Njia ya Neokatekumenato Yohane Paulo wa Pili na Carmen Hernández - ziara katika parokia ya Kuzaliwa kwa Yesu - Roma 1980

Maoni ya Kiko Argüello

Jioni njema kwenu nyote,

Namsalimu Mha. Carlos Osoro, Kardinali-Askofu Mkuu wa Madrid.

Mwadhama Kardinali Antonio Maria Rouco, Askofu Mkuu Mstaafu wa Madrid.

Kardinali Paolo Romeo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Palermo.

Maaskofu wakuu, maaskofu na maaskofu wasaidizi waliopo hapa.

Njia ya Neokatekumenato ufunguzi wa mchakato wa kutangazwa kuwa mwenye heri na mtakatifu wa Carmen Hernández 4-Des-2022
Chanzo: archimadrid.es – Luis Millán

Mama Mkuu wa Wamisionari wa Kristo Yesu na washauri wake. Ni furaha gani unayotupatia uwepo wenu katika hafla hii, madada!

Mkuu wa Chuo, Pd. Daniel Sada, Wakuu wa Vitivo na maprofesa.

Jumuiya za neokatekumenato zilizopokea katekesi kutoka kwa Carmen na mimi huko Madrid, Zamora, Barcelona, Roma, Florence, Ivrea na Paris.

Makatekista wasafiri, magombera na walezi wa seminari za Redemptoris Mater, mapadre, na ninyi nyote mliopo hapa. Natuma salamu za upendo kwa ndugu wengi hivi wa Njia ambao wanafuatilia tukio hili kupitia mtandao.

Tunashukuru kwa barua nyingi hivi tulizopokea kutoka maaskofu wakuu na maaskofu kutoka mabara yote matano, ambao, kwa kutoweza kuhudhuria tukio hili, wanashiriki furaha yao na ndugu wa Njia na kujiunga nasi kwa sala zao.

Ningependa kusoma maneno machache kutoka kwa Kardinali Farrell, Mkuu wa Idara ya Walei, Familia na Uhai, ambaye pia ametuandikia barua:

Wapendwa Kiko, Pd. Mario na María Ascensión,

Ninawashukuru kwa mwaliko mlionitumia ili kushiriki katika Tukio rasmi la Ufunguzi wa Mchakato wa Kutangazwa kuwa Mwenye Heri na Mtakatifu kwa Carmen Hernández, ambalo litafanyika, Mungu akijalia, katika Chuo Kikuu cha Fransisko wa Vitoria huko Madrid.

Ninafurahi kujua kwamba ombi la Kufunguliwa kwa Mchakato wa Carmen Kutangazwa kuwa Mtakatifu limekubaliwa na ninajiunga na furaha yenu na shukrani zenu kwa Bwana. Kwa masikitiko, majukumu ambayo tayari yamewekwa katika ratiba ya kipindi hicho yananizuia kuwa nanyi siku hiyo huko Madrid.

Kwa vyovyote vile, ninawahakikishia kuwakumbuka mbele za Bwana ili maisha ya Carmen, ushuhuda wake wa imani, kutumika kwake hadi mwisho kwa kupeleka mahali pote tangazo la Injili, viendelee kuwa kielelezo kwenu nyote na kwa Kanisa zima.

Nikirudia shukrani zangu na nikitumaini kwamba zitakuwepo nafasi nyingine za kukutana, ninawasalimu kwa moyo mkunjufu katika Bwana.

Kardinali Kevin Farrell. Mkuu wa Idara ya Walei, Familia na Uhai.

Mimi binafsi nimefurahi sana kwamba siku hii imewadia ambapo Kanisa linaanza awamu ya kijimbo ya Mchakato wa Kutangazwa Mwenye Heri na Mtakatifu kwa Carmen Hernández. Namshukuru Mwadhama Kardinali, Askofu Mkuu wa Madrid, Carlos Osoro, kwa kuanzisha uchunguzi juu ya maisha, fadhila na umaarufu wa utakatifu wa Carmen.

Bwana ametuunganisha, mimi na Carmen, kwa miaka 52, katika utume wa ajabu wa uinjilishaji -ulioanza katika jimbo hili la Madrid-, kama tunda la Mtaguso.

Ninalihisi kama tukio la upaji wa Mungu, kwamba ufunguzi wa Mchakato umeingiliana na mwaka tunapoadhimisha kumbukumbu ya miaka 60 ya kuanzishwa kwake Mtaguso wa Pili wa Vatikano; kwa sababu Carmen alitoa maisha yake ili kuuleta Mtaguso katika maparokia, kupitia Uingizwaji wa Kikristo, kwa huduma ya maaskofu, ambao unaitwa Njia ya Neokatekumenato.

Inashangaza kuona historia hii yenye matukio na watu halisi; kazi isiyofanyika ofisini juu ya meza, bali kwa utendaji wa Roho Mtakatifu. Yale yaliyokuwa yanafafanuliwa na kutengenezwa na kuandikwa kwenye Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano, sisi tuliyaona yakitendeka na walio maskini vibandani huko Palomeras kwa kazi ya Roho Mtakatifu. Tumeona hapo Bwana akitokea na kuumba msamaha, upendo, ushirika, jumuiya ya kikristo! Carmen, kama mimi vile vile, tumekuwa mashahidi wa uwepo wa Mungu katika uinjilishaji, mashahidi wa utendaji wa Mungu katika Kanisa la Mtaguso wa Pili wa Vatikano. Hatukuwa na mipango au mawazo yetu wenyewe. Kwa zaidi ya miaka 50 tumeweza kushuhudia kwamba Mungu yu hai katika Kanisa lake.

Carmen, akifuata nyayo za Mtakatifu Fransisko Ksaveri (sherehe yake tumeadhimisha jana), hakuwahi kufikiri kubaki Hispania, kwani ilikuwa kwake kama kushindwa katika lengo lake la kimisionari. Lakini Mungu alitaka tukutane huko Madrid, vibandani Palomeras Altas. Tulifahamiana mwaka 1964, baada ya kurudi kwake kutoka hija yake ya kihistoria kwenye Nchi Takatifu. Mimi nilikuwa nimeenda kuishi kwenye kibanda fulani pamoja na watu maskini wa Palomeras.

Huko Carmen alifahamu jumuiya ya ndugu waliokutana katika kibanda changu na alivutiwa sana na jibu walilotoa kwa Neno la Mungu. Aliamua kukaa kuishi nasi, tukamjengea kibanda.

Carmen aliona uwepo wa Yesu Kristo, anayekuja kuwaokoa wenye dhambi, kutekeleza fumbo la Pasaka na kuunda ushirika kati ya maskini: Yesu Kristo alikuwa akijitoa kama upendo bure kwa kila mtu.

Haya yote ambayo Mungu aliruhusu, uwepo wake huko Palomeras, ulikuwa kama udongo ambao Mungu alikuwa ametayarisha ili kuutia ndani ya Kanisa. Kile ambacho Mungu alituonjesha katikati ya ulimwengu fukara, Roho Mtakatifu alikuwa amekitayarisha kwa ajili ya Kanisa lake.

Uwepo kama zawadi ya mungu wa Askofu Mkuu wa Madrid huko vibandani ndicho kilichomfanya Carmen kuamua kushirikiana nami kwa namna mkataa. Isingalikuwa kwa Mhashamu Casimiro Morcillo, tusingalienda katika maparokia. Pia ni yeye aliyetufungulia milango huko Italia. Carmen aliona uwepo wa Kanisa katika askofu mkuu na alibadili kabisa msimamo wake juu yangu. Kwa uwepo wa Morcillo, aliiona ahadi ambayo Mungu alikuwa amemfanyia huko Israeli kutimia.

Wakati Carmen alipokuwa Israeli, mara kwa mara alijiuliza utume wake ulikuwa upi katika Kanisa, akafikiri kwamba alipaswa kuunda shirika la wamisionari. Huko Ein Karem alipata uhakika kamili, kama maono, kwamba Mungu alitaka kitu kutoka kwake kwa ajili ya Kanisa zima, kwamba halikuwa suala la kuanzisha shirika.

Ninawaambia haya ili mpate kuona, kama fumbo kuu la Bwana, ushirikiano kati yangu na Carmen.

Ilikuwa vigumu sana kwangu kumkubali Carmen, hadi Bwana aliponiambia ndani yangu kwamba Carmen alikuwa neema kubwa kabisa, yaani, kuwa na mtu karibu nami ambaye aliniambia ukweli kila mara, kwamba Mungu alikuwa amemleta kwa ajili ya utume fulani. Kwa hivyo, nilimpokea Carmen katika imani kama aliyetumwa na Bwana. Niliteseka mpaka nilipogundua kwamba yeye alitoka kwa Mungu, na tangu siku hiyo amekuwa neema kwangu.

Carmen amekuwa mzuri ajabu! Mwanamke wa pekee ambaye amefanya mema mengi, si tu kwa ajili ya ndugu wa Njia ya Neokatekumenato, bali kwa Kanisa zima.

Njia ya Neokatekumenato Carmen Hernández katika Kaburi Takatifu la Yesu
Carmen Hernández katika Kaburi Takatifu la Yesu

Carmen, mwanamke mzuri kama nini! Mwenye kipaji kikubwa mno cha uhuru na cha upendo kwa Kanisa. Hakuwahi kamwe kunisifu, daima aliniambia ukweli. Alibaki daima nyuma yangu; daima kando yangu, kunisaidia. Hakutafuta nafasi ya kwanza, hakutafuta kamwe umaarufu. Alijua wazi kwamba utume ambao Mungu alikuwa amempa ulikuwa kuniunga mkono, kunitetea na kunisahihisha, kwa manufaa ya Njia ya Neokatekumenato.

Kwa upendo kwa Kanisa na ndugu, amebaki nami kwa miaka 52, ingawa wakati mwingine ilikuwa vigumu kwake, lakini Carmen alijali tu kufanya mapenzi ya Mungu, ambayo aliona ilikuwa kukaa pamoja nami katika Uingizwaji huu wa Kikristo ambao ni Njia ya Neokatekumenato.

Mwanamke wa kipekee, kwa kweli, mwenye ukarimu mkubwa sana, alijikana mwenyewe ili mimi nionekane, pamoja na kunisahihisha, lakini alikuwa nyuma yangu kila wakati, akinitegemeza.

Yeye ni kielelezo katika ukarimu, katika unyofu, katika kusema kwa uhuru na watu wote; aliwaambia ukweli ndugu wa jumuiya. Na wakati ndugu mmoja alipoenda mbali, alimpigia simu na kumtafuta, kama kondoo aliyepotea, kwa upendo.

Alikuwa mwanamke wa ajabu, nabii wa kweli, mtume wa kweli, ambaye aliishi imani yake kwa kiwango cha kishujaa. Mwanamke wa kipekee! Muhimu sana kwa Kanisa, daima katika sala, aliye shikwa upendo na Kristo, Maandiko Matakatifu na Pasaka, na kwa upendo bila masharti kwa Papa na Kanisa.

Njia ya Neokatekumenato Kiko Argüello na Carmen Hernández katika Kanisa la Kupalizwa Bikira Maria huko Fuentes de Carbonero - Segovia - Hispania

Pamoja sisi ni waanzilishi wa karama ambayo Bwana amevuvia kwa msaada wa Kanisa lake. Maneno ya Baba Mtakatifu Fransisko katika kuadhimisha miaka hamsini ya Njia ya Neokatekumenato mwaka 2018, aliposema huko Tor Vergata, Roma: “Ninyi ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa”, yanathibitisha shauku ile aliyotamani Carmen zaidi: kwamba ionekane kuwa katika Njia ni Mungu anayetenda, kwamba ni kazi ya Roho Mtakatifu ndani ya Kanisa, ambayo Yeye mwenyewe ametuitia sisi kuwa waanzilishi wake.

Katika hadhira ya mwisho aliyotujalia mwaka huu kwa Kikundi cha Kimataifa cha Njia, Papa Fransisko alidhihirisha furaha yake kwa ufunguzi wa Mchakato.

Natamani kwamba Kanisa, katika Mchakato huu wa Kutangazwa Mtakatifu unaoanza, lichunguze maisha yake, ambayo mara nyingi yalikuwa maisha ya kusulubiwa, katika ukimya na mateso, kana kwamba “kwenye usiku wa vivuli”; Pia nataka kwamba fadhila zake zidhihirike, nyingi zikiwa zimefichika, nyingi kwa kiwango cha kishujaa. Kanisa lipambanue juu ya hayo.

Ninamshukuru Mungu kwa kuweza kumfahamu na kuweza kufanya kazi pamoja naye katika “kazi ngumu za Injili”! kama asemavyo Mtakatifu Paulo.

Carmen! mwanamke mkuu hivi, mwenye imani ya kipekee! Upendo gani mkuu amekuwa nao kwa Kristo na Kanisa lake!

Asanteni.

Njia ya Neokatekumenato ufunguzi wa mchakato wa kutangazwa kuwa mwenye heri na mtakatifu wa Carmen Hernández 4-Des-2022
Chanzo: archimadrid.es – Luis Millán

Sasa tusikilize Injili.

Jioni hii tungependa kuwasilisha kifungu cha Injili ambacho kilimgusa sana Carmen: Kugeuka Sura, ambayo ndiyo hatima ya ajabu na ya kushangaza katika historia ya mwanadamu, na ambayo imekwisha kukamilishwa na Bikira Maria, aliye sura, siyo tu ya Kanisa, bali pia ya ubinadamu wote.

Kugeuka Sura kwa Bwana kutamwongoza mwanadamu huyu aliyechukuliwa na Yesu Kristo hadi umunguisho kamili. Ni kuinuliwa hadi utukufu wa mbinguni, hadi Kupaa. Na hilo linaweza kuonjwa hapa, kwa sababu wakristo, kupitia ubatizo, tunageuzwa siku hadi siku; hata ikiwa mwili huu unachakaa, tunageuzwa kuwa sura ya Yesu Kristo. Hii ndiyo imani ya Kikristo inayozaa historia, kesho ya ubinadamu: Kugeuka Sura.

Tangazo la Injili: Mk 9:2-8.

Njia ya Neokatekumenato mchoro wa Kiko Argüello: Kugeuka Sura

Maneno ya mwombaji wa mchakato Carlos Metola

Kwa Mha. Askofu Carlos Osoro Sierra, Kardinali-Askofu Mkuu wa Madrid.

Madrid, Julai 20, 2021. Sherehe ya nabii Eliya.

“Kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, ndivyo njia zangu zilivyo juu sana kuliko njia zenu” (Isaya 55:9)

Mwenye kutia saini hapa chini, Bw. Carlos Metola Gómez, niliyeundwa kihalali kama Mwombaji wa Jimbo kwa niaba ya Njia ya Neokatekumenato, Taasisi ya Familia ya Nazareti kwa ajili ya Uinjilishaji msafiri iliyoko Madrid na Taasisi ya Familia ya Nazareti kwa ajili ya Uinjilishaji msafiri iliyoko Roma, pamoja na watendaji wa mchakato wa kutangazwa kuwa mwenye heri na kutangazwa kuwa mtakatifu kwa mtumishi wa Mungu

MARÍA DEL CARMEN HERNÁNDEZ BARRERA, katekista mlei
ANAOMBA kutoka kwako, Mheshimiwa sana, kwa niaba ya watendaji, na kwa kufuatana na Katiba ya Kitume Divinus perfectionis Magister, na pia na Normae Servandae in Inquisitionibus ab Episcopis Faciendis in Causis Sanctorum, na Maelekezo Sanctorum Mater juu ya mchakato elekezi wa kijimbo katika michakato ya Watakatifu,
AONE VEMA kuanzisha maelekezo ya kijimbo wa Mchakato unaorejea katika Jimbo lako Kuu la Madrid.
archimadrid.es – Luis Millán

Kukusanywa kwake Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano na Papa Mtakatifu Yohane XXIII kupitia Katiba Humanae Salutis lilisema kinabii: “Kanisa linashuhudia katika siku zetu dhahama kubwa ya ubinadamu. Mpango mpya unaundwa, na Kanisa linaona tume kubwa mbele yake, kama katika nyakati za huzuni zaidi katika historia. Kwa sababu kinachotakiwa kwa Kanisa leo ni kupenyeza ndani ya mishipa ya ubinadamu wa leo wema wa kudumu, ulio hai na wa kimungu wa Injili.”[1]

Moja ya matunda mengi ya Mtaguso huu wa Pili wa Vatikano ni Njia ya Neokatekumenato, kama Papa Mtakatifu Paulo wa Sita alivyosema: “Tazameni matunda ya Mtaguso! Ninyi mnafanya baada ya Ubatizo kile ambacho Kanisa la mwanzo lilifanya kabla ya Ubatizo: kabla au baada, si muhimu. Swala ni kwamba ninyi mnatazamia uhalisi, utimilifu, uwiano sawia, unyofu wa maisha ya Kikristo”.[2]

Pia Papa Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili aliandika katika barua yake Ogniqualvolta: “Natambua Njia ya Neokatekumenato kama njia ya malezi ya kikatoliki inayofaa kwa jamii na nyakati za leo”, na “Ninatamani kwa dhati kwamba ndugu zangu katika uaskofu wathamini na kusaidia – pamoja na mapadre wao – kazi hii kwa ajili ya uinjilishaji mpya.” [3]

Nilitaka kuanza kwa kuwanukuu hawa mapapa watatu watakatifu na wapendwa, kwa sababu ya upendo mkuu ambao Mtumishi wa Mungu María del Carmen Hernández Barrera amekuwa nao katika maisha yake yote kwa ajili ya Kanisa na kwa ajili ya kichwa chake kinachoonekana, Baba Mtakatifu. Yeye, pamoja na Kiko Argüello, wamekuwa waanzilishi wa Njia ya Neokatekumenato, ambayo, kama tulivyoeleza, ni tunda mojawapo la Mtaguso huu wa Pili wa Vatikano. Carmen Hernández alijitolea kwa nguvu zake zote kwa miaka 52 kwa huduma bila kukoma ya tangazo msafiri la Injili na kuwa chombo, kama “mtumishi asiyefaa” [4] wa Kristo katika upyaisho wa Kanisa lake.

María del Carmen Hernández Barrera alizaliwa Ólvega, jimbo la Soria, tarehe 24 Novemba 1930, kutoka familia ya kikatoliki yenye watoto tisa; yeye alikuwa mtoto wa tano, na tangu alipokuwa mdogo alitaka kuwa mmisionari, wito ambao ulizaliwa na kulishwa kila mara wamisionari Wajesuiti kutoka Tudela (Navarra, Hispania) walipofika shuleni kwake na kuzungumza kuhusu utume. Mfano wa Fransisko Ksaveri ulimtia alama ya moto kwa maisha yake yote.

Baadaye, alifikiri kwamba kumfuata Kristo hakukuwa kufuata taaluma yake ya Kemia (ambayo alifuzu kwa matokeo mazuri sana) na kufuatia hivyo mradi wa maisha wenye matumaini ambao baba yake alimwekea ndani ya kiwanda kilichositawi cha mpunga na cha kifamilia, bali kwa kuingia katika Taasisi ya Wamisionari wa Kristo Yesu, iliyoanzishwa na M. María Camino Sanz Orrio, kwa msaada mkubwa wa Askofu Mkuu wa Pamplona wa wakati huo, Mha. Marcelino Olaechea. Akafanya hivyo mwaka 1954. Wakati wa miaka minane ambapo Carmen alikuwa pamoja na hao Wamisionari alipata malezi bora ya kiroho, ya maisha ya kijumuiya na ya kitume. Kwa kusoma shajara zake na maelezo ya dhamiri yake ya miaka hii, unashangaza sana upendo kwa Yesu anaoonesha, msemo anaourudia zaidi ni: “Yesu wangu, mimi nakupenda!”. Yanashangaza sana pia matukio mengi ya kiroho yenye kina sana, “karibu ya kitaamuli” na kujitoa sadaka kwa namna za kishujaa ambayo kupitia hayo Bwana alikuwa akimwongoza. Kati ya 1957 na 1960 alisomea Dini katika Taasisi ya Sedes Sapientiae huko Valencia, akiwa na baadhi ya maprofesa wazuri kabisa ambao kila mara amewataja; matokeo yake yalionyesha kipaji kikubwa sana na alikamilisha tasnifu (Makala yake ya utafiti) kwa kiwango cha Summa cum laude kuhusu “Haja ya sala katika mawazo ya papa Pius XII”. Haya yote yalitia ndani yake upendo mkubwa sana kwa sala ya kiliturjia, Ekaristi na Maandiko Matakatifu, kama nafasi za uwepo halisi na unaohitajika wa Kristo katika maisha yake ya kila siku.

Wakati tayari ilionekana kwamba kila kitu kilikuwa kinaelekeza hadi utume huko India, baada ya kukaa mwaka mmoja na nusu London, kama ilivyokuwa desturi katika Taasisi yake, akijifunza Kiingereza na kumaliza maandalizi ya kutumwa, Carmen Hernández aliteseka anachokiita yeye “badiliko la mwelekeo wa ndege” kwenye njia yake ya kumtumikia Mungu: wakubwa wake wanatilia shaka ufaafu wake wa kukiri nadhiri za daima na kumrejesha Hispania. Ilikuwa miezi minane ya kungoja ambayo Carmen alikaa katika moja ya nyumba za Wamisionari hao huko Barcelona. Wakati huu, Bwana alimfanya kupitia “kenosis” ya kina sana, ambamo shauku yake yote ya kuwa mmisionari ilikuwa muhali; yeye anasema kwamba Barcelona ilikuwa kama Mlima Moria, ambapo ilimbidi kumtoa “Isaka” (mpango wake wa maisha) kama sadaka. Ilimfariji kwenda kwenye Jumba la Makumbusho la Marés ambako “kuna misalaba mingi ya mtindo wa kirumi ambapo Kristo anaonekana akitawala juu ya msalaba”, wala si kwa kuvaa taji la miiba bali kwa taji la Mfalme, na hiyo ilimwalika kubaki katika mateso hayo, katika msalaba huo, kwa sababu ndivyo alivyofanya Yesu Kristo.

Lakini, zaidi ya yote, katika “Gethsemane” hii alitokea, kama malaika aliyemfariji, Padre Pedro Farnés, mwanaliturjia mkuu. Alimpitishia upyaisho wote wa kiliturujia, ambao wakati huo ulikuwa unaanza, na ugunduzi wa Mkesha wa Pasaka na nguvu ya Ekaristi, lakini sio kwa njia ya kinadharia, bali “ikifanyika mwili ndani yake mwenyewe” na hali za “mateso na kifo” alizokuwa anazipitia, kwa sababu ikiwa hangekubaliwa kukiri nadhiri: angeenda wapi? Nafasi yake ilikuwa ni ipi katika Kanisa? Kwa sababu jambo moja lilikuwa wazi kwake: Bwana alikuwa akimwita kuwa mmisionari! Alikuwa ameacha kila kitu kwa ajili Yake na kwa ajili ya Kanisa Lake! Alijifunza kwamba “Ukumbusho wa Kifo na Ufufuko wa Yesu Kristo” unadhihirishwa katika Ekaristi, na mtu anamshiriki kwa kuingiza uwepo wake, akifa na kufufuka pamoja Naye.

Ilipothibitishwa kwamba hakukubaliwa kwa nadhiri za daima, mnamo Agosti 28, 1962, mashaka yake yakimaisha yalizidi kuwa makali. Mlango mdogo unafunguliwa kwa sababu Askofu wa Oruro, nchini Bolivia, Mha. Jorge Manrique, anamwalika kwenda jimboni kwake kufanya kazi kati ya maskini wachimba madini. Lakini yeye alisikia hitaji la kwanza kwenda kwenye Nchi Takatifu, “Injili ya tano”, na kupata kufahamu nchi ambayo Yesu wake mpendwa alikanyaga. Akiwa na vitu vichache sana kwa kujikimu, anafanya hija katika Mahali Patakatifu mbalimbali pamoja na dada mmoja wa Ireland aliyemfahamu huko London. Wote wawili walizuru maeneo ya Israeli, mara nyingi wakitembea, wakisoma Maandiko mahali pale ambapo matukio hayo yalitukia; na walipata pesa kwa kupitia kusafisha nyumba, za Wayahudi na za Waarabu. Cha ajabu ni kwamba katika Nchi Takatifu kishawishi kikubwa kinamtokea Carmen, anapoalikwa kufanya kazi katika Taasisi ya Teknolojia ya Israel, Technion, huko Haifa, katika mradi wa utafiti wa kemikali, ambao yeye angeweza kuukubali, lakini aliukana kwa sababu wito wa Mungu ulikuwa na nguvu zaidi. Jioni nyingi alienda kwenye Mwamba wa Ukulu wa Petro, ambapo sauti ya Yesu inasikika bado ikisema: “Je, wanipenda?” Na Carmen alikuwa akimjibu “Ndiyo” na kumuuliza Bwana “mahali pake palikuwa nini ndani ya Kanisa”. Mnamo Agosti 1964 alirudi Hispania na kwenda kuishi Palomeras Bajas, mtaa wa vibanda nje kidogo ya Madrid. Huko Mungu tayari aliutayarisha mkutano na Kiko Argüello, kupitia dada ya Carmen aliyemjua. Tenzi moja ya Salomoni inasema kwamba Mungu anao kwa kila mtu “mpango wa usanii usiosemeka ” [5], na ndivyo ulivyo mpango ambao Bwana alikuwa ametayarisha na Carmen Hernández: wito wake usiozuilika wa uinjilishaji, ulioimarishwa na maandalizi yake makuu ya kiteolojia, ya kiroho na ya kiliturjia, unaunganika na mpango uliotayarishwa na Mungu kwa Kiko Argüello: uwepo wa Kristo anayeteseka katikati ya walio maskini zaidi na uwezo wake wa kukusanya na kuunda jumuiya ndogo. Kwake mwenyewe, Bikira alimfunulia kabisa miaka mitano kabla, tarehe 8 Desemba 1959: “Inabidi kufanya jumuiya za kikristo kama Familia Takatifu ya Nazareti zinazoishi katika unyenyekevu, urahisi na sifa, mwingine ni Kristo.” Kutoka muungano huu wa utume wa Carmen Hernández na Kiko Argüello Njia ya Neokatekumenato ilizaliwa, ikitiwa moyo tangu mwanzo na aliyekuwa Askofu Mkuu wa Madrid wakati huo, Mha. Casimiro Morcillo.

Njia ya Neokatekumenato Kiko Argüello, Carmen Hernández, Casimiro Morcillo

Katika Njia hii ya Neokatekumenato Carmen Hernández anachangia teolojia, uvuvio, utafiti na masomo, na Kiko anachangia utekelezaji, “usanifu” katika muhtasari wa kiteolojia-kikatekesi na wa kimaadili ambao huvutia wale walio mbali zaidi na Kanisa walioishi vibandani, na ambao wakati huo huo unaweza kufufua na kuhuisha imani katika waumini wa parokia; imani iliyotiwa muhuri katika ubatizo uliopokelewa wakiwa watoto, lakini ambayo mara nyingi haikukomaa hadi kufikia kimo cha imani ya watu wapevu. Hivi sasa, baada ya mbegu hii kutoka vibandani kuenea kupitia Kiko na Carmen na maelfu ya makatekista walioundwa nao, Njia ya Neokatekumenato imeenea katika nchi zaidi ya 130, zenye jumla ya jumuiya 21,066 duniani kote, zenye ndugu milioni moja na nusu, katika parokia 6,800. Kiko na Carmen, daima wakisindikizwa na mpresbiteri, wakiunda kikundi cha makatekista wasafiri wa uinjilishaji, wamekuwa na miaka 52 ya utendaji endelevu wa kuinjilisha ambao umesitawi katika nchi nyingi ulimwenguni pote. Carmen alizoea kusema: “Hii si kazi yetu: ni Mungu anayeiongoza.” Waanzilishi wa Njia hiyo wamekuwa zaidi ya miaka hamsini, kama Mtakatifu Paulo anavyosema, ya “kuhangaikia makanisa yote” [6]: magumu, kushindwa, mateso, safari nyingi, mikutano, kuishi pamoja, usiku bila kulala, bila malipo yoyote au usalama wa kiuchumi, wakiishi kwa msaada wanaopewa. Tunao uhakika, unaotegemea na kungojea bado maamuzi ya mwisho ya Kanisa, kwamba Carmen ameishi miaka hii ya maisha yake kwa kujishugulisha na uenezaji wa injili kwa kiwango cha kishujaa, bila kuwa na “mahali pa kupumzisha kichwa chake” [7]. Bila shaka, tangazo hili la Injili pia lilijaa furaha na faraja nyingi, wakiona utendaji na uwezo wa Bwana: “Mimi nipo pamoja nanyi siku zote, mpaka ukamilifu wa dahali” [8].

Jambo la ajabu ni kwamba katika hekaheka hii ya uinjilishaji, Carmen Hernández, katika shajara zake, mara nyingi anadokeza nyakati za “utupu”. Zinasema neno kwa neno: “Nimo kwenye utupu”, au “utupu kwenye utupu”; Baada ya kuwa na maang’amuzi ya Yesu ya karibu sana, na kushuhudia utendaji wa Mungu katika nafsi yake yenyewe au kuona utendaji wake katika maisha ya ndugu, baada ya kumwona Mungu mwenye nguvu hivi katika uinjilishaji, anapitia vipindi vya “utupu”: Yesu, Bwana Arusi, ameondoka, amemwacha peke yake kwa muda na anaonja “kutokuwapo kitu”. Katika maandishi yake, mara nyingi ananakili mistari kutoka kwa Mtakatifu Yohane wa Msalaba, na kueleza kwamba hakuna kitu kutoka duniani kinamvutia, hajisikii kuzungukwa na watu, anafikiria tu juu Yake, kuwa peke yake na Yeye. Anaandika: “Hatimaye, peke yangu nawe.” Anataka kuambiwa kuhusu Yeye, ndiyo maana anafuatilia daima matukio ya Mapapa, akisikiliza Redio Vatikano au kusoma na kusoma tena vitabu visivyohesabika vya Teolojia katika maktaba yake.

Shajara za 1979-1981

Carmen Hernández alijua kwamba uingizwaji huu wa kikristo wa Njia ya Neokatekumenato haukuweza kutendeka bila nguzo imara kadhaa ambazo yeye aliishi na kujaribu kuzipitisha kwa ndugu wa jumuiya:

– Upendo na haja ya kusali: Carmen alisali saa zote za Sala ya Kanisa, kwa moyo na raha, alifurahia kusali, na ilikuwa njia ya kuitakasa siku. Zaidi ya yote, alipenda Ofisi ya Masomo, ambayo aliiita “Pambazauko”, ambayo aliisali alfajiri, kwa sababu alisema kuwa zaburi zake “ni za kimaisha sana”. Hakuacha kamwe hata saa moja katika Sala ya Kanisa, hata kwenye safari na kuhama.

– Upendo kwa sakramenti, hasa Ekaristi, ambayo alishiriki kila siku, na upendo kwa Kitubio. Carmen alitoa miaka mingi ya masomo kwa sakramenti hizi mbili kwa vitabu bora vya Kikatoliki na wanateolojia waliojiandaa vema zaidi, pia akifikia mizizi ya kiebrania ya Ukristo, akisoma juu ya sikukuu za kiebrania ambazo Yesu Kristo aliadhimisha kama Myahudi na ambazo ni kama vyanzo vya sakramenti zetu: Pasaka ya Kiyahudi, Siku ya Upatanisho (Yom Kippur) au Pentekoste (Shavuot).

– Upendo kwa Maandiko Matakatifu, ambayo alifahamu kikamilifu, na aliyokaa nayo kwa masaa na masaa, akisoma na kusoma tena vifungu, akigundua tofauti nyingi ndogo ndogo na maana nyingi mbalimbali. Biblia za Carmen zimepigiwa mistari tena na tena: inavutia kuziona kwa sababu ya jinsi “zimetumika na kupigwa mistari”.

– Carmen Hernández alikuwa msomi wa kudumu wa Imani ya Kikatoliki, pamoja na Mababa wa Kanisa na Mapokeo yote ya Mafundisho ya Kanisa, maktaba zake zina zaidi ya vitabu 4500 vya dini na mamia ya majarida ya Teolojia. Alisikiliza Redio Vatikano kila siku, alisoma “L’Osservatore Romano” (gazeti rasmi la Mji wa Vatikano, akilichora mistari na/au kukata makala ya kuvutia zaidi). Alisoma toleo la kila siku kwa Kiitaliano na lile la kila wiki kwa Kihispania. Alifuatilia hotuba zote za Mapapa, hasa za Mtakatifu Yohane Paulo II na Benedict XVI.

Siku zote alikuwa kando na Kiko Argüello, katika miaka hii hamsini, akimtia moyo na kumsaidia katika kuandaa na kuendeleza mikusanyiko, mikutano, kuishi pamoja na pia akimsahihisha (“kumsahihisha kindugu”) katika yale aliyoona ni muhimu, hasa ili asijivunie kwa kuona mafanikio mengi katika kazi hii ya Mungu, akimwambia kwamba walikuwa tu “watumishi wasiofaa”. Mara nyingi alikaa kimya (hasa mwishoni, alipokuwa na nguvu kidogo au kutokana na magonjwa), lakini aliendelea kuwatia wote moyo , iwe Kiko, kama vile makatekista na ndugu katika jumuiya. Vivyo hivyo, alikuwa mwanamke ambaye alizungumza kwa uhuru mwingi.

Njia ya Neokatekumenato ufunguzi wa mchakato wa kutangazwa kuwa mwenye heri na mtakatifu wa Carmen Hernández 4-Des-2022
archimadrid.es – Luis Millán

Alikuwa na upendo wa pekee kwa “kondoo waliopotea”, yaani, wale watu waliokuwa na hali ya mateso, ama ndugu wa jumuiya ambaye alikuwa anapitia nyakati ngumu, au aliyekuwa katika misukosuko; Carmen alimpigia simu na kumtia moyo ili akutane tena na Yesu Kristo katika sakramenti, katika Neno na katika sala, na kumwambia aombe msamaha. Alikumbuka na kujua majina na hali za familia na za kazi za mamia ya ndugu kutoka jumuiya ambazo wao wenyewe walikuwa wamewapatia katekesi, pamoja na mamia ya makatekista wasafiri kutoka vikundi mbalimbali vya uinjilishaji.

Katika miaka ya mwisho ya ugonjwa wake aliendelea, kadiri alivyoweza, kasi ya uinjilishaji wa ulimwengu: safari, kuishi pamoja, mikutano, kuhama hapa na pale… ingawa hii ilimaanisha mateso zaidi ya kimwili na maumivu zaidi, kutokana na magonjwa yake ya moyo, shinikizo la damu kupanda, maumivu ya mguu (alikuwa na kidonda ambacho hakingepona kutokana na mzunguko mbaya wa damu), maumivu ya mgongo (alikuwa na mifupa kadhaa iliyovunjika katika uti wa mgongo pamoja na maumivu makali sana) na maumivu ubavuni (baadhi ya mbavu zilivunjika kwa sababu ya kuanguka mara kadhaa; ambazo ijapokuwa baadaye ziliunganishwa tena, bado ilikuwa sababu ya mateso). Mara nyingi alishiriki katika mikutano akifuatilia sauti kutoka chumbani mwake. Kifo chake huko Madrid, Julai 19, 2016, kilikuwa mpito wenye utulivu kuelekea pumziko la milele; alikuwa “akizimia” bila wakati wowote wa kushindana au kuasi, bali kwa amani na utulivu mkubwa.

Kwa hivyo, Mwadhamu Mheshimiwa sana, TUNAAMINI NA KUTHIBITISHA kwamba:

– Carmen Hernández ameweza kuishi fadhila za Kikristo kwa kiwango cha kishujaa: imani, matumaini, mapendo, busara, haki, nguvu, kiasi, uvumilivu katika mateso, utauwa, kukubali mapenzi ya Mungu, upendo wa kina sana kwa Kanisa na Yesu Kristo, upendo mkubwa sana kwa sala, kwa viongozi wa Kanisa, mwenye uhuru mkubwa katika kusahihisha kindugu, na tunaamini tuna uthibitisho wa kutosha kwa hili, kupitia maandishi yake mengi ya kibinafsi, katekesi, barua na shuhuda kutoka kwa watu wengi ambao wamemjua.

– Kuna umaarufu mkubwa wa ishara na fadhila ulioenea kati ya taifa la Mungu, kwamba Carmen Hernández anawaombea mbele za Mungu, kutokana na neema na fadhila nyingi ambazo wamemwomba na wanaendelea kumwomba kila siku. Tumepokea shukrani zaidi ya 1,500 kutoka zaidi ya nchi 70 tofauti duniani pote.

– Idadi kubwa sana ya wanaozuru kaburi la Carmen Hernández (zaidi ya watu 50,000 kutoka nchi 70 tofauti duniani wamepita), na kuacha katika vitabu vya rambirambi shukrani na maombi takriban 25,000.

– Maelfu ya waumini huhudhuria Misa za mazishi, pamoja na Misa za kumbukumbu yake, Julai 19 ya kila mwaka, katika sehemu nyingi za dunia.

– Mapokezi makubwa kwa upande wa watu ya vitabu na maandishi ya Carmen Hernández au wasifu wake, vilivyochapishwa hadi sasa, na manufaa makubwa ya kiroho yanasema vitabu hivi vinafanya.

– Na umaarufu huu wote wa utakatifu wa Carmen Hernández, ambao tunauthibitisha na kuuhakikisha, umeonekana bila kuwa na kipeperushi chochote cha ombi, au tovuti yoyote, au matangazo maalum, ili kutoshawishi wala kutunga umaarufu huo wa utakatifu.

Kwa sababu hizi zote, IKISHAPITA MIAKA MITANO baada ya kifo cha mtumishi wa Mungu, kama ilivyo kanuni katika Michakato ya watakatifu:

NAOMBA kutoka kwako, Mheshimiwa sana, kupitia Supplex Libellus hii, uone vema kuangalia manufaa ya KUANZISHA MCHAKATO kuhusu maisha, fadhila na umaarufu wa utakatifu wa Mtumishi wa Mungu María del Carmen Hernández Barrera, aliyefariki katika Jimbo Kuu lako Julai 19, 2016.

Ni neema ambayo natamani kuipata kutoka kwako Mheshimiwa sana, na Mungu akuhifadhi kwa miaka mingi.

Amani

Carlos Metola Gómez
Mwombaji wa Awamu ya kijimbo

KIAMBATISHO

Kama inavyotakiwa na makala n. 37 ya Maelekezo Sanctorum Mater, ninaliambatanishia Ombi hili hati zifuatazo:

  1. Mamlaka yangu ya usimamizi kama Mwombaji wa Mchakato;
  2. Wasifu wa mtumishi wa Mungu María del Carmen Hernández Barrera;
  3. Vielelezo halisi na nakala zao za machapisho ya mtumishi wa Mungu; baadhi ni maandishi yaliyochapishwa na tayari yamewekwa hadharani; na nyingine ni hati ambazo hazijachapishwa hadharani, zilizochapishwa “pro manuscripto” kwa matumizi ya ndani ya makatekista wa Njia ya Neokatekumenato.
  4. Orodha ya mashahidi wanaoweza kusaidia kufafanua ukweli kuhusu maisha, fadhila na umaarufu wa utakatifu wa mtumishi wa Mungu.

[1] Katiba ya Kitume “Humanae Salutis”, 3. 25 Desemba 1961.

[2] Hadhira ya wote ya Papa Paulo wa Sita, 8 Mei 1974, Mji wa Vatikano.

[3] Barua “Ogniqualvolta” kwa Mha. Paul Josef Cordes, 30 Agosti 1990.

[4] Taz. Lk 17:10.

[5] Tenzi za Salomoni, 24.

[6] Taz. 2 Kor 11:28.

[7] Taz. Mt 8:20

[8] Taz. Mt 28:20.


archimaddrid.es – Luis Millán

SHAIRI LA KISIMFONIA AKEDAH

Tutasikiliza shairi la kismfonia lenye jina la “Aquedá”. Neno Akedah, ni neno la kiebrania, ambalo linamaanisha “Nifunge” na liko katika Targum Neofiti, ambayo ni ufafanuzi wa kiebrania unaopatikana katika maktaba huko Roma ambapo Waebrania walihubiriwa. Na katika targum hiyo imo tafsiri ya kifungu cha Abrahamu kinachoelezea sadaka ya Isaka na kuongeza kile ambacho malaika anamwambia: «Njooni mwone imani juu ya nchi: baba anayemtoa mwanawe wa pekee, na mwana mpendwa anayemtolea shingo yake».

Nimeweka muziki kwa andiko hili linalomhusu Isaka, sura ya unyenyekevu wa Kristo, ambaye akiwa Mwana wa Mungu alijinyenyekeza, akajifanya dhambi kwa ajili yetu. Kipande hiki kinaakisi wakati Abrahamu alipokuwa akijiandaa kumtoa mwanawe sadaka, na akimkazia macho anamweka juu ya kuni. Na anapoelekea kumuua, Isaka anamwambia: “Nifunge, nifunge sana, baba yangu, nisije nikashindana kwa hofu, na sadaka ikawa bure nasi tukakataliwa.”

Kwa sababu kutokana na utaratibu wa Hekaluni, mwanakondoo aliyetolewa sadaka alipaswa kuwa mpole sana. Ndiyo maana walikuwa wakitafuta kati ya wanakondoo jike wote—ambayo ni sura ya Bikira Bila doa—kondoo jike ambaye alikuwa mpole hivi kwamba angemzaa mwanakondoo ambaye wakati watakapomfunga hatapiga teke, kwa sababu akitikisika na kupiga teke, sadaka inabatilika. Hiyo iko katika Talmud, katika mapokeo ya marabi, na hivyo unyenyekevu wa Bwana Wetu Yesu Kristo umebashiriwa, kwa sababu Isaka ni mfano wa Kristo.

Carmen alisimulia mara nyingi kwamba aliishi katika mwili wake mang’amuzi ya Abrahamu: ahadi ya kuwa mmisionari ilimsindikiza katika utoto wake na ujana wake, hadi alipokaa Barcelona ambayo ilimaanisha kwake kupanda Mlima Moria. Kama vile Abrahamu alivyompeleka Isaka kutolewa sadaka kwenye Mlima Moria, Carmen atampeleka na kumtoa sadaka “Isaka wake”, yaani, wito wake mwenyewe, mpango wake wa maisha ya kimisionari, tamaa zake za kwenda katika utume mbalimbali.

Carmen alisimulia kwamba ulikuwa wakati wa majaribu wenye nguvu zaidi wa maisha yake, wa kushuka mpaka kilindini kabisa; lakini wakati huohuo ni pale ambapo aliuona uso wa Mungu, Ufufuo na Uzima wa Milele.

SHAIRI LA KISIMFONIA “BINTI ZA YERUSALEMU”

Shairi la pili la muziki linaitwa “Binti za Yerusalemu”, na pia linatupeleka Israeli. Kilichomsisimua Carmen zaidi kuhusu Yerusalemu ilikuwa kuona kwamba kutoka kwenye Mlima wa Mizeituni msalaba wa Kristo ungeweza kuonwa kidogo. Nimejaribu kuweka muziki kwa kifungu cha Mateso ya Bwana kadiri ya Mtakatifu Luka. Kristo amewekwa chini ya mateso ambayo, kulingana na mwandishi Cicero, hakujawahi kuwepo mateso makubwa zaidi ulimwenguni: mateso ya msalaba.

Mfikirini Yesu Kristo akivuka Yerusalemu akiwa amejitwalia msalaba, mwili wake wote ukiwa umevimba kwa mapigo aliyopokea na mijeledi ya kirumi. Juu ya Sanda Takatifu unaweza kuona alama zilizosababishwa na mijeledi ambayo Yesu Kristo alipokea, ambazo zilimfanya mwili wake wote kuvimba. Kumwona Kristo kwa namna hii kwa kweli kulionekana kama dubwana, akijaa damu. Ndivyo ilivyo sura ya Bwana wetu Yesu ambaye akipita katika barabara kulikuwa na wanawake ambao walipomwona walianza kupiga kelele kama wafanyavyo huko Mashariki. Yesu anasimama na kuwaambia: “Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, jililieni nafsi zenu na watoto wenu. Kwa sababu wakitenda haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?».

Maneno haya ya Injili ni ya kutisha: “wakitenda haya katika mti mbichi”; Ikiwa haya yanafanyika kwa yule asiye na hatia, ni nini kitakachofanywa na wenye hatia wa kweli, tulio sisi? Je, Yesu Kristo anamaanisha nini kwa hili? Kwamba hana budi ila kwenda kuokoa ubinadamu wote, sisi sote, kutoka mateso matupu, kutoka motoni, kutoka yale shetani alikuwa ametayarisha kwa ajili ya mti mkavu tulio sisi. Neno hili la injili, lenye kina sana, lenye kushangaza sana, linalotoa maana kwa Mateso na Kifo cha Bwana Wetu Yesu Kristo, ndilo tunaloelekea kusikiliza. Nimejaribu kidogo kuweka muziki juu yake na ninatumaini uweze kuwasaidia.

Njia ya Neokatekumenato ufunguzi wa mchakato wa kutangazwa kuwa mwenye heri na mtakatifu wa Carmen Hernández 4-Des-2022
Okestra ya Kisimfonia na Kwaya ya Njia ya Neokatekumenato imeundwa na walimu na wanamuziki walio ndani ya Njia ya Neokatekumenato.

Leo wapo:

  • Wanamuziki 94 (wapiga ala na mpiga kinanda mmoja)
  • Wanakwaya 80

Okestra inaongozwa na Tomáš Hanus:

Anatoka Jamhuri ya Czech; ameoa; ana watoto 8 na yupo ndani ya Njia ya Neokatekumenato. Mnamo 1999 alishinda shindano la kimataifa la waongozaji wa okestra na tangu wakati huo ameongoza okestra za Philharmonic (Pendauwiano) katika nchi kadhaa za Ulaya, pia katika Teatro Real huko Madrid. Kwa sasa anafanya kazi katika Prague Philharmonic na ni Mkurugenzi wa Muziki wa Opera ya Kitaifa ya Wales.


Maneno ya Mha. Carlos Osoro Sierra, Kardinali-Askofu Mkuu wa Madrid

Ninasalimia kwa upendo mkubwa kikundi cha kimataifa cha Njia ya Neokatekumenato, Kiko, Padre Mario na Ascensión, wanaoendeleza Mchakato ya Kutangazwa Mtakatifu ambao tumefungua sasa hivi. Nawasalimu kindugu Makardinali, Maaskofu wakuu na Maaskofu wote ambao mmetaka kuandamana nasi katika wakati huu muhimu sana hivi, sio tu kwa maisha ya Njia ya Neokatekumenato, bali kwa maisha ya Kanisa. Nawasalimia kwa upendo mapadre wote na waumini walei, hasa wale ambao wako kwenye utume, na wale wote wanaofuatilia tukio hili mtandaoni.

Njia ya Neokatekumenato ufunguzi wa mchakato wa kutangazwa kuwa mwenye heri na mtakatifu wa Carmen Hernández 4-Des-2022

Sisi sote ambao tumemfahamu Carmen kwa karibu, kama mimi, hasa nilipokuwa Askofu Mkuu wa Valencia, tunajua kwamba amekuwa mtu mwenye karama nyingi, jasiri, mwenye shauku, aliyeshikwa upendo kwa dhati na Yesu Kristo. Wakati mwingine mwenye shauku kiasi kwamba iliweza kuonekana kama kukosa adabu (“politically incorrect”) . Ningependa kuangazia vipengele vyake vitatu ambavyo kwangu ni muhimu sana kwa Kanisa letu na jamii yetu:

Kwanza, upendo wake mkubwa kwa Kanisa, na hasa kwa Papa. Tayari kama kijana mnovisi alifanya tasnifu yake juu ya “Haja ya sala katika mawazo ya Pius XII”. Lakini ilikuwa na Mtakatifu Paulo wa Sita ambaye alianza naye kuwa na uhusiano wa karibu na kila mmoja wa Mapapa, uhusiano ambao ulikuwa na nguvu sana hasa na Mtakatifu Yohane Paulo II, na Benedict XVI, na Papa Fransisko. Alimpenda Papa, yeyote awaye, hakuwa wa Papa huyu ama wa yule. Alipokuwa tayari mgonjwa hapa Madrid, Papa Fransisko alimpigia simu. Alimwambia atulie, kwa sababu magugu hayafi kamwe, na alimwambia kwamba angempatia sigara. Uhusiano wake na mrithi wa Petro ulifikia hali hiyo ya kuaminiana. Lakini kilicho nyuma ya ukaribu huu ni upendo wa kina kwa Kanisa, katika roho ya utii kama mwana. Ina maana kubwa kwamba alitambua kwamba inambidi kukaa na Kiko vibandani alipoona uwepo wa Askofu Mkuu Morcillo.

Pili, nataka kuangazia ujasiri wake wa kusema bila woga kuhusu Injili, ukweli na haki. Maneno yake, ambayo wakati fulani yalikuwa makali sana, yalizaliwa na kusadikishwa kwamba ukweli peke yake ndio humweka huru mwanadamu, na Kristo ndiye ukweli. Carmen alitangaza Injili hadi miisho ya dunia, akifuata roho ya umisionari ambayo aliona kuzaliwa ndani yake akiwa mtoto. Kama tulivyokumbuka katika wimbo mwanzoni mwa tukio hili, aliweza kusema na maisha yake: “Vifungo vyangu vimevunjika … naenda mahali pote.”

Na tatu, ingawa tungeweza kusema mambo mengi, nataka kusisitiza umuhimu na heshima ambazo Carmen alimpa mwanamke, kwa nafasi yake katika maisha, katika jamii na katika Kanisa. Uzuri wa tumbo la uzazi, ambamo kila mtu ametungwa, na ambamo Mwana wa Mungu alifanyika mwili. Muujiza wa uhai ambao huzaliwa ndani ya mwanamke. Na pia mwelekeo wake wa kieskatolojia: mwanamke aliyevikwa jua ambaye hushinda nyoka.

Hatupaswi kusahau, lakini, kwamba tukio hili linamaanisha mwanzo tu wa mchakato wake wa kutangazwa kuwa mwenye heri, ambamo tutakusanya hati zote na shuhuda zote ambazo baadaye zitamsaidia Papa kupambanua juu ya maisha yake, fadhila zake na umaarufu wake wa utakatifu. Ni mwanzo wa njia ndefu, ambapo tutakagua shuhuda zote kinaganaga, zile zinazosaidia mchakato huu, kama vile zile ambazo zitaenda kinyume na mchakato huu. Ninawahamasisha mwombe maombezi yake Mtumishi wa Mungu Carmen Hernández. Na ninatamani kutoka moyoni kwamba mchakato huu ufikie hatima njema, Mungu akipenda.


Share: