Alizaliwa Ólvega (Soria) tarehe 24 Novemba 1930 na aliishi utotoni mwake huko Tudela (Navarra). Tangu alipokuwa mtoto, alisikia wito wa kimisionari , akivutiwa na roho ya Mt. Fransisko Ksaveri. Alisomea Sayansi za Kemia katika Chuo Kikuu cha Madrid. Kwa miaka kadhaa alikuwa sehemu ya “Taasisi ya Kimisionari ya Kristo Yesu” na alisoma Teolojia huko Valencia. Mwaka 1964 alimfahamu Kiko Argüello katika vibanda vya Palomeras Altas huko Madrid, na baada ya kuitangaza Injili kwa maskini ambao waliishi nao, Bwana aliwaongoza kwenye muundo wa kiteolojia-kikatekesi uliosimikwa juu ya Neno la Mungu, Liturjia, na Jumuiya, ambao ukawa msingi wa Njia ya Neokatekumenato, ambayo Statuta zake zilichapwa rasmi na Kiti Kitakatifu mwaka 2008. Askofu Mkuu wa Madrid wakati ule, Mhashamu Casimiro Morcillo, aliwapa moyo kueneza Njia hii katika maparokia. Kwa miaka zaidi ya 50, pamoja na Kiko Argüelllo, Carmen alitoa maisha yake akiitangaza Injili duniani kote. Alikuwa na upendo mkuu kwa Yesu Kristo, kwa Kanisa, kwa Bikira Maria, kwa Papa, kwa Liturjia, kwa Maandiko Matakatifu na kwa mizizi ya kiyahudi ya Ukristo. Alifariki huko Madrid mnamo tarehe 19 Julai 2016.