 20 kutoka Mashariki ya Kati, Asia, na Oceania, umeweza kusikika uzuri kamili wa siku hizi, wa Jubilei hii ya Matumaini. Na vijana hawa (pamoja na mamia ya maelfu ya wengine waliokusanyika katika jiji hili la milele la Roma, mahali walipouawa mitume Petro na Paulo na maelfu ya wafiadini wengine) wanaweza kugeuka kuwa mashahidi halisi wa uzuri wa imani ya kikristo katika jamii inayozidi kuduniaishwa na kutojali.
Mkutano huo uliendeshwa kwa kufuata utaratibu wa kawaida wa Mikutano ya Miito ya Siku nyingine za Vijana Duniani: Kiko, akisindikizwa na Padre Mario Pezzi na Maria Ascension, alitambulisha kusanyiko kwa ufupi kabla ya kuanzisha wimbo uliochukuliwa kutoka katika kitabu cha nabii Isaya, ambao huwa unazindua na kutia muhuri katika mikutano hii: “Nakuja kukusanya mataifa yote”, na ambao kusanyiko hilo ni picha yake hai.
Kufuatia salamu za Kadinali Reina, akisindikizwa na mapadre 100 kutoka seminari mbalimbali za Redemptoris Mater, picha ya Bikira Maria iliingia jukwaani ili kuongoza mkutano, sambamba na msalaba mkubwa. Aidha iliwekwa picha ya Carmen Hernández, Mtumishi wa Mungu aliyemsindikiza Kiko kufungua Njia ya Neokatekumenato ndani ya Kanisa kama uingizwaji wa kikristo, ambayo sasa ipo katika nchi 138 ulimwenguni kote.
Baada ya maneno machache kutoka Acensión, aliyewaelezwa vijana maisha ya Mtakatifu wa Ars, Mt. Yohane Maria Vianney, ambaye sikukuu yake Kanisa liliadhimisha siku hiyo, Neno la Mungu likatangazwa, likichukuliwa kutoka Waraka wa Pili wa Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho, neno hasa lenye nguvu kubwa linalotualika “msiipokee neema ya Mungu bure”. Kisha, Injili ya siku hiyo iliimbwa: Mathayo 9:35-10:1: kifungu kilichofaa kwelikweli kwa mazingira hayo, chenye maneno ya Bwana yaliyofaa zaidi kwa mkutano huo wa miito: “Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake”.
Kiko amefanya kuvuma kwa nguvu tangazo la habari njema, ambayo ni mpya daima, kwa sababu inaleta hapa na sasa neno la Mungu “NIPO”: upendo wake, kifo na ufufuko wa Mwanae Yesu Kristo, anayeshinda dhambi ya mwanadamu, ili kumpeleka katika utimilifu wa uzima ambao ndiyo mbinguni: “Ni ipi hamu ya ndani zaidi ya Mungu?” Kiko aliuliza. Akajibu: “Kukupatia zawadi ya Roho Mtakatifu, ya maisha yake, ya furaha yake.”
“Lakini ili kukupa zawadi hiyo, Mungu anahitaji uhuru wako, kwa sababu kama anavyotukumbusha Mtakatifu Augustino: ‘Mungu, aliyekuumba bila wewe, hatakuokoa bila wewe’.”.

Kiko, kwa kusoma upya tangazo la kitabu cha Mwanzo, ameonyesha kwamba nyuma ya udanganyifu wa nyoka, mwanadamu aliyepokea katekisi ya shetani kwa kutomtii Mungu, kwa kumkataa, anajikuta amepotea, amekufa: si shida ya kimaadili, bali ya kiutu: ikiwa Mungu hayupo, ikiwa hakuna Muumba, mimi ni nani? Nini maana ya maisha yangu?
Kwa kujikuta bila jibu la kweli la kiutu, mwanadamu anapotoka katika kutafuta chochote kitakachoweza kumpa jibu: anjitolea mwenyewe mambo yote, bali akijikuta kwamba anazidi kuwa mpweke, bila uwezo wa kupenda.
Na mwanadamu anakuwa hivyo mtumwa wa upweke, wa kuogopa kifo. Mwanadamu sasa anaishi ulimwenguni kupitia mtazamo wake mwenyewe, katika ulimwengu ambao mhimili wake, kiini chake, si Mungu tena, bali yeye mwenyewe: ubinafsi wake. Hiyo ndiyo dhambi. Si suala la kimaadili, bali la kiutu. Dhambi hii, inayokaa ndani kabisa ya utu wangu, inanilazimisha kwanza kujitolea kila kitu kwangu mwenyewe, kwa sababu mimi ndimi mungu wangu mwenyewe na ninataka kuwa na furaha; ninajitolea kila kitu.
Hiki ndicho kinachomzuia Mungu akupe Roho wake Mtakatifu, Kiko aliendelea kusema: dhambi inayokaa ndani yako. Na hii ndiyo maana ya mkutano wetu alasiri ya leo, ya Jubilei hii: Yesu Kristo anataka kujitoa kwako. Mtakatifu Paulo asema hivi: “Upendo wa Kristo unatuhimiza kufikiri, kwamba ikiwa Kristo alikufa kwa ajili ya wote, hivyo wote walikufa. Naye alikufa kwa ajili ya wote, ili wale wanaoishi wasiishi tena kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili ya Kristo”.
Kiko, akinyosha kidole kwa msalaba wa Kristo, alisema: “Ninawaalika kutazama msalaba huu: Hii ndiyo picha ya uhuru. Msalaba ndiyo picha ya uhuru. Hapa kuna mtu ambaye amejitoa kwa ajili yako, ambaye atakuweka huru ili ujitoe kwa wengine na ili uache kujitolea kila kitu wewe mwenyewe. Unawezaje kumpokea Roho Mtakatifu leo? Ikiwa unakubali kwamba utu wako usulibiwe na Kristo.”

Na aliendelea kueleza mazungumzo kati ya Yesu na Petro baada ya kufufuka kwake. Petro alikuwa amemsaliti, lakini Yesu hakumtelekeza; akamtafuta, akamwuliza, “Petro, unanipenda?”. Na, akiwaelekea vijana, Kiko alisema kwamba Bwana anatuuliza kila mmoja wetu swali hilo hilo jioni hii: “Je, unanipenda?” Tukiwa na jibu upande wetu, Yeye anaweza kutupatia kipaji cha Roho Mtakatifu: anaweza kutufanya watakatifu.
Huu ndio mpito wa Mungu kati yetu, wito wake. Hija, Jubilei, inasimama mbele ya hii: “MIMI HAPA, NIPO” ya Mungu. “MIMI HAPA” hii inangoja “MIMI HAPA” ya kwako leo, kama Bikira Maria.
Ili kuweka muhuri juu ya ukweli wa mkutano huu, wa kile kilichokuwa kinaadhimishwa, baada ya maneno machache kutoka kwa Padre Mario, ambaye alikumbusha wito wake na kuwaalika vijana wasiogope kuitikia kwa Yesu Kristo, Kiko akaanzisha kuitisha miito kwa mkutano huo.
Ilishangaza kuona jinsi vijana wengi hivi walivyokuwa wakingojea wito huo, kwa sababu mara tu Kiko alipomaliza kuongea, wengi wao walianza kuelekea jukwaani, wakitengeneza mto halisi wa watu: kutoka vikundi vyote, kutoka nchi zote, wakizungumza lugha zote, wakiwa wamevaa mitindo ya aina zote, wakiwa njiani kuitikia wito wa Bwana.
Kwanza wavulana—5,000 kati yao walisimama!—kisha wasichana—5,000 kati yao walisimama!— wakaenda jukwaani kupokea baraka za makardinali na maaskofu. Wito huu wa kwanza baadaye utathibitishwa na kukomazwa katika vituo mbalimbali vya miito, lakini kuitikia wito wa Bwana leo kunaweza kuanzisha mabadiliko ya maisha ambayo, kama Kiko alivyosema, yanaendana na mpango wa Mungu: kukufanya mtakatifu!
Kardinali Reina alihitimisha mkutano huo kwa maneno ya matumaini. Tunaleta hapa baadhi yake: “Baada ya kupokea Kerygma, tamanini yaliyo makubwa zaidi, utakatifu”; “Na hili liwe jibu la wito wa Papa Leo”; “Bwana ametoa mwaliko huu kwetu; Bwana anatuita sisi sote kwa utakatifu”; “Siku zote achieni nafasi kwa Neno la Mungu, kwa sababu Mungu haondoi chochote kutoka furaha yetu”; “Kwa baadhi yenu leo njia ya furaha inafunguliwa, kuelekea maisha yaliyojaa, yaliyojaa Mungu, yaliyojaa heri.”

