Kiko Argüello

Baba Mpendwa:

Asante kwa uwepo wako, asante kwa kukubali kutuma familia hizi katika utume.

Njia ya Neokatekumenato hadhira pamoja na Papa Fransisko Kiko Argüello Pd. Mario na María Ascensión

Tunawasalimu Kardinali Kevin Farrell, Maaskofu wakuu na Maaskofu waliopo, na pia washiriki kutoka Idara ya Walei, Familia na Uhai, ambao wamekubali kushiriki tukio hili pamoja nasi.

Baba Mtakatifu, kabla hatujaanza, tunataka kukushirikisha habari ambayo tunajua itakufurahisha: Jimbo kuu la Madrid limetufahamisha kwamba mchakato wa kutangazwa kuwa mwenye heri na wa kuwa mtakatifu wa Carmen Hernández utafunguliwa rasmi hivi karibuni. Makofi kwa Carmen!

Kwanza kabisa, nataka kutambulisha familia katika utume huko Ukraine ambao, mwanzoni mwa vita, kwa mateso makubwa, walilazimika kuacha taifa, lakini ambao wanatamani kurudi, kwa muujiza wa neema ya Mungu. Wanasema: Vipi tusirudi ikiwa tumewaacha huko ndugu wengi, watu wengi wanaotuhitaji? Simameni, familia mliopo huko Ukraine.

Sasa tunazitambulisha familia misionari:

Simameni familia katika utume katika mataifa ambayo sasa nitataja: Urusi, Latvia, Lithuania, Estonia, Romania, Bulgaria, Hungary, Austria, Ujerumani, Ufaransa, Uswidi, Norway, Iceland, Uingereza, Ireland, Italia, Kipro, Ugiriki , Hispania, Ureno, Uturuki, Albania, Serbia, Montenegro, Kroatia na Moldova. Makofi kwa hizi zote zinazokwenda Ulaya.

Sasa tunatambulisha familia zitakazoenda Asia: Kazakhstan, Mongolia, Japan, Korea Kusini, Taiwan, Kambodia, Laos. Makofi.

Kwa Amerika: Kanada, Marekani, Meksiko, Puerto Rico, Jamaika, Chile, Ekuador (Amazon), na Argentina. Makofi.

Kwa Afrika: Misri, Tunisia, Ethiopia, Sudan, Kenya, Camerun, Uganda, Gabon, Guinea ya Ikweta, Cape Verde, Ivory Coast na Afrika Kusini. Makofi.

Kwa Australia na Oshenia. Makofi.

Tunawatambulisha Makatekista Wasafiri Wawajibikaji wa Njia ya Neokatekumenato katika mataifa 134. Makofi!

Mapadre wengine mliopo hapa.

Waseminari kutoka seminari za Redemptoris Mater.

Na hatimaye, ndugu wengi sana kutoka jumuiya za neokatekumenato kutoka Roma.

Baba Mtakatifu, ni tukio zuri ajabu ambalo tutaishi hapa leo. Katika kizazi hiki Mungu anawaita familia, kwa sura ya Familia Takatifu ya Nazareti, kupeleka furaha ya upendo wa Mungu kwa watu ambao hawamjui bado.

Ni Familia 430 ambazo zinasubiri kuthibitishwa na kutumwa Nawe, ili wakijaa Roho Mtakatifu wapate kuondoka ili kuwa mashahidi wa upendo na uwezo wa Kristo Mfufuka. Asante, Baba Mtakatifu, kwa kuwa hapa nasi.

Familia hizi zinahitaji kuthibitishwa na Petro. Mbele ya magumu mengi watakayokutana nayo na dhiki zitakazofika, uwepo wa Papa utakuwa kwao faraja, msaada mkubwa na ulinzi.

Njia ya Neokatekumenato ni tunda la Mtaguso wa Vatikano II, kama alivyotambua kutoka mianzo yake Mtakatifu Paulo VI. Safari hii ya uingizwaji wa kikristo unawapeleka watu kwa imani pevu, kupitia kugundua upya utajiri wa ubatizo wetu.

Mbele ya tukio la uduniaisho, la ukanamungu na la ukengeufu wa maadili, utamaduni na falsafa, bila shaka ni ajabu zuri sana kwamba Bwana ameamsha familia nzima, pamoja na watoto wao, ili kuondoka na kuhamia kwenye maeneo yaliyojaa uduniaisho na umaskini zaidi ili kupeleka tangazo la Yesu Kristo.

Kristo amefufuka! Hii ndiyo sababu ya ndugu hawa kuacha nyumba yao, ndugu, marafiki, nchi yao yenyewe na kwenda kuinjilisha, kwa sababu Kristo amewajalia kushiriki ushindi wake juu ya dhambi na juu ya mauti na wanaweza kutoa maisha yao kwa ajili ya wengine.

Tunakumbuka kwa shukrani maneno uliyotuambia mara ya mwisho tulipokutana, tarehe 4 Mei 2018, huko Tor Vergata, kwa kuadhimisha miaka 50 ya Njia: “Ninyi ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa”. Kwa hiyo, kabla ya kusikiliza Injili, tunataka kumwita Roho Mtakatifu ili asaidie familia zinazotoka sasa na familia zilizo tayari katika utume. Tuombe kwa ajili yao Roho Mtakatifu, pamoja na vipaji vyake, ili waweze kuwa na subira katika mateso na wapate pumziko la kweli katika Msalaba wa Kristo. Sote tunamhitaji Roho Mtakatifu, kwa sababu bila Yeye hakuna lililo safi wala takatifu ndani yetu. Tuimbe tenzi kwa Roho Mtakatifu.


Papa Fransisko

Asubuhi hii, 27 Juni 2022, katika Ukumbi wa Paulo VI, Baba Mtakatifu Fransisko amepokea katika Hadhira Familia za Njia ya Neokatekumenato zilizotumwa kwenye utume na amewaambia maneno yafuatayo:

Hotuba ya Baba Mtakatifu

Tumesikia utume wa Yesu: “Nendeni, toeni ushuhuda, hubirini Injili”. Kutoka siku hiyo mitume, wanafunzi, watu wote walisonga mbele kwa nguvu hiyo hiyo aliyowapa Yesu: ni nguvu inayotoka kwa Roho. “Nendeni na kuhubiri… Mbatize”.

Lakini tunajua kwamba, tukiisha batiza, jumuiya inayozaliwa kutoka Ubatizo huo ni huru, ni Kanisa jipya; sisi tunapaswa kuiruhusu kukua, kuisaidia kukua kwa namna zake zenyewe, utamaduni wake mwenyewe… Hii ndiyo historia ya uinjilishaji. Sote tuko sawa kwa yanayohusu imani: nasadiki kwa Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, katika Mwana aliyepata mwili, kufa na kufufuka kwa ajili yetu, katika Roho Mtakatifu anayetusiadia na kutufanya tukue: imani hiyo hiyo. Lakini kila mtu kwa namna ya utamaduni wake mwenyewe ama utamaduni wa mahali alipohubiriwa imani.

Kazi hii, utajiri huu wa tamaduni nyingi wa Injili, unaozaliwa na mahubiri ya Yesu Kristo na unageuka kuwa utamaduni, ni, kwa namna fulani, historia ya Kanisa: tamaduni nyingi lakini Injili hiyo hiyo. Mataifa mengi, Yesu Kristo yule yule. Mapenzi mengi mema, Roho huyo huyo. Na kwayo tumeitwa: kusonga mbele kwa nguvu za Roho, tukibeba Injili moyoni na mikononi. Injili ya Yesu Kristo, siyo ile yangu:

Roho hii ya kimisionari, yaani, kujiruhusu kutumwa, ni uvuvio kwenu nyote. Nawashukuru kwa hayo, na ninawaomba usikivu kwa Roho anayewatuma, usikivu na utii kwa Yesu Kristo katika Kanisa lake. Yote katika Kanisa, hakuna kitu nje ya Kanisa. Hii ndiyo tasaufi inayotakiwa kutusindikiza daima: kumhubiri Yesu Kristo kwa nguvu za Roho katikaKanisa na pamoja na Kanisa. Na yeye aliye kichwa -tuseme- cha Makanisa mbalimbali ni askofu: songeni mbele daima na askofu, daima. Yeye ndiye kichwa cha Kanisa, katia Nchi hii, katika Jimbo hili…

Songeni mbele! Jipeni moyo! Asante kwa ukarimu wenu. Msisahau mtazamo wa Yesu, aliyewatuma kila mmoja wenu kuhubiri na kulitii Kanisa. Asanteni sana!

Njia ya Neokatekumenato hadhira pamoja na Papa Fransisko kutumwa familia kwenye utume.
Share: