Wenye shukrani kwa Mungu kwa huduma yake ya thamani katika Kanisa
Alfajiri ya leo (tarehe 15 Machi, 2024) Bwana amemwita Kardinali Paul Josef Cordes kwa zawadi ya uzima wa milele. Kanisa zima, na hasa Njia ya Neokatekumenato, linamshukuru sana kwa kazi aliyoifanya kwa miaka mingi ya maisha yake, akisindikiza, kupitia ushauri wake wenye busara, kuzaliwa, kukua na kuingizwa polepole ndani ya Kanisa kwa vyama na mikondo mingi sana ya kikanisa, ambayo baada ya Mtaguso imesitawi, huko akitekeleza huduma yake kama Makamu wa Raisi wa Idara ya Kipapa kwa ajili ya Walei (1980-1995).
Tayari mnamo 1986 (tarehe 21 Oktoba, kupitia barua ya Katibu wa Jimbo, Kardinali Casaroli), na kwa matakwa ya Papa Yohane Paulo II, ambaye alitaka kuhamasisha uingizwaji bora wa Jumuiya za Neokatekumenato katika Kanisa, pamoja na ufafanuzi uliohitajika wa kitambulisho chake cha kisheria na cha kikanisa, Mons. Cordes aliagizwa kuitekeleza. Mnamo 1990, Mtakatifu Yohane Paulo II alimwandikia Mons. Cordes barua ya “Ogniqualvolta“, kama msimamizi “ad personam” (“katika nafsi yake”) kwa ajili ya Utume wa Jumuiya za Neokatekumenato. Katika barua hiyo Njia ilitambuliwa “kama mwendo wa malezi ya Kikatoliki, ufaao kwa jamii na nyakati za leo”, na humo pia Papa alitamani kazi hiyo ya uinjilishaji mpya ithaminiwe na kusaidiwa na Wachungaji .
Mons. Cordes daima amekuwa na umakini na upendo wa pekee kwa waanzilishi wa Njia, Kiko Argüello na Carmen Hernández, na amewaunga mkono na kuwatia moyo katika njia yao ya ukuaji, katika vipindi vyote vya historia yao, akiwasaidia na kusindikiza hatua mbalimbali zilizoipeleka Njia ya Neokatekumenato kuidhinishwa “kama namna ya kijimbo ya uingizwaji wa kikristo na ya malezi ya kudumu ya imani” (Statuta, n. 1,2) na kutambuliwa kutoka Idara ya Mafundisho ya Imani, maandiko yote ya katekesi kama “Mwongozo wa Katekesi”.
Katika miaka hii mirefu ya historia, katika njia hii yote, Kardinali Cordes si amekuwa mtu wa karibu tu, bali pia rafiki na msaada ufaao kwa Waanzilishi na kwa Jumuiya zote za Neokatekumenato, zilizo na deni kubwa kwa kazi yake, na vile vile Wachungaji wengi aliowahimiza kusaidia na kuipatia nguvu kazi hii kwa manufaa ya Kanisa.
Kwa namna ya pekee, tunakumbuka uchapishaji wa kitabu chake: “Kushiriki kikamilifu katika Ekaristi. ‘Actuosa participatio’ katika jumuiya ndogo” katika kulinda Ekaristi iliyoadhimishwa katika jumuiya ndogo, ambayo walitetea sana Kiko na Carmen.
Tunayo furaha ya kukumbuka hapa yale ambayo Papa Benedikto XVI mwenyewe alimwandikia katika barua wakati wa kuadhimisha miaka 75 ya kuzaliwa kwake:
“Kwa ujasiri na ubunifu, mwanzoni mwa utendaji wako hapa Roma umefungua njia mpya za kuwaongoza vijana kwa Kristo… Umechangia pia katika kuanzisha na kukuza Siku za Vijana Duniani (SViD). Tabia yako haswa ya msukumo wako wa kichungaji imekuwa na imebakia kuwa kujitolea kwako kwa “mikondo”: Mkondo wa Wakarismatiki, Ushirika na Ukombozi (“Comunione e Liberazione”), na Njia ya Neokatekumenato zina sababu nyingi za kuwa na shukrani kwako. Ingawa waandaaji na wapangaji wa Kanisa mwanzoni walikuwa na mashaka mengi kuhusu mikondo hii, wewe mara moja umehisi uzima uliokuwa ukijitokeza pale: nguvu ya Roho Mtakatifu inayofungua njia mpya na kwa njia isiyotabirika hulidumisha Kanisa kijana daima. Umetambua tabia ya kipentekoste ya mikondo hii na umejitolea kwa moyo mkuu kuhakikisha kwamba inakaribishwa na wachungaji wa Kanisa.”
Tunaikabidhi kwa maombi ya ndugu wote ukumbusho huu wa shukrani wa Kardinali Cordes ili wamwombe Bwana amkaribishe huyu “mtumishi mwema na mwaminifu” katika Ufalme wake (Mt 25,21).