Ushuhuda wa Kiko Argüello. Pentekoste 2025

Naitwa Kiko Argüello na, pamoja na Mtumishi wa Mungu, Carmen Hernández, sisi ni waanzilishi wa Njia ya Neokatekumenato, utaratibu wa kijimbo wa uingizwaji wa kikristo ambao – kupitia katekesi, Neno la Mungu na sakramenti zinazoshirikiwa katika jumuiya – huwaongoza watu kuishi imani kipevu na ushirika wa kindugu.
Mimi ni mchoraji mhispania. Wakati wa miaka yangu ya chuo kikuu, baada ya dhahama kubwa ya kiutu, nilikuwa mkutano wa kina na Bwana, ambaye aliniita kuacha yote na kwenda kuishi kati ya maskini. Baadaye, Mungu amenipa nafasi ya kuweka sanaa yangu katika huduma ya uzuri mpya katika Kanisa. Nilienda kuishi katika vibanda pembezoni mwa mji wa Madrid, nikifuata nyayo za Mtakatifu Charles de Foucauld: kuishi maisha yaliyochika ya Kristo, kuishi kama Familia Takatifu ya Nazareti.

Carmen Hernández, mwanakemia na mwanateolojia, ambaye alikuwa akitafuta kikundi cha kwenda katika utume huko Amerika ya Kusini, alikutana na watu maskini ambao walikusanyika kwenye kibanda changu na alishangazwa sana hivi kwamba aliamua kukaa na kuishi katika kibanda kimoja karibu na chetu. Vibandani huko, tuliona jinsi Roho Mtakatifu alivyoumba ushirika kati ya wazururaji, wahalifu na watu wengine walioharibika sana. Tulishuhudia upendo usio na masharti wa Mungu uliodhihirishwa ndani ya Yesu Kristo kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu, ili kumtoa katika dhiki na dhambi. Uwepo huu wa Mungu katikati ya maskini, ndicho alichotaryarisha Roho Mtakatifu kwa Kanisa lake. Katikati ya maskini tumegundua muhtasariwa kipekee wa muunganiko wa teolojia na katekesi, ambao ndio utakuwa msingi wa Njia ya Neokatekumenato.

Ni njia ambayo Mungu amelipatia Kanisa lake, baada ya Mtaguso, kwa ajili ya kufungua ndani ya maparokia safari ya uingizwaji wa Kikristo, sawa na ile ya Kanisa la kwanza, kupitia hatua mbalimbali, ambapo mtu wa nyakati hizi anaweza kuzaliwa kwa maisha mapya ambayo Kristo mfufuka ameleta kwa kuja kwake. Safari hii ya malezi ya kikristo inafanyika katika jumuiya ndogondogo, kwa sura ya Familia Takatifu ya Nazareti, ili mbegu tuliyoipokea katika Ubatizo iweze kufikia ukomavu wake kamili.

Nikifikiria mkesha huu wa Pentekoste, nilijiuliza maswali kadhaa: Je, tunawezaje leo kumfikia mkanamungu asiye na imani tena? Maana yake nini kuwa mkristo? Maana yake nini kupenda? Injili inatukumbusha: “Mpendane kama vile mnavyopendana. Kwa upendo huu, wote watajua ya kuwa ninyi ni wanafunzi wangu” (taz. Yn 13:34). “…Mkiwa mmoja kikamilifu, ulimwengu utasadiki” (taz. Yn 17:21), mtu huyu aliyeduniaishwa atasadiki. Kwa hiyo basi, ni suala la kupenda kwa namna hii: upendo kwa adui. Kristo alijiachia kuuawa nasi na kwa ajili yetu, maadui zake: upendo kwa adui. Ili kuufikia upendo huu, hadi hatua ya kukomaa katika imani, tumegundua kwamba inahitajika kuanza safari ya uingizwaji wa kikristo katika jumuiya.
Nimechora picha ndogo ya Bikira Maria kwa sababu Njia hii imevuviwa na Bikira Maria Mtakatifu. Picha ya asili iko katika chumba kimoja cha Kathedrali ya Madrid. Kwenye picha hii imeandikwa: “Inabidi kufanya jumuiya za kikristo kuwa kama Familia Takatifu ya Nazareti, zinazoishi katika unyenyekevu, urahisi na sifa. Mwingine ni Kristo”. Inabidi kuunda jumuiya ambamo wakristo wanaweza kupevuka, ili watimize utume wao katika ulimwengu uliopoteza ono la Mungu na kuwa Mwili wa Kristo mfufuka, ambapo mwingine ni Kristo.
Njia hii, kama uingizwaji wa Kikristo, huunda jumuiya za Kikristo katika parokia, zinazoundwa na familia, vijana, wazee, watu wa karibu na wa mbali na Kanisa, na inashiriki pamoja na majimbo yao katika tukio la Jubilei katika taratibu zake mbalimbali, wakiamini kwamba mwaka huu ni wakati mwafaka na wenye neema ya pekee kwa ajili ya kuwa na mkutano wa dhati na Yesu Kristo, ambao utatupatia sisi na ulimwengu wa leo tumaini hilo linalohitajika sana hivi.
Njia ya Neocatekumenal imeinuliwa na Roho Mtakatifu, kama vile Mapapa hao wote wamethibitisha, ili kulisaidia Kanisa katika uinjilishaji wa Milenia ya Tatu. Tumejaa na shukrani tele kwa Bwana na kwa Bikira Maria, aliyetaka Njia hii izaliwe, kwa ajili ya kuchaguliwa kwa Papa mpya, Leo XIV. Tegemezo la Mapapa daima limekuwa la msingi katika maendeleo ya Njia hii.
Katika Njia wapo vijana wengi sana, na bila shaka Jubilei inayosubiriwa zaidi ni ile ya vijana, mwanzoni mwa Agosti. Maelfu ya vijana watawasili huko Roma wakisindikizwa na makatekista na maaskofu wao. Baada ya kukutana na Papa, watakuwa na mkutano wa miito pamoja nasi ili kusaidiwa katika upambanuzi wa kutambua wito wao. Hakika maneno ya Papa Leo XIV, aliyoyatoa kwenye wosia wake wakati wa sala ya Malkia wa Mbingu (“Regina Coeli” ) katika Siku ya Miito Ulimwenguni: “Msiogope”, yatazaa matunda mengi.

