Leo tarehe 27 Juni 2022, wakati wa kuhitimisha Mkutano wa Kumi wa Familia Duniani, Baba Mtakatifu Fransisko, aliyekaribishwa kwa furaha katika Ukumbi wa Paulo wa Sita kwa wimbo wa Bikira Maria, alituma Familia 430 za Njia ya Neokatekumenato, pamoja na watoto wao, hadi sehemu zilizopoteza zaidi Ukristo wao ulimwenguni ili kuonyesha kwa maisha yao ushuhuda wa upendo wa Mungu kwa walio mbali zaidi.

Pamoja na Familia hizi, walikuwepo Kikundi cha Wawajibikaji wa Kimataifa wa Njia, Kiko Argüello, Padre Mario Pezzi na Ascensión Romero, vikundi vya makatekista wasafiri, wanaowajibika na Njia katika Nchi 134 za Dunia na maelfu kadhaa ya ndugu kutoka jumuiya za Neokatekumenato kutoka Roma na mkoa wa Lazio, pamoja na mapresbiteri wengi na waseminari. Waseminari wa Seminari ya Redemptoris Mater ya Macau, seminari iliyotamaniwa na Baba Mtakatifu Fransisko kwa ajili ya uinjilishaji Asia, na ambao baada ya siku chache wataenda China, walishiriki pia katika mkutano huo.

Kiko kabla ya kuzitambulisha familia hizo, alimshukuru Baba Mtakatifu kwa kukubali kuwatuma katika utume: ni mara ya kumi na tisa (19) ambapo Mapapa wametuma Familia za Njia katika mabara matano; Kiko pia alishukuru Kard. Kevin Farrell, Mkuu wa Idara ya Walei, Familia na Uhai, ambaye ametaka kuwepo pamoja na timu kutoka Idara yake, na maaskofu kadhaa ambao wametaka kusindikiza tukio hili.

Alihitimisha mwingilio wake mfupi kwa kukumbusha kwamba Njia ya Neokatekumenato ni tunda la Mtaguso wa Pili wa Vatikano, alivyotambua toka mwanzo Papa Mtakatifu Paulo wa Sita. Safari hii ya uingizwaji wa kikristo inaongoza watu kwa imani ya watu wapevu, kupitia kugundua upya utajiri wa ubatizo wetu. Kadhalika, amekumbuka kwa shukrani maneno ya Baba Mtakatifu Francisko katika mkutano wa mwisho uliofanyika Tor Vergata, tarehe 4 Mei 2018, wakati wa kuadhimisha miaka 50 ya Njia: “Ninyi ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa” ; Kiko alimalizia kwa kusema: “Hakika ni ajabu kwamba Bwana ameinua familia nzima, pamoja na watoto wao, ili kuhama na kupandikizwa katika maeneo yasiyo ya kidini na yaliyo maskini zaidi na hivyo kubeba tangazo la Yesu Kristo kupitia ushuhuda wa maisha yao wenyewe”.

Kisha kwa ufupi alitambulisha kwa Baba Mtakatifu familia zilizo katika utume zilizotumwa katika nchi mbalimbali za Ulaya, akianza na zile za Ukrainia na Urusi, na pia huko Latvia, Lithuania, Estonia, Romania, Bulgaria, na nchi nyingine 14 za Bara la Ulaya; ametambulisha pia familia zilizopo Asia: Kazakhstan, Mongolia, Japani, Korea Kusini, Taiwan, Kambodia, Laos; katika Amerika: Kanada, Marekani, Mexico, Puerto Rico, Jamaica, Ekuador (Amazon), Argentina; barani Afrika: Misri, Tunisia, Ethiopia, Sudan, Kenya, Kamerun, Uganda, Gabon, Guinea ya Ikweta, Cabo Verde, Côte d’Ivoire na Afrika Kusini. Amehitimisha na familia zinazofanya kazi Australia na Oceania.

Baada ya kutambulishwa, kiliimbwa kifungu cha Injili cha kutumwa kwa Mitume na Yesu, Mt 28: 16-20, na Baba Mtakatifu akatoa salamu zake na neno lake la kusindikiza, neno ambalo litategemeza Familia hizi katika magumu na furaha sawia za utume.

“Tumesikiliza utume wa Yesu – alisema Papa – “Nendeni, toeni shuhuda, hubirini Injili”. Na tangu siku ile mitume, wanafunzi, watu wote walisonga mbele kwa nguvu zile zile walizopewa na Yesu; ni nguvu zitokazo kwa Roho”. “Nendeni mkahubiri… Mkabatize…”.

Baada ya Ubatizo kupokelewa, jumuiya lazima ikue, inahitaji kusaidiwa kukua, pamoja na namna zake, na utamaduni wake. “Na kazi hii, utajiri huu wa tamaduni wa Injili, unaozaliwa kutokana na mahubiri ya Yesu na kugeuka kuwa utamaduni, ni kidogo historia ya Kanisa: tamaduni nyingi lakini Injili hiyo hiyo. Mataifa mengi sana, Yesu Kristo yule yule”… “Mhubirini Yesu Kristo kwa nguvu za Roho katika Kanisa na pamoja na Kanisa”… “Roho hii ya umisionari, yaani, kujiachia kutumwa, ni msukumo kwenu nyote. Ninawashukuru kwa jambo hili, na ninawaomba usikivu kwa Roho anayewatuma, usikivu na utii kwa Yesu Kristo katika Kanisa lake.

Na Baba Mtakatifu alihitimisha hotuba yake fupi kwa kuzishukuru Familia zilizohudhuria, kwa mwaliko dhahiri: “Endeleeni! Jipeni moyo! Asanteni kwa ukarimu wenu. Msisahau mtazamo wa Yesu, ambaye amewatuma kila mmoja wenu kuhubiri na kulitii Kanisa. Asanteni sana!”.

Kisha Baba Mtakatifu akaibariki misalaba ambayo Familia zitabeba, kama ishara ya uwepo wa Bwana, aliyekufa na kufufuka kwa ajili yao, na alisalimia baadhi ya familia, pamoja na watoto wao, kama wawakilishi wa familia zote.

Familia 430 za leo, ambazo zinafanya idadi ya familia za Njia kwenye utume kufikia zaidi ya 2,000, ni za makundi mawili: familia 157 ni mpya, wakati zingine 273 ni familia ambazo tayari zilikuwa zimeondoka kwa ajili ya utume katika miaka ya hivi karibuni, lakini ambazo, kwa sababu ya covid 19, Papa alikuwa bado hajawatuma.

Katika kujiandaa kutuma Familia hizi 430, Kikundi cha Kimataifa, pamoja na Vikundi vya Wasafiri walifanya mkutano wa wiki moja nao huko Porto San Giorgio (Fermo) ambapo walisikilizwa na kisha kuchaguliwa kwa bahati nasibu kwa utume mbalimbali zilizoombwa na Maaskofu.

Mang’amuzi haya ya uinjilishaji ya Njia ya Neokatekumenato yalianza mwaka 1986 na tangu wakati huo Mapapa Yohane Paulo II, Benedikto XVI na Papa Fransisko wamerudia kutuma huku kwa Bara 5 kwa mara 19. Zaidi ya Familia 2,000 zimesambazwa kama ifuatavyo:

  • Familia 960 zinainjilisha katika missio ad gentes 200, pamoja na mpresbiteri na baadhi ya madada.
  • Familia 800 ziko katika mataifa tofauti ili kuimarisha jumuiya mahalia, wakitegemeza Njia yao ya imani.
  • Zaidi ya 300 ni familia zinazounda, pamoja na mpresbiteri na kijana mwingine, kikundi cha uinjilishaji, kinachowajibika kwa taifa au maeneo fulani.
Share: