Tafsiri yetu ya makala iliyochapishwa kwa idhini ya Vatican News

Kutokana na hafla ya Jubilei ya Familia, simfonía zote mbili za mwanzilishi wa Njia ya Neokatekumenato, zilipigwa pamoja kwa mara ya kwanza jioni ya Juni 1, 2025, kwenye “Auditorio Parco della Musica” (“Ukumbi wa Bustani ya Muziki”)huko Roma: Monsinyori Fisichella asema: simfonia ya aina hii imetufundisha kuwa sisi si watazamaji bali washiriki.

Débora Donnini – Mji wa Vatikano 

Ni muziki unaozama katika mateso ya Kristo na ya Bikira Maria miguuni pa Msalaba, na wakati huo huo unaandika moyoni uhakika wa Ufufuo. Ushiriki wa kila mtu uliohisiwa baada ya kusikia Kazi ya Kisimfonia za Kiko Argüello, msanii mhispania na mwanzilishi wa Njia ya Neokatekumenato pamoja na Mtumishi wa Mungu Carmen Hernández, ulikuwa wenye nguvu na wa moja kwa moja. Ushiriki ulioelezwa si tu kupitia makofi yalilyopigwa mara nyingi, lakini juu ya yote kupitia ushiriki wa wasikilizaji wenyewe wakati wa kuimba kiitikio pamoja na kwaya.

Jana, katika Ukumbi wa Parco della Musica huko Roma, kazi mbili za kisimfonia za Kiko ziliimbwa kwa pamoja kwa mara ya kwanza: Mateso ya Wasio na Hatia, wimbo uliotolewa kwa ajili ya uchungu wake Mama wa Kristo, na Masiya, kwa heshima ya wafiadini wa leo. Mwongoza orkestra ya Njia ya Neokatekumenato , inayojumuisha wanamuziki 100 —wapiga ala na mpiga kinanda mmoja, Claudio Carbó— pamoja na wanakwaya 120, ni Tomáš Hanus, Mwongoza Orkestra ya Kisimfonia ya Iceland.

Tukio hilo likawa sehemu ya Jubilei ya Familia, na tafakari za mtunzi wa Kazi ya Kisimfonia, Kiko Argüello, katika kuingizia sehemu ya kwanza, zinaanza haswa kutokana na ukweli huu: katika nchi za Magharibi, anasisitiza, upweke unakuwa ugonjwa mkuu kuliko yote. Katika ulimwengu uliojaa talaka, utoaji mimba, na euthanasia (“kifo cha huruma”): “Mungu anaziita familia za Kikristo, kwa mfano wa Familia Takatifu ya Nazareti, kumleta Kristo kwa wanadamu”. ” Kutoka familia huzaliwa mustakabali wa mataifa,” alisisitiza Papa Leo XIV katika homilía yake kwenye Misa ya Jumapili asubuhi, tarehe 1 mwezi Juni . Kiko alirudia maneno hayo ya Papa, ambayo yalipokelewa na makofi mengi kutoka kwa waliohudhuria.

Baada ya hapo, aliwakumbusha uvuvio aliopokea kutoka kwa Bikira Maria: “Inabidi tufanye jumuiya za kikristo kama Familia Takatifu ya Nazareti, zinazoishi kwa unyenyekevu, urahisi, na sifa: mwingine ni Kristo”. Njia ya Neokatekumenato ilizaliwa kama uingizwaji wa Kikristo kwa lengo la kugundua hazina za Ubatizo, ambao unawaongoza kuutekeleza katika jumuiya ya mapendano. “Mpendane kama nilivyowapenda ninyi, kwa upendo huo ili watu wote watakua ya kuwa ninyi ni wanafunzi wangu,” yaani, ninyi ni wakristo. Huu, Kiko anasisitiza, ndio utume wa familia za kikristo, utume wa kieskatologia (yaani, utume unaoangalia mustakabali wa mtu): kuonyesha kwa ulimwengu kwamba upendo upo.”

Mateso ya Wasio na Hatia 

Simfonia ya kwanza ilizaliwa kutokana na maang’amuzi aliyoyaishi Kiko katikati ya miaka ya 1960 alipoenda kuishi kati ya maskini mitaa ya vibanda ya Madrid, akivutiwa na mateso ya watu wengi wasio na hatia, akaelewa kwamba jibu pekee la kweli kwa mateso ni Bwana Yesu.

Kazi hii ilifanyika kwa mara ya kwanza mnamo 2011 katika Nchi Takatifu, katika kituo cha Domus Galilaeae, kwenye Mlima wa Heri, na baadaye katika kumbi zilizo muhimu zaidi, kumbi za tamasha, viwanja na Kathedrali mbalimbali ulimwenguni kote: kutoka kwa Kathedrali ya Madrid hadi New York Metropolitan, kutoka Suntory Hall ya huko Tokyo hadi kwa Ukumbi wa Gerard Behar huko Yerusalemu hadi Ukumbi wa Paulo VI huko Mji wa Vatikano, hapo yakiwa baadhi tu ya maeneo.

Inajumuisha sehemu tano zinazotofautiana kwa misisitizo tofauti tofauti katika ala za muziki: “Gethsemane,” ambapo ngoma inatukumbusha kwamba Yuda anakaribia. Kisha, “Ombolezo” kwa kinubi; “Uwasamehe,” na “Upanga,” zinazohusu mateso ya Bikira Maria, ambapo wasikilizaji wote husimama na kuimba pamoja na kwaya, “Maria, Mama wa Mungu.” Inahitimisha kwa “Resurrexit.”

Masiya

Baada ya simfonia ya kwanza, Kiko amewasilisha ya pili, Masiya. ambayo ilizinduliwa mwaka 2023 katika Teatro Verdi huko Trieste, Italia, na inahusu hasa Mateso na maumivu ya Kristo na imetolewa kwa ajili ya wafiadini wa leo. Kiko anasisitiza: “Sisi wakristo, siku zote tunabeba ndani ya miili yetu namna ya Kristo kufa, kwa sababu tumefundishwa kunyosha mikono yetu msalabani: katika ndoa, kazini, pamoja na watoto wetu, pamoja na babu na babu zetu, pamoja na jumuiya, na kila mtu. Siku zote tukibeba ndani ya miili yetu kifo cha Yesu, ili ionekane ndani yetu kwamba Kristo yu hai.” Kiko anatukumbusha kwamba “mkristo ameitewa kupenda kwa namna ya msalaba, upendo kwa adui.”

Sehemu tatu za shairi zinasisitiza hilo kwa usahihi. Sehemu ya kwanza inaitwa Akedah na inarejelea sura ya Isaka ambaye, kulingana na mapokeo ya kiyahudi, anamwomba baba yake Abrahamu afungwe ili asiasi wakati wa kutoelwa sadaka. Kisha, inafuata Binti za Yerusalemu, ambayo inakumbuka maneno ambayo, kulingana na mwinjili Luka, Yesu aliwaambia wanawake wanaomtazama anapopita katikati ya mji baada ya kupigwa mijeledi Ili kusisitiza drama ya wakati huu, Kiko anamrejelea mtunzi wa Enzi za Kati za Uhispania Tomás Luis de Vitoria.

Hatimaye, sehemu ya mwisho inasimama juu ya maneno ya mfiadini kutoka karne ya 4, Victorinus wa Pettau: “Masiya, simba kwa kushinda, alijifanya mwanakondoo ili ateseke,” kwa sababu, Kiko anakazia, “sote tungepaswa kujifunza kuwa wanakondoo ili tuteseke,” tunaoitwa kuonyesha Upendo wa Kristo, unaoshinda Mauti. Pia inaongezwa nukuu kutoka kwa Mtakatifu Quodvultdeus, askofu wa Karthago kutoka karne ya 5, aliyesema: “Alipanda msalabani ili awe bwanaarusi, kwa ajili ya kufa. Na damu yake ameitoa, kuwa mahari kwa Bibi Arusi wake Bikira”.

Hivyo, swala ni upendo huo “ambao Kristo anaweka ndani ya kila mmoja wetu kwa njia ya Roho Mtakatifu.” Kisha kwaya inahitimisha kwa wimbo wa ushindi, shangilio ya furaha, Aleluya ya Pasaka.

Fisichella: simfonia inayoongoza na kutupeleka kutenda

Hafla hiyo iliandaliwa na Assunta Cannata, ambaye alikuwepo pamoja na Kiko Argüello, Padre Mario Pezzi na Ascensión Romero, Kikundi cha ya Kimataifa cha Njia ya Neokatekumenato, pamoja na Askofu Mkuu Monsinyori Rino Fisichella. Naibu Mkuu wa Idara ya Uinjilishaji, kitengo cha masuala ya msingi juu ya uinjilishaji duniani.

Monsinyori Fisichella alisema kwa vyombo vya habari vya Vatikano kwamba “Simfonia hii, kwanza kabisa inadhihirisha ustadi wa Kiko na uwezo wake wenye sura nyingi: anahama kutoka kwa uchoraji hadi muziki kwa urahisi wa ajabu, akijua wazi pia kwamba anafanya kazi ya uinjilishaji. Ninaamini hiki ndicho kipengele kinachopaswa kutiliwa mkazo. Katika uinjilishaji, njia za uzuri wa sanaa -uimbaji, uchoraji, maandishi- zote ni namna za kipekee kwa ajili ya kueleza na kufikisha tangazo la Injili ambayo ni tangazo la Fumbo la Kifo na Ufufuko wa Yesu.”

Askofu mkuu anakumbusha kwamba “hakika mwanzo wa simfonia lazima ueleze Gethsemane, ukimya wa mateso,” huku kwa upande mwingine ipo furaha ya mwisho ya Ufufuo, “tangazo la utukufu.” “Hivyo”, anasisitiza, “kwa mara nyingine tena, kwa simfonia ya aina hii tunafundishwa kwamba sisi si watazamaji bali washiriki. Kwamba wasikilizaji wote waalikwe kusimama na kujiunga na sauti zao na za kwaya ilinikumbusha Simfonia ya Tisa ya Beethoven, ambapo kwaya iliingizwa katika orkestra kwa mara ya kwanza. Hapa Kiko hajaingiza tu kwaya, bali wasikilizaji wote. Tunayoishi ni simfonia ambapo kuna utendaji, hisia yenye shauku, pamoja na ushiriki kutoka kwa wale wanaohudhuria, ni hisia ya kutojisikia kutengwa, bali kuhusishwa kutoka ndani ya tangazo hili linalotolewa”.

Inafaa pia kuangazia kwamba Kazi hii inafanywa wakati wa Jubilei ya Familia. Katekista alidokeza hilo kwa kukumbuka maneno ya Leo XIV. Alisisitiza pia kwamba “tunaishi, hasa katika nchi za Magharibi, dhahama ya familia”. “Katika jamii ambapo teknolojia inatawala, ikiwa familia haitapata tena nafasi yake, ikiwa haitakuwa kiini cha msingi wake, nembo ya uhalisia ambapo kila mmoja anajihisi kukaribishwa, ambapo hakuna mmoja anayehisi kuwa peke yake, basi lazima tuseme kwamba hatutembei katika njia ya maendeleo kwenda mbele, bali ya kurudi nyuma.” “Kanisa”, yeye anasisitiza, “linapaswa lifanye lolote liwezekanalo ili kutimiza wajibu wake wa kinabii kuhusu familia”, likiiweka kama kiini cha uchungaji wake na likifanya kwamba ulimwengu, jamii, na utamaduni vielewe kwamba ikiwa familia inawekwa kando, hakuna mwelekeo wa kweli ambao mtu anaweza kuelekezwa, “badala yake, kuna hali ya kujiangalia tu; hali ya kufungwa katika tekinolojia bila familia inapoteza kile kipimo cha cha ubinadamu wa kina, ambao mtu wa leo ana haja kubwa nao.”

Ouellet: utulivu na tumaini katika muziki huu

Kwa upande wake, Kardinali Marc Ouellet, Mkuu Mstaafu wa Idara kwa ajili ya Maaskofu anasisitiza kwamba sehemu ya kwanza ya Kazi ya Kisimfonia“ inazungumza juu ya hadhi ya mateso. “Kinachonishangaza,” anasema kwa vyombo vya habari vya Vatikano, “ni utulivu na matumaini vilivyomo katika muziki huu; upo ushindi wa Mfufuka”: inagusia mada yenye huzuni nyini, “lakini muziki wake si wa kuhuzunisha, hata pale ambapo yanapoonekana maombolezo; yanaonekana kufunikwa na melodia yenye uwiano, na hii inanishangaza sana, kibinafsi”.  Kuhusu sehemu ya pili, yeye anakumbusha kwamba mada ni tofauti: “Hii inatafakarisha zaidi juu ya dhambi, juu ya ushuhuda wetu mdhaifu, lakini yote haya daima yakipenyezwa na kipaji cha Msulubiwa. Hicho ndicho kinachotawala.

Kwa ujumla, “muziki umenivutia kwa sababu ya mahadhi yake ya kiyahudi na kihispania; kuna aina ya mchanganyiko wa midundo na melodia, mchanganyiko ulio muhtasari mzuri na wa kina… Ninaelewa kwa nini Wayahudi walijiona kusikika”, anasema Kardinali, kwa sababu marabi wengi pia wamehudhuria katika sehemu mbalimbali za dunia ambako imeimbwa. Kuhusu familia, anasisitiza kwamba “nguvu ya karama ya Neokatekumenato ni familia” na kwamba “utume wa Kanisa unapaswa kuingia kupitia familia.”

Kwa hivyo, ni simfonia ambayo kutoka mitazamo tofauti tofauti, kwa upande wa katekesi na wa kisanii, inatafsiriwa, kwanza kwa kugusa moyo wa kila mtu binafsi, kwenye njia ya uinjilishaji.

Share: