Carmen Hernández
Novemba 24, 1930, † Madrid, Julai 19, 2016
Carmen alikuwa, pamoja na Kiko, mwanzilishi wa Njia. Alizaliwa huko Ólvega (Soria, Hispania) mnamo Novemba 24, 1930. Alikuwa mtoto wa tano kati ya ndugu tisa – wanaume wanne na wanawake watano- na aliishi utoto wake huko Tudela (Navarra, Hispania).
Huko Tudela alisoma katika Shirika la Maria na alikuwa na mawasiliano na Shirika la Yesu (Wajesuiti). Akivutiwa na roho ya kimisionari ya Mtakatifu Fransisko Ksaveri, tangu alipokuwa kijana sana alisikia wito wa kwenda utume huko India. Kwa utashi wa baba yake, mnamo 1948 alianza kusoma Kemia huko Madrid, ambapo alihitimu na alama za juu kabisa mnamo 1954.
Kwa muda alifanya kazi na baba yake katika kiwanda cha chakula familia ilikuwa nacho huko Andújar (Jaén), lakini anaamua kukiacha na kuhamia Javier, anamoingia kwenye taasisi mpya ya kimisionari: Wamisionari wa Kristo Yesu. Baada ya novisiati, alisoma Teolojia katika nyumba ya malezi ya kiteolojia kwa watawa huko Valencia. Mnamo 1960 alipangiwa kwenda India. Kwa utume huu ilimbidi kujiandaa huko London (wakati huo India ilikuwa ndani ya Jumuiya ya Madola), ambapo alikaa kwa mwaka mmoja. Wakati huo, kulikuwa na badiliko la mwelekeo katika Wamisionari wa Kristo Yesu ambalo lilipunguza uwazi wao mbele ya utume, hivyo Carmen alirejea kutoka London hadi Barcelona. Huko anakutana na padre Pedro Farnés Scherer aliyekuwa amemaliza masomo yake katika Taasisi ya Liturjia ya Paris, muda mfupi kabla ya Mtaguso wa Vatikano II alimoshiriki kwa ustadi katika Consilium, tume kwa ajili ya utekelezaji wake.
Katika masomo yake, P. Farnés aliwasilisha vyanzo vya kipasaka vya Ekaristi, pamoja na eklesiolojia iliyofanywa upya, iliyoonyesha Kanisa kama mwanga wa mataifa. Mawasiliano hai ya Carmen pamoja na waandishi wa upyaisho huu wa Mtaguso ukawa na ufwatiliaji mkubwa, baadaye, katika uundaji wa katekesi za Njia ya Neokatekumenato.
Kuanzia katikati ya 1963 hadi katikati ya 1964, Carmen alizuru Nchi Takatifu akibeba Biblia, akifahamu Maeneo Matakatifu . Aliporejea Madrid, alianza kufanya kazi katika vibanda vilivyokuwa nje ya mji, akifikiria kwenda kama mmisionari hadi Bolivia pamoja na walei wengine. Hata hivyo, huko alikutana na Kiko Argüello, aliyeishi katika vibanda vya Palomeras Altas, na akaamua kukaa katika eneo hilo hilo. Katikati ya maskini, wote wawili waligundua uwezo wa Fumbo la Pasaka na wa mahubiri ya Kerigma (Habari Njema ya Kristo aliyekufa na kufufuka) na waliona jumuiya ya kwanza kuzaliwa. Kupitia kwa uthibitisho wa mkondo huu mpya na Askofu Mkuu wa Madrid wakati huo, Mons. Casimiro Morcillo, Carmen alishirikiana na Kiko akipeleka katika parokia -kwanza Madrid, kisha Roma na kutoka hapo hadi miji na mataifa mengine- kazi hii ya upyaisho wa Kanisa.
Carmen Hernández alifariki mnamo Julai 19, 2016 huko Madrid. Katika mazishi yake, yaliyoongozwa na Kardinali Askofu Mkuu wa Madrid Carlos Osoro Sierra, na kuhudhuriwa na maelfu ya watu, P. Mario Pezzi alisisitiza kuwa katika Njia “ni mara ya kwanza katika historia ambapo mkondo wa kikanisa umeanzishwa na mwanamume na mwanamke ambao wamekuwa wakishirikiana sikuzote pamoja zaidi ya miaka 50.” Zaidi ya hayo, Papa alituma ujumbe ambapo alihakikisha kupokea “kwa hisia” habari za kifo cha Carmen na alisisitiza juu yake ” maisha marefu yaliyotiwa alama na upendo wake kwa Yesu na shauku kubwa ya kimisionari”. “Namshukuru Bwana kwa ushuhuda wa mwanamke huyu, aliyehuishwa na upendo wa dhati kwa Kanisa, ambaye ametumia maisha yake katika tangazo la Habari Njema katika kila mahali, pia pale palipo mbali zaidi, bila kuwasahau waliotengwa zaidi”, aliandika Papa Fransisko.