Benedict XVI, Kiko Argüello, Carmen Hernández  na Pd. Mario Pezzi hadhira

UJUMBE WA KIKO KWA JUMUIYA ZA NEOKATEKUMENATO

Madrid tarehe 31 Desemba 2022 Kumbukumbu ya Mtakatifu Silvester, Papa

Ndugu wapendwa:

Tumepokea hivi punde habari za kwenda kwa Baba kwa Papa Mstaafu Benedict XVI.

Nakwakumbusha kwamba, tangu alipokuwa Profesa, na baadaye akiwa Mkuu wa Idara ya Mafundisho ya Imani, na kisha akiwa Papa, tumekuwa daima na shukrani ya pekee na upendo kwake; baada ya Papa Mtakatifu Paulo VI na Papa Mtakatifu Yohane Paulo II, ameitegemeza na kuitetea Njia ya Neokatekumenato.

Tangu miaka ya 1970, kama profesa katika Chuo Kikuu cha Regensburg, baada ya kuifahamu Njia ya Neokatekumenato kupitia ushuhuda wa wanafunzi wake wawili, Stefano Gennarini, Shahada ya Uzamivu katika Fizikia, na Toni Spandri, Shahada ya Uzamivu katika Sheria, na pia kupitia mkutano binafsi pamoja na Carmen na mimi, katika nyumba yake huko Pentling (Bavaria) mnamo 1973, aliandika barua kwa maparoko watatu kutoka Munich huko Bavaria mnamo Juni 22, 1974, akipendekeza waifungue Njia katika parokia zao, akisema:

“Nimesadiki, baada ya mazungumzo mengi (pamoja na wanafunzi wale wawili na Kiko na Carmen), kwamba hapa tunashughulikia tumaini la kweli la upyaisho ambao, ukitokana na roho ya Biblia na Mababa, umejikita vema katika Kanisa halisi, unajiunga na paroko, lakini pia wakati huohuo unafungua njia mpya za maisha katika imani. Kwa yale niliyoyasikia, hata Papa (Paulo VI) kwa sasa, kutokana na mada ambazo zimewasilishwa kwake, amejieleza juu ya mkondo huu kwa namna chanya kupita maelezo ya kawaida. Kwa hiyo, ingekuwa shauku yangu kubwa kwamba mang’amuzi haya yapate pia kuanza nchini Ujerumani.”

Akiwa Kardinali, na Mkuu wa Idara ya Imani, kwa amri ya Papa Yohane Paulo II, alianzisha mchakato wa uchambuzi kwa ajili ya kuziidhinisha Katekesi na Statuta, na baada ya kuteuliwa kama Papa Benedict XVI, akaziidhinisha kikamilifu: Statuta za Njia ya Neokatekumenato kupitia Tamko la Mei 11, 2008, na Mpangilio wa Katekesi kupitia Tamko ya Desemba 10, 2010.

Yangekuwa mengi matukio ambayo yangepaswa kukumbukwa, msaada wake wa daima na upendo wake kwangu na kwa Carmen na kwa Njia ya Neokatekumenato, hasa katika Ujerumani.

Katika ushirika na Papa Fransisko na Kanisa zima, tunaziomba Jumuiya zote za Njia ya Neokatekumenato kumwomba Bwana apokee roho yake, amsamehe dhambi zake na kumshirikisha katika Utukufu wake Mbinguni.

Kwa shukrani kwa Bwana, kwa zawadi nyingi alizotupatia wakati wa upapa wake, ninawaalika tumwombee kwa Bwana.

Niombeeni! Heri ya Mwaka Mpya 2023!


Benedict XVI akiwa na familia katika utume wakati wa hadhira kwa ndugu wa Njia.
Share: