Madrid. Kardinali Cobo Cano ataongoza Misa Takatifu katika maadhimisho ya miaka 60 ya Njia ya Neokatekumenato na Tukio la kufunga awamu ya kijimbo ya mchakato wa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Carmen Hernández kuwa mwenye heri.

Siku ya Jumamosi, Mei 30, saa 2:00 usiku, Kardinali José Cobo Cano, Askofu Mkuu wa Madrid, ataongoza adhimisho la Ekaristi katika Kathedrali ya Bikira Maria Mama Yetu wa Almudena, ili kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 60 ya Njia ya Neokatekumenato. Maaskofu kadhaa na mapadri zaidi ya 100 wataadhimisha kwa pamoja. Hili ni tukio la furaha kwa Njia nzima ya Neokatekumenato: safari hii ya Uingizwaji wa Kikristo, inayotekelezwa katika jumuiya ndogo na kwa sasa imeenea katika parokia zaidi ya 6,250 katika majimbo takriban 1,400 duniani kote, na ambayo ilianzia katika moja ya maeneo maskini zaidi ya mji mkuu wa Hispania (Madrid).

Baada ya hapo, Jumanne, Juni 2 saa 2:00 usiku, litafanyika tukio la kufunga awamu ya kijimbo ya mchakato wa kutangazwa mwenye heri na kutangazwa mtakatifu kwa Mtumishi wa Mungu Carmen Hernández Barrera katika Seminari ya Redemptoris Mater huko Madrid. Awamu hii, iliyoanza katika mji mkuu wa Hispania (Madrid) mnamo Desemba 4, 2022. Tukio hili litaongozwa na Askofu Mkuu wa Madrid, Kardinali José Cobo Cano. Pia watahusika katika tukio hilo, Carlos Metola, mwombaji rasmi wa awamu hiyo ya kijimbo, na Kiko Argüello, mwanzilishi wa Njia ya Neokatekumenatom pamoja na Carmen Hernández, aliyeshirikiana naye katika uinjilishaji kwa miaka zaidi ya 50. Mara tu awamu ya kijimbo itakapokamilika, hati zitatumwa kwa Idara ya Kipapa ya Michakato ya Watakatifu kutangazwa, na mchakato utaendelea katika “awamu ya kirumi”.

Carmen alifariki akiwa na umri wa miaka 85 mnamo Julai 19, 2016, huko Madrid, baada ya kuugua kwa muda mrefu na maisha yaliyowekwa wakfu kwa kujitolea bila masharti kwa huduma ya Injili, kama vile alivyotamani tangu utotoni. Tukio la tarehe 2 Juni hufanyika karibu miaka kumi baada ya kifo chake na litafanyika mahali pale pale alipozikwa. Hadi sasa, zaidi ya watu 118,000 wametembelea kaburi lake, na neema na fadhila kadhaa zinapokelewa kila mara kupitia maombezi yake. Mchango wa Carmen Hernández ulikuwa wa kimsingi kwa Njia ya Neokatekumenato, kutokana na masomo yake kuhusu upyaisho wa Mtaguso wa Pili wa Vatikano. Mchango huu ulionekana wazi katika nyanja nyingi: uundaji wa jumuiya ndogo za kikristo, liturujia, Pasaka, uhusiano na Neno la Mungu, Agano la Kale likiwemo, na chemchemi za imani katika mababa wa Kanisa na mizizi ya kiyahudi ya imani ya kikristo.

Mang’amuzi ya Njia ya Neokatekumenato yalipiga hatua zake za kwanza halisi katika vibanda vya Palomeras Altas, huko Madrid, ambapo Kiko na Carmen walikutana katikati ya miaka ya 1960.

Hakika, mnamo Novemba 1964, Kiko alipokuwa mchoraji kijana, aliacha kazi yake na akiona katika mateso ya wasio na hatia fumbo la Kristo aliyesulubiwa, na kwa kufuata nyayo za Mtakatifu Charles de Foucauld—aliyetaka kuishi maisha yaliyofichwa ya Yesu huko Nazareti— aliamua kwenda kuishi miongoni mwa walio maskini zaidi, katika kibanda kimojawapo nje kidogo ya Madrid. Wakimzunguka, alipokuwa akisali, akipiga gitaa, na kusoma Biblia, walikusanyika polepole “gypsies”, wahalifu, na watu waliotengwa na jamii waliosikiliza tangazo la kerygma.

Jeshi la Wananchi lilipofika Agosti 1965 kubomoa vibanda, Kiko alifanikiwa kumpigia simu Askofu Mkuu wa Madrid, Mons. Casimiro Morcillo, ambaye alikuja mara moja na kusimamisha ubomoaji. Askofu Mkuu aliguswa sana kuona “jumuiya” hiyo ndogo ya watu maskini kama hao wakisali. Upendo na umakini ambao Carmen aliona kwa Mons. Morcillo ulimshawishi kushirikiana na Kiko, kwani aliona kwamba jumuiya hiyo, ambayo ilikuwa imeundwa bila mpangilio wowote miongoni mwa maskini, ilikuwa kazi ya Mungu. Ilikuwa ni Askofu Mkuu mwenyewe aliyewatia moyo kuleta Uingizwaji huo wa kikristo katika parokia za Madrid; na kwa hivyo, mnamo 1966, katekesi zilianza katikati ya Madrid. Lakini mang’amuzi ya huko vibandani ndiyo yalitengeneza “kitalu” ambamo safari hii ya ugunduzi mpya wa Ubatizo iliainishwa, iliyosimama juu ya “miguu mitatu” ya “Neno, Liturujia na Jumuiya”, na inayong’amuliwa, kwa sababu hiyo hiyo, katika jumuiya ndogo ambapo upendo kwa jirani unaonekana.

Hivyo, katikati ya miaka ya 1960, bila mipango ya awali na katika muktadha wa kutengwa, Uingizwaji huu wa Kikristo kwa watu wazima ulizaliwa. Leo, umeenea katika mataifa 138 katika mabara yote matano, ukiwa na jumuiya zaidi ya 20,350. Katika kipindi hiki cha miaka sitini, mamia ya familia, pamoja na watoto wao, wametoa maisha yao kwa uinjilishaji, wakiacha usalama wao wenyewe, hivyo wakiiwezesha Injili kufikia miisho ya dunia. Hivi sasa, familia zipatazo 2,000 zinaendelea na kazi hiyo ya kuwasaidia maaskofu na maparoko, wakihudumu kama makatekista wasafiri au wamisionari katika maeneo maskini sana, au kama wale waliotumwa kwa njia ya ad gentes (Utume kwa Watu wa Mataifa) katika maeneo yaliyopoteza zaidi Ukristo au ambayo hayajawahi kuinjilishwa ipasavyo. Miongoni mwa matunda ya mkondo huu wa kikanisa pia zipo seminari 116 za kijimbo za kimisionari Redemptoris Mater, ambapo zaidi ya mapadre 3,400 wamelelewa; mamia ya watawa wa maisha ya kitaamuli, pamoja na wamisionari wengi waseja, wa kiume na wa kike. Statuta (Sheria) za Njia ya Neokatekumenato ziliidhinishwa dhahiri na Vatican mnamo 2008 na Mwongozo wao wa Katekesi ulifuata mnamo 2010.

Share: