“Yesu wangu, nipeleke kwenye utakatifu wako”; “Wewe unaniongoza kwenye utakatifu”

(“Kitabu cha kumbukumbu 1979-1981”, na. 85; na.199)

Tarehe Desemba 4, 2022, “Tukio” lenye nguvu na maana maalum kwa Kanisa zima lilitukia huko Madrid: ufunguzi wa hatua ya kijimbo ya Kutangazwa Mwenye Heri na Kutangazwa Mtakatifu kwa Carmen Hernández Barrera, mwanzilishi mwenza, pamoja na Kiko Argüello, wa njia hiyo ya uanzishwaji wa kikristo inayoitwa Njia ya Neokatekumenato.


Ufunguzi wa mchakato

Katika mazingira rasmi ya Chuo Kikuu cha Francisco de Vitoria cha Madrid, mbele ya Kardinali Carlos Osoro, Makardinali 2 na Maaskofu 41 na angalau watu elfu mbili kutoka nchi mbali mbali za Ulaya na Ulimwenguni kote- utume uliotekelezwa na Carmen na Kiko unajumuisha nchi 135 kwenye mabara yote 5 na wengi wameomba kuweza kushiriki katika uzinduzi huu adhimu- Tukio rasmi la Jimbo la Madrid lilifanyika.

Lilifanyika katika sehemu nne: kwanza, salamu na maneno machache ya utangulizi kutoka kwa Kiko Argüello, pamoja na sala na somo la Injili (Mk 9:2-8), kifungu cha Kugeuka Sura kwake Bwana. – kifungu ambacho kilipendwa sana na Carmen; sehemu ya pili, kikao cha ufunguzi wa Mchakato, “Supplex libellus” likisomwa, yaani, ombi lililotolewa na mwombaji, kwa niaba ya kikundi cha kimataifa cha Njia, ili Jimbo lianzishe mchakato huu; vile vile, “Nihil obstat” (“Hakuna Pingamizi”) ikasomwa, kutoka Idara ya Kiti kitakatifu inayohusika na Michakato ya Watakatifu ili kuanzisha mchakato huo, ikifuatiwa na kumwita Roho Mtakatifu, ili asindikize kazi hii yote. Pia zilifuatwa na kiapo cha Askofu Mkuu wa Madrid aliyekubali ombi lililotungwa, pamoja na uteuzi wa mahakama ya kijimbo itakayoshughulikia mchakato mzima. Waliapa, mmoja baada ya mwingine, mjumbe wa maaskofu, mtetezi wa haki, mthibitishaji (na naibu wake) na mwombaji wa Mchakato. Sehemu hii ilihitimishwa na somo la “Matendo ya kikao” na Kansela- Katibu na tamko la Kardinali Osoro.

Katika sehemu ya tatu ya Tendo hili, Okestra ya kisimfonia ya Njia ya Neokatekumenato ilitoa zawadi mbili, mashairi mawili ya kisimfonia yaliyotungwa na Kiko: “Akedah” na “Binti za Yerusalemu”. Ya kwanza, “Akedah” , inawasilisha sadaka ambayo Abrahamu aliitwa kufanya, juu ya Mlima Moria, ya mwanawe Isaka, na huyu ambaye kwa hiari anatoa shingo yake ili sadaka isibatilishwe: hivi ndivyo imani inavyoonekana duniani; ya pili, “Binti za Yerusalemu”, ni wakati wa mkutano alio nao Yesu, akibeba msalaba, na wanawake wanaomlilia; Bwana anawaambia: “Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu…, kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?” (Lk 23:28.31). Ni mashairi mawili yaliyojaa hisia kali na mvuto wa muziki.

Kwa maneno machache ya mwisho, na salamu ya Askofu Mkuu wa Madrid, Tukio lilihitimishwa.


Salamu ya Kiko

Twadhani ni muhimu kuwaletea salamu ambayo Kiko alitoa mwanzoni mwa mkutano kwa wale waliohudhuria: baada ya kuwasalimu Makardinali na Maaskofu waliokuwepo, wana mamlaka zwa kitaaluma, Wakuu wa Shirika la Wamisionari wa Kristo Yesu, ambamo Carmen alikuwepo kwa miaka minane hivi, na wengine wote waliohudhuria (makatekista wasafiri, magombera wa Seminari za Redemptoris Mater na ndugu kutoka jumuiya zilizoanzishwa na Kiko na Carmen zaidi ya miaka 50 iliyopita), Kiko alisoma barua iliyotumwa kwa ajili ya tukio hilo na Kardinali Farrell, Mkuu wa Idara ya Walei, Familia na Uhai, na alitoa maoni yake kuhusu ufunguzi huu wa Mchakato wa Carmen Kutangazwa Mwenye Heri kwa maneno haya:

Mimi binafsi nimefurahi sana kwamba siku hii imewadia ambapo Kanisa linaanza awamu ya kijimbo ya Mchakato wa Kutangazwa Mwenye Heri na Mtakatifu kwa Carmen Hernández. Namshukuru Mwadhama Kardinali, Askofu Mkuu wa Madrid, Carlos Osoro, kwa kuanzisha uchunguzi kuhusu maisha, fadhila na sifa za utakatifu zake Carmen.

Bwana ametuunganisha, mimi na Carmen, kwa miaka 52, katika utume wa uinjilishaji wa ajabu -ulioanza katika jimbo hili la Madrid-, kama tunda la Mtaguso.

Ninalihisi kama tukio la upaji wa kimungu, kwamba ufunguzi wa Mchakato umeingiliana na mwaka tunapoadhimisha kumbukumbu ya miaka 60 ya kuanzishwa kwa Mtaguso wa Pili wa Vatikano; kwa sababu Carmen alitoa maisha yake ili kuuleta Mtaguso katika parokia, kupitia Uingizwaji wa Kikristo, kama huduma kwa maaskofu, na ambao unaitwa Njia ya Neokatekumenato.

Inashangaza kuona historia hii yenye matukio na watu halisi; kazi isiyofanyika ofisini juu ya meza, bali kwa utendaji wa Roho Mtakatifu. Yale yaliyokuwa yanafafanuliwa na kuandikwa kwenye Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano, sisi tuliyaona yakitendeka na maskini wa vibandani huko Palomeras kwa kazi ya Roho Mtakatifu. Tumemwona Bwana hapo akitokea na kuumba msamaha, upendo, ushirika, jumuiya ya Kikristo! Carmen, kama mimi vile vile, tumekuwa mashahidi wa uwepo wa Mungu katika uinjilishaji, mashahidi wa utendaji wa Mungu katika Kanisa la Mtaguso wa Pili wa Vatikano. Hatukuwa na mipango au mawazo yetu wenyewe. Kwa zaidi ya miaka 50 tumeweza kushuhudia kwamba Mungu yu hai katika Kanisa lake.

Carmen Hernández na Kiko Argüello, Ufilipino 2003

Carmen, akifuata nyayo za Mtakatifu Francis Xavier (sherehe yake tuliadhimisha jana), hakuwahi kufikiria kubaki Hispania, kwani ilikuwa kwake kama kushindwa katika lengo lake la kimisionari. Lakini Mungu alitaka tukutane huko Madrid, vibandani Palomeras Altas. Tulifahamiana mwaka 1964, baada ya yeye kurudi kutoka hija yake ya kihistoria katika Nchi Takatifu. Mimi nilikuwa nimeenda kuishi kwenye kibanda fulani pamoja na maskini wa Palomeras.

Huko Carmen alifahamu jumuiya ya ndugu waliokutana katika kibanda changu na alivutiwa sana na jibu walilolitoa kwa Neno la Mungu. Aliamua kukaa na kuishi nasi, tukamjengea kibanda.

Carmen aliona uwepo wa Yesu Kristo, anayekuja kuwaokoa wenye dhambi, kutekeleza fumbo la Pasaka na kuunda ushirika kati ya maskini: Yesu Kristo alijitoa kama upendo bure kwa watu wote.

Haya yote ambayo Mungu aliruhusu, uwepo wake huko Palomeras, ulikuwa kama udongo ambao Mungu alikuwa ametayarisha ili kuutia ndani ya Kanisa. Kile ambacho Mungu alituonjesha katikati ya ulimwengu fukara, Roho Mtakatifu alikuwa amekitayarisha kwa ajili ya Kanisa lake.

Uwepo kwa bahati ya Mungu wa Askofu Mkuu wa Madrid huko vibandani ndio uliyomfanya Carmen kuamua kushirikiana nami kwa hakika. Isingalikuwa kwa Mhashamu. Casimiro Morcillo, tusingalienda kwenye parokia. Pia ni yeye aliyetufungulia milango huko Italia. Carmen aliona uwepo wa Kanisa katika askofu mkuu na alibadili kabisa msimamo wake juu yangu. Kwa uwepo wa Morcillo, aliiona ahadi ambayo Mungu alikuwa amempa huko Israeli kutimia.

Wakati Carmen alipokuwa Israeli, mara kwa mara alijiuliza utume wake ulikuwa upi katika Kanisa, akafikiri kwamba alipaswa kuunda shirika la wamisionari. Huko Ein Karem alipata uhakika kamili, kama maono, kwamba Mungu alitaka kitu kutoka kwake kwa ajili ya Kanisa zima, kwamba halikuwa suala la kuanzisha shirika.

Ninawaambia haya ili mpate kuona, kama fumbo kuu la Bwana, ushirikiano kati yangu na Carmen.

Ilikuwa vigumu sana kwangu kumkubali Carmen, hadi Bwana aliponiambia kwa ndani kwamba Carmen alikuwa neema kubwa sana, yaani, kuwa na mtu karibu nami ambaye aliniambia daima, kwamba Mungu alikuwa amemleta kwa ajili ya utume fulani. Kwa hivyo, nilimkubali Carmen katika imani kama aliyetumwa na Bwana. Niliteseka mpaka nilipogundua kwamba yeye alitoka kwa Mungu, na tangu siku hiyo alikuwa neema kwangu.

Carmen amekuwa mzuri ajabu! Mwanamke wa ajabu ambaye amefanya mema mengi, si tu kwa ajili ya ndugu wa Njia ya Neokatekumenato, bali kwa Kanisa zima.

Carmen, mwanamke mzuri kama nini! Mwenye kipaji kikubwa fundishi cha uhuru na upendo kwa Kanisa. Hakuwahi kamwe kunisifu, daima aliniambia ukweli. Alifanikiwa kuwa daima nyuma yangu; daima kando yangu, ili kunisaidia. Hakutafuta nafasi ya kwanza, hakutafuta kamwe umaarufu. Alijua wazi kwamba utume ambao Mungu alikuwa amempa ulikuwa kuniunga mkono, kunitetea na kunirekebisha, kwa manufaa ya Njia ya Neokatekumenato.

Kwa upendo kwa Kanisa na ndugu, amebaki nami kwa miaka 52, ingawa wakati mwingine ilikuwa vigumu kwake, lakini Carmen alijali tu kufanya mapenzi ya Mungu, ambayo aliona ilikuwa kukaa pamoja nami katika Uingizwaji huu wa Kikristo ambao ni Njia ya Neokatekumenato.

Mwanamke wa kipekee, kwa kweli, mwenye ukarimu mkubwa sana, alijikana mwenyewe ili mimi nionekane, pamoja na kunisahihisha, lakini alikuwa nyuma yangu kila wakati, akinitegemeza.

Yeye ni kielelezo katika ukarimu, katika unyofu, katika kusema kwa uhuru na watu wote; aliwaambia ukweli ndugu wa jumuiya. Na wakati ndugu mmoja alipoenda mbali, alimpigia simu na kumtafuta, kama kondoo aliyepotea, kwa upendo.

Alikuwa mwanamke wa ajabu, nabii wa kweli, mtume wa kweli, ambaye aliishi imani yake kwa kiwango cha kishujaa. Mwanamke wa kipekee! Muhimu sana kwa Kanisa, daima katika sala, katika kushikwa upendo na Kristo, Maandiko Matakatifu na Pasaka, na kwa upendo bila masharti kwa Papa na Kanisa.

Pamoja sisi ni waanzilishi wa karama ambayo Bwana amevuvia kwa msaada wa Kanisa lake. Maneno ya Baba Mtakatifu Fransisko katika kuadhimisha miaka hamsini ya Njia ya Neokatekumenato mwaka 2018, aliposema huko Tor Vergata, Roma: “Ninyi ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa”, yanathibitisha hamu ile aliyotamani Carmen zaidi: kwamba ionekane kuwa katika Njia ni Mungu anayetenda, kwamba ni kazi ya Roho Mtakatifu ndani ya Kanisa, ambayo Yeye mwenyewe ametuitia sisi kuwa waanzilishi wake.

Katika hadhira ya mwisho aliyotujalia mwaka huu kwa Kikundi cha Kimataifa cha Njia, Papa Fransisko alidhihirisha furaha yake kwa ufunguzi wa Mchakato.

Natamani kwamba Kanisa, katika Mchakato huu wa Kutangazwa Mtakatifu unaoanza, lichunguze maisha yake, ambayo mara nyingi yalikuwa maisha ya kusulubiwa, katika ukimya na mateso, kana kwamba “kwenye usiku wa vivuli”; Pia nataka kwamba fadhila zake zidhihirike, nyingi zikiwa zimefichika, nyingi kwa kiwango cha kishujaa. Kanisa lipambanue juu ya hayo.

Ninamshukuru Mungu kwa kuweza kumfahamu na kuweza kufanya kazi pamoja naye katika “kazi ngumu za Injili”! kama asemavyo Mtakatifu Paulo.

Carmen! mwanamke mkuu, mwenye imani ya kipekee! Upendo gani mkuu ambao amekuwa nao kwa Kristo na Kanisa lake!

Asanteni.

Sasa tusikilize Injili.

Jioni hii tungependa kuwasilisha kifungu cha Injili ambacho kilimgusa sana Carmen: Kugeuka Sura, ambayo ndiyo hatima ya ajabu na ya kushangaza katika historia ya mwanadamu, na ambayo imekwisha kukamilishwa na Bikira Maria, aliye sura, siyo tu ya Kanisa, bali pia ya ubinadamu wote.

Kugeuka Sura kwa Bwana kutamwongoza mwanadamu huyu aliyechukuliwa na Yesu Kristo hadi umunguisho kamili. Ni kuinuliwa hadi utukufu wa mbinguni, hadi Kupaa. Na hilo linaweza kuonjwa hapa, kwa sababu wakristo, kupitia ubatizo, tunageuzwa siku hadi siku; hata ikiwa mwili huu unachakaa, tunageuzwa kuwa sura ya Yesu Kristo. Hii ndiyo imani ya Kikristo inayozaa historia, kesho ya ubinadamu: Kugeuka Sura.

Tangazo la Injili: Mk 9:2-8.


Utakatifu wa Carmen leo

Picha na “archimadrid.es” – Luis Millán

Kusema juu ya “utakatifu” katika ulimwengu wa leo, hata ndani ya Kanisa lenyewe, kunaweza kuonekana sio muhimu, kwamba ni mambo ya mtu binafsi, ambayo hayana uhusiano wowote na matatizo halisi … Lakini je, ni hivyo kweli?

Utakatifu, kabla ya kuwa kitu kinachotuhusu sisi, ni kilio chenye shauku cha Mungu: “Kuweni watakatifu, kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu” (Law 19:2), “… kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi kuweni watakatifu… Kwa maana imeandikwa, ‘Kuweni watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu’” (1 Pet 1:16). Kuzumgumza juu ya utakatifu, kwa yule aaminiye, ni kumdhihirishia Yule Aliye Mtakatifu, Mungu, ni kudhihirisha kutenda kwake, utukufu wake unaotafuta na kutamani uzima wa mwanadamu: “Utukufu wa Mungu ni mtu anayeishi,” anasema kwa mshangao Mt. Ireneo. [1]

Na kusema juu ya utakatifu wa Carmen ni, juu ya yote, kudhihirisha utendaji wa Mungu ndani yake, kuzungumza juu ya yale ambayo historia yake na maisha yake yamemaanisha na ipi tabia yake. Inastaajibsha sana kufungua “Vitabu vyake vya kumbukumbu” na kufuatilia mawazo yake, mateso yake, sala yake, roho yake:

Siku ambayo mnamo 1979 Papa Mtakatifu Yohane Paulo II aliwatangaza wenye heri wawili kuwa watakatifu, aliandika katika kitabu chake cha kumbukumbu:

Maskini na bila kitu, hamu ya ndani ya uwepo wako wa kipekee inanijia. Utakatifu, Bwana, tamaa zilizofichwa za utakatifu, za kujitoa, kuijaza siku na uwepo wako. Sala. Bwana, njoo Wewe Uujaze wema na vitu na maana …” (“Kumbukumbu 1979-1981″, na. 77, Aprili 29, 1979).

Ee Yesu, jiwe la msingi, uzima usiotikisika uliojengwa juu ya Msalaba. Njoo, Yesu, uangazie uso wako juu ya maisha yangu. Nisaidie kuegemeza utu wangu katika Wewe. Yesu wangu, nipeleke kwa sala, kwa utakatifu wako, kimbilio langu, uzima wangu. Njoo, Roho Mtakatifu sana, uwe na huruma kwa utu wangu maskini” (“Kumbukumbu 1979-1981”, na. 85, May 8, 1979).

Utakatifu kwa Carmen ni, zaidi ya yote, ungamo la imani katika Yesu huyo ampendaye: “Mwororo kupitiliza, mtakatifu, mtukufu” (“Shajara 1979-1981”, na. 780, Desemba 15, 1981); katika uaminifu wake: “…nautumainia UPENDO wako, wewe ni mwaminifu na MTAKATIFU, Uhimidiwe, ee Yesu, huruma zako zinifikie, nami nitaishi” [2]; 366. “Usiruhusu miguu yangu itikisike. Unilinde. Wewe, Mwaminifu, Mtakatifu, Yesu wangu (“Kumbukumbu 1979-1981”, na. 366, Septemba 4, 1980); katika kujiruhusu kusulubiwa kwa upendo: “Wewe ni Mtakatifu, bila mipaka, mwororo sana. Na umesulubiwa kwa upendo kwangu”(“Kumbukumbu 1979 -1981”, na. 231, Aprili 1, 1980). Carmen anatafuta kwa shauku: “Yesu wangu, Mtakatifu pekee, Uliye wa Pekee, uko wapi?” (“Kumbukumbu 1979-1981”, na. 267, Mei 15, 1980); Anamsikia kweli kama mkombozi wake: “Wewe, mkombozi, mtakatifu, wa ajabu, mwanga, uzima, ufufuko wa wafu, mwenye haki na aliyesulubiwa”(“Kumbukumbu 1979-1981”, na. 187, Februari 16, 1980); Yeye ndiye ambaye kwa jina lake anapigana vita vyote: “Katika jina lako, Yesu, Yesu, ninapigana vita vyote. Wewe ndiwe. Jina lako takatifu. Njoo Yesu” (“Kumbukumbu. 1979-1981”, na. 299, Juni 23, 1980).

Mchakato huu uliofunguliwa leo na Askofu Mkuu wake, Kardinali Carlos Osoro, katika Jimbo kuu la Madrid, umeteua Mahakama ya Jimbo itakayosimamia utakatifu huo wa Carmen, kwa kuandikisha ushuhuda na hati, ambavyo baadaye vitapelekwa Roma ili kupata azimio rasmi, wakati yote yatakapokuwa tayari.


Baadhi ya habari kuhusu Njia ya Neokatekumenato (30/11/2022)

Jumuiya: 21,066

Majimbo: 1.366

Parokia: 6.293

Mataifa: 135

Seminari za “Redemptoris Mater” (SRM): 121

Waseminari katika SRM: 1.900

Mapadre waliopata malezi katika SRM: 2.950

Familia katika utume: zaidi ya 2.000, zikiwa na watoto takriban 6.500

Familia 1.000 zinainjilisha kwenye Missio ad Gentes 212 katika mataifa 62, wakisindikizwa na padre na baadhi ya dada.

Familia 800 ziko kwenye nchi mbali mbali ili kuimarisha jumuiya mahalia mbali mbali, wakiwategemeza katika safari yao ya imani.

Familia hizo zipo zaidi ya 300, zinazounda, pamoja na padre na kijana, kikundi cha uinjilishaji, kinachowajibikia taifa zima au maeneo mbali mbali.


[1] Mt. Ireneo, Adv. haereses  (“Dhidi ya Uzushi”), IV, 20,7.

[2] Hati za Carmen Hernández, Vol. 32, maandiko yake ya 21/10/1970.

Share: