«WAKATI MAWE YANAONGEA TENA»
Oktoba 12 iliyopita (2022), sikukuu ya Bikira wa Pilar (Bikira wa Nguzo)- siku ambayo Hispania inaadhimisha kwa taadhima, kutokea kwake Bikira Mama wa Mungu kwa mtume Santiago na wenzake katika mwaka wa 40 BK kwenye nguzo ya marumaru kwenye ukingo wa mto Ebro, ili kuwatia moyo katika kuendelea na uinjilishaji – huko Fuentes de Carbonero el Mayor, kijiji kidogo karibu na Segovia kilichotelekezwa na watu tangu 1960, ilitukia sherehe yenye kwa kweli maana ya pekee mno.
Ekaristi iliongozwa na Askofu wa Segovia, Mhashamu Mons. Askofu César Franco, akisindikizwa na mapadre zaidi ya thelathini na wakiwepo kama watu 500 waliojaza kanisa hilo na eneo linalozunguka. Pia alikuwepo mkuu wa mkoa wa Segovia, Miguel Ángel de Vicente, na meya wa Carbonero el Mayor, María Ángeles Sanz, pamoja na mamlaka nyingine na wawakilishi wa Njia ya Neokatekumenato wa kaskazini-magharibi mwa Hispania na ndugu wengi kutoka jumuiya mbalimbali za neokatekumenato wa eneo hilo. Kushiriki kwa wakaaji wengi wa Carbonero, au wa watoto wa familia za asili ya pale Fuentes, kabla ya nyumba za kijiji hiki kidogo kutelekezwa na kugeuka magofu, kuligusa sana.
Licha ya kanisa dogo ambalo sasa limekarabatiwa kikamilifu kutokana na juhudi na kazi zilizotekelezwa na Njia, eneo hilo limezungukwa na mashamba. Kwa mbali zinaonekana kuta zilizoharibika za baadhi ya nyumba za zamani za mashambani, pamoja na chemchemi ndogo chini ya mteremko, na pia shamba moja upande wa pili wa shimo.
Ni nini cha upekee kuhusu mahali hapa? Kwa nini kanisa limejengwa upya mahali palipoachwa na watu na ambalo lingefikiriwa pia kutelekezwa na mkono wa Mungu?
Hayo yalikumbukwa kabla ya Ekaristi na Don Antonio Riquelme, padre wa kikundi cha Njia kinachohusika na eneo hili, ambaye alisoma ujumbe uliotumwa na Kiko Argüello, aliye mwanzilishi pamoja na Carmen Hernández wa Njia ya Neokatekumenato, na ambaye hakuweza kuwepo kwenye tukio hilo, lakini ambaye historia yake imeambatanishwa na mahali hapa na hiyo ndiyo sababu ya ukarabati wa jengo hili.
Tumruhusu Kiko aongee:
Ninamshukuru Mungu ambaye ameruhusu kujengwa upya kwa kanisa hili dogo, ambalo lilikuwa muhimu sana hivi kwangu. Namshukuru Askofu kwa uwepo wake na wote waliowezesha ukarabati wa hekalu hili.
Njia ya Neokatekumenato ni Uingizwaji wa Kikristo ulioidhinishwa rasmi na Kiti Kitakatifu (Holy See) mwaka 2008. Bwana alitutumia Carmen na mimi kwa kufanya upya Kanisa lililozaliwa baada ya Mtaguso wa Pili wa Vatikani. Ilianza mwaka wa 1964 kati ya wakaaji wa vibandani mwa Palomeras Altas huko Madrid, wakati maskini tulioishi nao walipotuomba tuwatangazie Injili ya Yesu Kristo. Ufunguzi wa mchakato wa Kutangazwa Mwenye Heri wa Carmen Hernández tarehe 4 Desemba utakuwa furaha kuu kwa Njia nzima na kwa Kanisa.
Mungu ametaka kwamba, katika mwaka wa 1965, nikitamani kupata mahali pa mafungo na sala, nilikuta kanisa la Fuentes de Carbonero likiwa limetelekezwa. Nilipokuwa nikitembea nyanda tambarare za Kastiya siku yenye mawingu, mwali wa jua uliangazia madini ya ulanga ambayo yalienea katika eneo hilo na ghafla kila kitu kiliangazwa na nilivutiwa kabisa: kanisa kwenye uwanda ule wazi lilikuwa ni tokeo halisi la kimungu. Lilikuwa wazi na tupu; bado lilikuwa na baadhi ya picha na sanamu nyuma ya altare; sakristia ilikuwa na jukwaa la mbao iliyonisaidia mimi kulala. Nilibaki nikiishi huko siku kumi na tano, nikisali peke yangu na kwa matunda makubwa. Kwa kuona kwamba palikuwa mahali pazuri ajabu, nilirudi hapo mara kadhaa, nikiishi peke yangu, katika kufunga na kusali, na nikilala na mfuko wangu wa kulalia katika sakristia.
Kwa kuwa mto fulani ulipita karibu na hapo, niliamua kuwachukua akina ndugu kutoka vibandani kwa siku chache wakati wa kiangazi ili na wao pia wapate likizo. Tuliishi wiki ya mapumziko, ushirika na upendo. Nilishangaa sana kwamba wakati nyumba zote katika kijiji hicho ziliharibika, kitu pekee kilichobaki kikisimama katika kijiji hicho kilichotelekezwa kilikuwa kanisa, na kanisa ambalo limejaa maskini. Niliwaambia ndugu wa vibandani waende kukusanya majani makavu. Walienda shambani na kila familia walijitayarishia vitanda vyao kwa majani haya na blanketi. Iligusa na kupendeza sana, mpaka ingefaa kwa ajili ya kutengeneza filamu. Nje, nyumba zote zilizobomoka; ndani, kanisa limejaa maskini.
Siku ya mwisho tulifanya misa na wote wa kijijini walioishi Carbonero walikuja. Wengine wanasema kwamba waliposikia sauti ya kengele walilia kwa furaha, kwa sababu walikuwa hawajasikia kengele zikigongwa kwa miaka mingi. Tuliadhimisha misa na walifika katika misa pamoja nasi. Walisisimka mno; walipata kusikia tena kengele za kijiji chao. Kanisa lilijaa. Tulilipamba kwa maua na kulitayarisha vizuri sana; lilipendeza sana.
Baada ya muda, Kerigma hii iliyotangaza kwa masikini ilibainishwa katika muhtasari wa katekesi unaosimama katika miguu mitatu ya “Neno la Mungu-Liturujia-Jumuiya” na ambao kusudi lake ni kuwaongoza watu kwenye ushirika wa kindugu na imani mpevu.
Njia hii mpya ya uangizwaji wa Kikristo iliamsha shauku ya Askofu Mkuu wa Madrid wa wakati huo, Monsinyori Casimiro Morcillo, ambaye alituhimiza kuipeleka kwenye parokia; hivyo ilienea katika Madrid na majimbo mengine ya Hispania. Mwaka wa 1968 Njia ilianza huko Roma na tangu wakati huo imeenea ulimwenguni kote.
Hapa tulisherehekea Mkesha wa Pasaka na ndugu wa vibandani na wale wa jumuiya ya kwanza ya Madrid. Hatukuwa na umeme; Tulijiangazia na nuru ya mshumaa mkubwa wa zamani tulioukuta. Kulipopambazuka tulikula mwana-kondoo tuliyekuwa tumeagiza huko Carbonero.
Vipi kutombariki Bwana, vipi kutomshukuru Bikira Maria ambaye alivuvia Njia ya Neokatekumenato na ambaye katika sikukuu ya Bikira wa Pilar anaturuhusu kulifungua tena! Leo hii unaadhimishwa uvumbuzi wa Amerika mnamo 1492. Bikira Maria wa Pilar, ambaye ni mtakatifu somo wa Amerika ya Kusini, nyota ya uinjilishaji wa bara hilo. Kutoka hapa waliondoka makatekista wasafiri wa kwanza wa Njia kwenda kuinjilisha Amerika, ambayo leo imejaa jumuiya.
Mniombee.
Baada ya kusomwa ushuhuda wa Kiko, baraka ya kanisa lililokarabatiwa na adhimisho la Ekaristi uilifuata. Askofu katika homilia yake alitaka pia kusisitiza kwamba, ukarabati wa mahali hapa ni “muujiza” wa Mungu anayetenda mambo makuu ndani yetu, akisisitiza umuhimu wa kielelezo wa ujenzi mpya wa kanisa, kwa kuwa ni ishara ya utume wa Kanisa wa kumtangaza Kristo. : “Jengo hili—alitia mkazo—linatoa mfano wa kile ambacho Kiko Argüello alitaka kufanya na pia ya yale ambacho Kanisa limefanya tangu asili yake, yaani, kuinjilisha, kufanya katekesi, kutuma ulimwenguni wale walio na imani ili kuuendeleza utume mkuu na wa kipekee wa Kristo” . Kisha alimtakia Kiko kwamba aendelee kuwa na “ujasiri ambao kwao amewahubiria watu wengi hivi kupitia Njia, Njia ambayo inazaa matunda mengi kwa Kanisa”. Haswa, kujengwa upya kwa kanisa hili ni “tunda lingine la Njia ya Neokatekumenato”.
Ndoto – Maono
Ushuhuda wa Kiko na baraka ya kanisa la Fuentes baada ya kazi ya kujengwa upya zinafanya kwamba, kutoka mahali hapa palipoachwa, kumbukumbu ya mwanzo wa baadhi ya matukio ambayo ni ya msingi kwa historia ya Njia, na ambayo asili yao imetukia hapa Fuentes vifike kwetu: mkesha wa Pasaka, ulioadhimishwa kufuatana na ugunduzi mpya wa Mtaguso wa Pili wa Vatikano, na pia namna hii ya utume kwa vikundi vya makatekista wasafiri.
Katika masimulizi/ushuhuda mwingine wa Kiko, aliongeza baadhi ya maelezo ambayo tunafikiri ni muhimu kukumbuka ili kukamilisha yale yaliyosemwa kabla. Katika safari yake ya imani, Kiko alihisi kwamba Kristo alikuwepo katika mateso ya “wale wa mwisho wa dunia”. Kwa kufuata nyayo za Mtakatifu Charles de Foucauld, mwaka 1964 aliamua kwenda kuishi na walio maskini zaidi, katika kibanda kimoja cha Palomeras Altas, pembezoni mwa Madrid, ambako alikutana na Carmen Hernández, na hivyo walianzisha aina mpya ya kuhubiri ambayo muda mfupi baadaye ilipelekea uundaji wa jumuiya ya kikristo.
Kiko anasimulia:
“Vibandani huko kulikuwa na Vicenta fulani (aliyejitoa kwenda kusaidia wale waliokuwa vibandani) na siku moja nilimwambia: “Angalia, kabla hujaja, hatujawahi kupigana, na tumekuwa na ushirika sikuzote; tangu umefika, hapa kuna fujo…”. Akakasirika, akaamua kuondoka. Alikuwa kutoka Segovia na hivyo siku moja nilifikiri kwenda kumtafuta ili kumwomba msamaha. Nilifika kijijini kwake, Carbonero el Mayor, na kwa kuwa sikuwa na anwani yake, nilimuulizia, wakaniambia alikuwa shambani.
Nilianza kutembea kwa utulivu kwenye nyanda za Kastiya, ambazo ni jangwa; nyanda hizo ni za ajabu, zinafanana na zile za Urusi. Siku hiyo ilikuwa na mawingu na ghafla mwali wa mwanga ulijifunua na uling’aa ukiishia huko Fuentes. Inanaonekana kwamba mawe ya mji huo ni ya madini ya ulanga, na yanang’ara; na ghafla kila kitu kilimulikwa na nikabaki nimevutiwa mno. Kanisa katikati ya mbuga hiyo lilikuwa kabisa kama tokeo halisi kutoka mbinguni…
Mwaka 1967 tuliadhimisha Mkesha wa Pasaka katika kanisa la Fuentes pamoja na ndugu kutoka Palomeras na wale wa parokia ya kwanza ya Madrid.
Mnamo 1969 nilimwambia Pd. Fransisko Cuppini – padri wa kwanza ambaye alitusindikiza Carmen na mimi- aje nami kuishi Juma Takatifu. Tulikwenda huko, wala hatukuwa na umeme, lakini kulikuwa na mshumaa mkubwa wa zamani na tuliuwasha. Tuliagiza mwana-kondoo kutoka kijiji jirani kwa ajili ya karamu ya Pasaka, alfajiri yake. Tulisherehekea Mkesha wa Pasaka bila umeme; Pd. Fransisko Cuppini aliuongoza.
Pia ilikuwa huko Fuentes ambapo Mkutano wa kwanza wa makatekista wasafiri ulifanyika na kutoka hapo vikundi vya kwanza kwa ajili ya Amerika waliondokea kwenda kuinjilisha.
Kiko alishangazwa sana na “mwali wa mwanga” ambao ulimulika mawe yale ya madini ya ulanga, ambayo yalileta sura mpya kwa eneo hilo lote, lenye kanisa lililotelekezwa. Sura hii inatukumbusha kanisa lingine, neno lingine na ndoto nyingine, kutoka maisha ya Mtakatifu Fransisko wa Asizi.
Katika maisha ya Mtakatifu Fransisko wa Asizi kuna mambo mawili yanayovutia sana na, tuseme, yapo karibu sana na sisi. Inasemekana kwamba akiwa karibu na kanisa la Mtakatifu Damiano, jengo dogo lililokuwa katika magofu, karibu na Asizi, aliingia kusali. Wakati wa kusali, macho yake yakiwa yameelekezwa kwenye Msalaba wa Bwana, alisikia sauti ikimwambia “Fransisko, nenda ukarabati kanisa langu ambalo, kama unavyoona, limekuwa gofu”. Mtakatifu Fransisko alianza mara moja kufanya kazi ya kukarabati kanisa, lakini mapema alielewa kwamba mwito wa Bwana ulikuwa ukielekea mbali zaidi. Katika “Masimulizi Makuu”, maisha ya Mtakatifu Fransisko yalivyoandikwa na Mtakatifu Bonaventura, inasimuliwa ndoto ya Baba Mtakatifu Inosenti III, ndoto ambayo imechorwa kwa namna ya ajabu na msanii, jina lake Giotto, ndani ya Basilika la Asizi. Katika ndoto hiyo, aliliona Basilika la Mtakatifu Yohane huko Laterano, Roma, ambalo lilikuwa linaelekea kuporomoka, na lilitegemezwa na mtawa wa kiume… Sote tunajua kazi ambayo Mungu amefanya katika Kanisa kupitia marekebisho ya kifransiskani, na si tu katika Kanisa la wakati huo, bali hata leo hii.
Kujengwa upya kwa Kanisa la Fuentes kunaleta ulinganifu wa kushangaza kati ya hali ya Kanisa katika karne hiyo ya 12 na hali ya leo hii. Kwa hakika, bila majigambo yoyote, tunajua kwamba ni historia mbili tofauti na ni matukio mawili tofauti: huko historia iliyothibitishwa, hapa bado ni “maono”, lakini inatosha kufungua macho yetu kidogo kuona jinsi Mungu anavyoongoza historia: Uingizwaji katika ukristo, ulioanzishwa na Kiko na Carmen, chini ya mwanga wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano na kwa kufuata nyayo zake. Uingizwaji huu uliofunguliwa katika nchi 135 kutoka mabara yote matano ni jambo ambalo kweli linaweza kuwa la kiuamuzi kwa Kanisa la siku zetu.
Kiini, moyo wa Njia hii ni ugunduzi mpya wa Pasaka, wa Mkesha wa Pasaka, ambao Papa Fransisko mwenyewe, kwa maaskofu wa Santo Domingo katika ziara yao ya “ad limina”, aliutambua kama sifa ya Njia ya Neokatekumenato. Mkesha huo ulizaliwa hapa, Fuentes. Kwa kweli, Kiko na Carmen, pamoja na jumuiya ya kwanza iliyozaliwa kati ya maskini wa vibandani, walithubutu kusherehekea Pasaka ya mwaka 1967—usiku kucha—, na baadaye, Siku Tatu za Pasaka, mwaka 1969. Pasaka pia imekuwa ya msingi katika kuunda mpangilio wa Neokatekumenato, ili kutia nguvu na msukumo kwa miaka hiyo ya kwanza ya Njia. Kwa uzuri na neema za Siku Tatu za Pasaka na Mkesha, upitishaji wa imani kwa familia zinazounda jumuiya umepata misingi yake.
Miaka michache baadaye, kuanzia Agosti 1 hadi 20, 1969—baada ya mwanzo wa Njia huko Italia—Kiko na Carmen walikutana tena hapa Fuentes, katika kuishi pamoja na ndugu wa kwanza waliozaliwa toka nafasi hizo za uinjilishaji. Na hapa ndipo kilipoundwa kikundi cha kwanza cha wamisionari wasafiri walioondoka kwenda Kolombia.
Kujenga upya kanisa hili la Fuentes— ambalo ni muhimu sana hivi kwa Kiko, kama alivyokumbusha katika salamu zake—ni kama kukumbuka miaka hii karibia 60 ya historia ya Njia: shukrani za lazima kwa Mungu ambaye, kutoka vibandani na kutoka Fuentes, amesukuma maisha ya Kiko na Carmen na yale ya wasafiri wa kwanza kwenye safari ambayo imepeleka ule “mwali wa mwanga” kwenye mabara yote matano na kuangaza kwa haya “mawe ya ulanga” ili ziwe ishara za matumaini katika ulimwengu wa leo kwa maelfu na maelfu ya watu.