
Njia ya Neokatekumenato imepokea habari za kuchaguliwa kwa Kardinali Robert Prevost kuwa Khalifa wa Petro kwa furaha kubwa. Maneno yake ya kwanza yametujaza furaha, akimweka Kristo Mfufuka kama kiini cha yote, ambaye anatupatia amani yake, pamoja na uinjilishaji unaozaliwa kutoka katika moyo wa kimisionari.
Kumekuwa na mwangwi wa pekee katika mioyo ya ndugu wote wa Njia—na hasa ule wa kwangu— kutokana na kwamba uchaguzi huu ulifanyika siku ya Bikira Maria wa Pompeii, kwa sababu Maria wa Pompeii amekuwa na umuhimu na uwepo wa pekee katika historia ya Njia ya Neokatekumenato. Mnamo 1968, mimi na Mtumishi wa Mungu Carmen Hernández tulipowasili Roma, tuliongozwa na Don Dino Torreggiani, mwanzilishi wa “Watumishi wa Kanisa,” ili kuweka miguuni pa Bikira Maria wa Pompeii utume ulioanza kati ya viabnda vya Palomera Altas, pembezoni mwa mji wa Madrid. Tangu wakati huo, matukio kadhaa ambayo yamekuwa yakitukia tarehe 8 Mei yameisindikiza Njia kwa namna ya pekee.
Wakati wa huduma yake ya uaskofu huko Peru, Mhashamu Prevost alipata pia fursa ya kukutana kibinafsi na kikundi cha wajibikaji wa Njia, pamoja na kuwasindikiza na kuongoza mkutano wa miito ambapo aliwahimiza vijana kuwa wamisionari wa Kristo.
Jina ambalo amejitwalia kama Mrithi wa Petro, Papa Leo XIV, limetukumbusha kwamba mtangulizi wake, Papa Leo XIII, alipaswa kuliongoza Kanisa katika nyakati ngumu kwelikweli, katika kutetea utambulisho wa kikristo.
Zaidi ya yote, Njia ni karama inayoweka kama kipaumbele utume kupitia Uanzishwaji wa Kikristo unaotolewa kwa majimbo na parokia; baadhi ya ishara halisi za hayo ni maelfu ya familia katika utume kwenye maeneo ambapo ukristo umetoweka zaidi, seminari za Redemptoris Mater, ambapo mapadre wanapata majiundo kwa ajili ya Uinjilishaji Mpya na huduma zote za kifamilia na kwa vijana. Tunayo furaha ya kuweza kuendelea, pamoja na Baba Mtakatifu huyu, kuweka karama hizi zote za Bwana kwa huduma ya Kanisa kwa ajili ya wema wa wanadamu wote, na hasa kwa wale “wengi waliobatizwa ambao hatimaye wanaishi… katika hali ya kumkana Mungu kwa matendo yao,” kama Papa Leo XIV alivyokumbusha katika mahubiri yake ya kwanza katika Kanisa la Sistine Chapel.
Tunamhakikishia Baba Mtakatifu sala zetu na za ndugu zetu wote ili huduma yake iweze kuzaa matunda yote ambayo mtu wa leo anayahitaji.
Kiko Argüello
Mei 8, Bikira Maria wa Pompeii
